WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki,
amekamata kontena la futi 40 likiwa limesheheni pembe za ndovu kisiwani
Unguja, Zanzibar jana alasiri.
Akizungumza na gazeti hili kwa simu jana kutoka kisiwani humo, Waziri
Kagasheki alisema kuwa kontena hilo lilikuwa likitokea Bandari ya Dar
es Salaam na kwamba watu wawili wanashikiliwa kwa mahojiano zaidi
wakilisaidia Jeshi la Polisi.
Waziri Kagasheki alisema kuwa hadi sasa haijulikani mzigo huo una
thamani kiasi gani na kwamba unasadikiwa kumilikiwa na raia wa China.
Alisema kuwa operesheni hiyo ni endelevu ili kuwabaini wahusika wanaojihusisha na biashara hiyo haramu ya ujangili.
Tukio hilo linakuja zikiwa ni wiki mbili tangu waziri huyo kukamata
pembe za ndovu 706 jijini Dar es Salaam zikimilikiwa na raia wa China.
Pembe hizo 706 ni sawa na tembo 353 waliouawa katika hifadhi za wanyamapori hapa nchini.
Wachina hao walikamatwa katika Mtaa wa Kifaru, Mikocheni wilayani
Kinondoni chini ya operesheni iliyoongozwa na Waziri Kagasheki, ambaye
aliambatana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Tarish
Maimuna.
Waliokamatwa na shehena hiyo ya pembe za ndovu ni raia watatu wa
China, ambao ni Xu Fujie, Chen Jinzha na Huang Qin wote kutoka mji wa
Guandung, ambao wamefikishwa mahakamani wiki iliyopita.
0 comments:
Post a Comment