James Lembeli
MWENYEKITI wa Kamati ya Maliasili na Mazingira, James Lembeli,
amesema wanaokamatwa na kuhusishwa na utoroshwaji wa nyara za serikali
nje ya nchi ni vidagaa huku makambare yakiachwa.
Lembeli alitoa kauli hiyo jijini Dar es Salaam jana na kupongeza
juhudi za Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, kwa
kufanikisha kukamatwa kwa majangili hao.
“Waliokamatwa na wanaoendelea kukamatwa ni vidagaa, lakini makambare
wameachwa, ingawa wanajulikana sasa ni vema wakakamatwa wahusika wenyewe
na sio hao watumwaji,” alisema Lembeli.
Lembeli ambaye pia ni mbunge wa Kahama, alishauri ni vema operesheni
ya Tokomeza Majangiri ikaendelea baada ya wao kumaliza uchunguzi na
kubaini kasoro zilizojitokeza katika operesheni hiyo.
Alisema dunia nzima kwa sasa inapingana na kitendo cha ujangili na
wanaiunga mkono operesheni iliyoanzishwa nchini hivyo ni vema pia
serikali na wadau wengine mbalimbali wakaunga mkono juhudi hizo.
Hivi karibuni shehena yenye urefu wa futi 40 ilinaswa Zanzibar ikiwa
na nyara za serikali ambapo hadi sasa watuhumiwa watano wamekamatwa huku
uchunguzi ukiwa unaendelea kubaini wengine.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment