chademaleo2_0eecc.jpg
Mwanasheria Mkuu wa Chadema, Mhe. Tundu Lissu akieleza maazimio ya Kamati Kuu ya Chadema kwa wanahabari (hawapo pichani).

Aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba wamevuliwa vyeo vyao vyote baada ya kuhusika na waraka wa mkakati wa siri wa kukipasua chama unaojulikana kama 'Waraka wa Ushindi' ambao umevunja katiba za chama hicho, kupandikiza chuki za kidini, majungu na kukashifu viongozi wa chama.
SABABU ZA ZITTO, DK. KITILA NA MWIGAMBA KUVULIWA VYEO VYAO
Mhe. Tundu Lissu amesema kuwa Kamati Kuu imenasa waraka huo wa mkakati wa siri wa kukipasua chama vipande vipande unaohusisha watu wanne ambao ni Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo, Samson Mwigamba na mtu mwingine ambaye hajajulikana.

Anasema lugha iliyotumika katika waraka huo ni ya siri ambapo kuna mtu anaitwa MM ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe, M1 ni Dk. Kitila Mkumbo, M2 hajajulikana na Dk. Mkumbo alikana kumfahamu kabisa M2 na M3 ni Samson Mwigamba.

Waraka huo uliojulikana kama Waraka wa Ushindi unavunja katiba ya chama kwa sababu umepandikiza chuki za kidini, majungu na kukashifu viongozi wa chama kinyume na katiba ya CHADEMA.

Tuhuma zote zilizoko katika waraka huo hazijawahi kuwasilishwa kwenye kikao chochote halali cha chama kinyume na matakwa na masharti ya katiba ya chama.

Anaongeza kuwa hakuna taasisi yoyote inayoweza kupuuza wala kuvumilia mambo haya yaliyopo kwenye waraka huo kwani umewatukana sana viongozi wa chama.

Anasema matusi hayo ni ya muda mrefu na viongozi wakuu wamekuwa wakiyavumilia kwa muda mrefu lakini yalivumiliwa kwa lengo la kuwapa nafasi wanamtandao hao kujirekebisha.

Kamati Kuu imeamua kuwavua nyadhifa zao zote watu wote waliotajwa katika waraka huo ambao ni Zitto Kabwe, Dk. Kitila Mkumbo na Samson Mwigamba.

Pia Kamati Kuu imeunda kamati ya kuchunguza na kufuatilia mhusika mwingine M2 ambaye anadaiwa ni Mtumishi wa Makao Makuu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa dhidi yake.

Kamati Kuu imeagiza wahusika wote waandikiwe barua za kujieleza ni kwa nini wasivuliwe uanachama kwa makosa hayo makubwa waliyofanya.

Pia Kamati Kuu imeagiza mchakato wa kumvua Zitto nafasi yake ya Unaibu wa Kambi ya Upinzani Bungeni.

Lissu anasema Naibu Katibu Mkuu Zitto Kabwe na Dk. Kitila Mkumbo waliomba kujiuzulu nyadhifa zao zote baada ya waraka wao kukamatwa lakini Kamati Kuu iliwakatalia baada ya kuona kuwa kukubaliana na maombi yao hayo ilikuwa ni kama kuwaacha wajiuzulu kwa heshima ambayo hawaistahili hata kidogo.

Kamati Kuu pia imeazimia kuusambaza waraka huo kwenye vyombo mbalimbali vya habari ili Watanzania waone na kujua ukweli.

Lissu amemalizia kwa kuwaomba Watanzania na wanachama wote wa CHADEMA nchi nzima wasife moyo na waendelee kukijenga chama na nchi yao.

TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top