JESHI la Polisi limeonyesha wazi kuwa halina
dhamira ya dhati ya kuwasaka na kuwatia nguvuni wahalifu waliowateka,
kuwatesa na kuwaumiza vibaya Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri nchini
(TEF), Absalom Kibanda, na Mwenyekiti wa Jumuia ya Madaktari, Dk. Steven
Ulimboka.
Ni zaidi ya mwaka mmoja na miezi minne tangu Dk. Ulimboka atendewe
unyama huo lakini hadi leo suala hilo limegeuzwa sinema na jeshi hilo
kwa kumkamata mtu asiyehusika ambaye baadaye walilazimika kumwachia
huru.
Hivi ndivyo imetokea pia kwa Kibanda ambaye ni Mahriri Mtendaji wa
Kampuni ya New Habari (2006), kwani tangu ateswe na kung’olewa jicho,
kucha, meno na kukatwa kidole, hakuna mtuhumiwa hata mmoja aliyekamatwa
ikiwa ni zaidi ya miezi saba sasa.
Lakini jana Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk. Emmanuel Nchimbi,
akiongozana na maofisa wengine wa jeshi hilo akiwemo Kamishna wa Kanda
Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, waliitisha mkutano na waandishi
kuwataja ‘vibaka’ waliokamatwa wakihusishwa kumshambulia na kumwibia
Dk. Sengondo Mvungi.
Dk. Mvungi ni mjumbe wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba ambaye alivamiwa
na majambazi hao takriban wiki mbili zilizopita na kukatwa mapanga na
kuporwa kompyuta mpakato (laptop) na fedha.
Kwa sasa hali yake ni mbaya akiwa bado hajitambui na hivyo kulazimika
kupelekwa nchini Afrika Kusini kujaribu kuokoa maisha yake.
Hatua ya Waziri Nchimbi kujitokeza jana kuzungumzia tukio hilo na
kuonyesha juhudi za haraka za kuwanasa watuhumiwa, iliwasukuma waandishi
wa habari kuhoji kulikoni matukio ya Ulimboka na Kibanda yamewekwa
kiporo.
Kama kawaida yake, Kamishna Suleiman Kova alijibu kuwa kila tukio lina
mazingira yake, hivyo tukio la Mvungi halifanani la Kibanda wala Dk.
Ulimboka na kueleza kuwa mfumo wa suala hilo kiupelelezi unakwenda
vizuri.
“Tukio la Mvungi na la kina Kibanda na Ulimboka mazingira yake ni
tofauti; unapeleleza halafu unatuhumiwa wewe mwenyewe, ila
watapatikana,” alisema Kova.
Katika taarifa yao hiyo, Dk. Nchimbi na Kova walisema kuwa wamekamatwa
watuhumiwa wengine watatu zaidi wanaodaiwa kumvamia, kumjeruhi kwa
mapanga na kumpora mali Dk. Mvungi.
Kova alisema kuwa operesheni ya kuwasaka waliomshambulia Dk.Mvungi
imefanikiwa kwa asilimia zaidi ya 80 ambapo mpaka sasa wamekamatwa watu
tisa wakiwa na vifaa walivyotendea uhalifu huo ambavyo ni mapanga
matano, simu ya mkononi na kigoda.
Aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Msigwa Kopelo, Chibango Magozi, Ahmed
Ally, Zakaria Rafael (23) dereva wa boda boda, Manda Salowaa ( 40),
Paulo Jailos (29), Juma Hamisi (29), Longishu Semaliki (29) muuza ugoro
Vingunguti na Masunga Makenza (40).
Dk. Mvungi ambaye pia ni mshauri wa masuala ya kisheria wa Chama cha
NCCR-Mageuzi alipatwa na mkasa huo usiku wa kuamkia Novemba 3, mwaka
huu, akiwa nyumbani kwake Kibamba Msakuzi, Manispaa ya Kinondoni jijini
Dar es Salaam.
Baada ya kumjeruhi waliiba sh milioni moja, bastola, simu mbili za mkononi na kompyuta mpakato (laptop).
Utendaji huu wa jeshi la polisi unaacha mashaka makubwa hasa kwa
matukio makubwa ya utekaji na utesaji ambayo ni mageni nchini, kwani
uchunguzi wake wa kuwasaka watuhumiwa unalegalega.
Itakumbukwa kuwa mara tu baada ya tukio la Dk. Ulimboka Julai 26 mwaka
jana, jeshi hilo liliunda kikosi kazi kilichowashirikisha wataalamu
mbalimbali wa kanda maalumu na makao makuu.
Hadi sasa ripoti yake haikuwahi kutolewa hadharani kama Kova
alivyojigamba wakati akiitangaza, badala yake hivi karibuni amekuwa
akitupiana mpira na wakuu wake kuhusu ripoti hiyo.
Dk. Ulimboka kwa kiapo aliwataja watu aliowatuhumu kuhusika na tukio
hilo, mmoja wao akiwa ni ofisa usalama wa taifa-Ikulu lakini hakuwahi
kufanyiwa gwaride la utambuzi wala kuhojiwa na kamati hiyo ya uchunguzi.
Siku chache kabla ya Dk. Ulimboka kumtaja ofisa huyo, gazeti la
MwanaHalisi lilichapisha habari iliyoeleza tukio zima lakini serikali
ikalifungia kwa muda usiojulikana kwa kile kinachoitwa kosa la
uchochezi.
Tukio hilo la Dk. Ulimboka limekuwa kama sinema kwani hata mtuhumiwa
pekee raia wa Kenya, Joshua Mulundi, aliyekuwa amekamatwa na kuwekwa
ndani kwa muda kadhaa na kufunguliwa kesi, ukamatwaji wake ulikuwa wa
kutia mashaka.
Wakati vinywa vya wananchi vikiwa bado vinatafakari unyama huo, tasnia
ya habari nayo iliingiliwa kwa kushambuliwa kiongozi wa wahariri katika
tukio kama lilelile la Dk. Ulimboka.
Matukio haya ni kama ya kupangwa kutokana na kufanyika kwa ustadi wa
hali ya juu na kwa muda mfupi tena bila wahusika kuchukua chochote kwa
mteswaji.
Kama ilivyokuwa kwa Dk. Ulimboka, pia kwa Kibanda, iliundwa kamati ya
uchunguzi iliyoongozwa na wataalam wakiwemo walewale walioshindwa
kuwakamata watesaji wa Dk. Ulimboka.
Hadi leo hakuna mtuhumiwa hata mmoja ametiwa nguvumi na jeshi la
polisi ambalo kila siku viongozi wake wamekuwa wakijinasibu kuwa na
intelijensia ya hali ya juu inayobaini matukio ya kihalifu kabla ya
kutokea, mathalani kuzuia maandamano na mikutano ya vyama kwa madai ya
kuepusha vurugu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment