Rais Jakaya Kikwete
Rais Jakaya Kikwete ameitaka Wizara ya Nishati na Madini kuacha
urafiki wa dhambi na baadhi ya wachimbaji wakubwa wanaohodhi maeneo
makubwa na badala yake wazingatie sheria ili kutoa haki kwa wachimbaji
wadogo.
Akizungumza katika siku yake ya mwisho kutembelea
Mgodi wa Dhahabu wa Baraka uliopo wilayani Geita katika Kijiji cha
Nyaruyeye juzi, Rais Kikwete alisema kilio cha wachimbaji wadogo hivi
sasa ni maeneo lakini wanaweza kuchimba sawa na wachimbaji wakubwa hivyo
kuitaka wizara hiyo kuzingatia sheria kwa kuwafutia umiliki wenye
maeneo ambayo hawayafanyii kazi.
“Mkiyatwaa watapiga kelele, acheni wapige kelele
lakini timizeni sheria. Masele (akimwangalia Naibu Waziri Nishati na
Madini Stephen Masele) na wenzako lazima mzingatie sheria.
Wanyang’anyeni maeneo haya wapeni wachimbaji wadogo wachimbe. Acheni
kufanya urafiki wa dhambi na hawa,” alisema Rais Kikwete.
Rais Kikwete ambaye alieleza kufurahishwa kwake na
wachimbaji wadogo kuanza kuchimba kisasa alisema sheria ya umilikaji wa
maeneo ya utafiti na uchimbaji wa madini inaelekeza kuwa iwapo mwombaji
akija kuomba tena (renewal) leseni ya eneo alilopewa anapaswa
kulipunguza kwa asilimia 50 ili wapewe wengine na vivyohivyo anapokuja
kwa mara ya pili, pia anapaswa kupunguziwa eneo lake kwa asilimia 50.
“Pamoja na kwamba sheria ipo wazi, ukiwauliza
wizara kwa nini hawafanyi hivyo, hawana maelezo wapo kimya, sijui
wanaingia kigugumizi gani kutimiza sheria hii. Wanaposhindwa kufanya
haya ni hasara kwa taifa maana haya madini hayachimbwi, wangezingatia
sheria hii na kuchukua maeneo haya wangewapa wengine wakachimba leo
tusingekuwa na kelele za wachimbaji wadogo,” alisema.
Rais Kikwete alisema madini yakiwa chini hayana thamani yoyote mpaka yanapochimbwa na kubainisha kwamba iwapo watu waliopewa leseni watazishikilia bila ya kuendeleza maeneo yao, watakwamisha ajira na maendeleo kwa nchi.
Rais Kikwete alisema madini yakiwa chini hayana thamani yoyote mpaka yanapochimbwa na kubainisha kwamba iwapo watu waliopewa leseni watazishikilia bila ya kuendeleza maeneo yao, watakwamisha ajira na maendeleo kwa nchi.
Aidha, aliitaka wizara hiyo kuwa makini wakati wa
kutimiza matakwa ya sheria hiyo ya umiliki wa maeneo ya uchimbaji,
akitahadharisha kuwa wamiliki wengine wanaweza kubadili majina pindi
watakaponyang’anywa maeneo yao.
“Wana tabia ya kubadili majina, mkimnyang’anya
atakuja upya. Kama alikuwa anaitwa Kikwete & Sons sasa atakuja tena
anajiita SK lakini ndiye huyohuyo, tazameni sana. Najua, mnayajua mengi
maana na ninyi ni wabia wao lakini ninachotaka ni kuzingatia na
kusimamia sheria,” alisema.
Akizungumzia Mgodi wa Mzawa alioutembelea, Rais
Kikwete alisema amejionea jambo kubwa na la kushangaza kiasi cha kusema
kwamba iwapo angeishia kusimuliwa mambo hayo na watu bila ya kufika,
asingeamini kama Watanzania wanaweza kuendesha migodi kama huo.
Alisema Serikali inathamini mchango wao na
kuwataka kujiandikisha Tume ya Uwekezaji ili nao waweze kuomba msamaha
wa mafuta na zana mbalimbali kama ilivyo kwa wawekezaji wakubwa wa nje.
Awali, Masele alimwomba Rais kuangalia uwezekano
wa kuwapatia wachimbaji wadogo msamaha wa kodi akisema vifaa
wanavyotumia havina tofauti na vile vya wachimbaji wakubwa.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment