HATIMA ya mawaziri watano kuendelea na nyadhifa zao iko shakani baada ya wabunge kuwatuhumu kushindwa kuwajibika ipasavyo na kusababisha migogoro ya wafugaji na wakulima.

Kufuatia kadhia hiyo iliyojitokeza wakati wa kutekelezwa kwa Operesheni Kimbunga na Operesheni Tokomeza Ujangili, Bunge limeamua kuunda kamati teule kuchunguza migogoro ya wakulima na wafugaji ambayo imesababisha vifo, ukiukaji wa haki za binadamu na upotevu wa mali.

Wabunge wengi waliochangia hoja hiyo waliwataja wazi mawazi kadhaa akiwemo Waziri Mkuu Mizengo Pinda, wakitaka wawajibishwe kwa kuondolewa kwenye nyadhifa zao kutokana na kushindwa kuchukua hatua wakati operesheni hizo zikipoteza maisha ya watu na mifugo.

Mbali na Pinda, wamo pia Dk. Emmanuel Nchimbi (Mambo ya Ndani), Khamis Kagasheki (Maliasili na Utalii), David Mathayo David (Mifugo na Uvuvi) na Shamsi Vuai Nahodha (Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa).

Dalili mbaya kwa viongozi hao zilianza kuonekana jana asubuhi baada ya Spika wa Bunge, Anne Makinda, kutangaza kuwa amekubali hoja za wabunge wawili waliotaka shughuli za Bunge ziahirishwe ili kujadili jambo la dharura.

Alisema Mbunge wa Sikonge, Said Nkumba (CCM) alitaka Bunge lijadili kuhusu migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi, huku Mbunge wa Mwibara, Kangi Lugola (CCM), alitaka Bunge lijadili vitendo vinavyofanywa na watendaji katika Operesheni Tokomeza Ujangili.

Lugola alidai watendaji wamekuwa wakiwaua kwa risasi ng’ombe waliowakamata kwenye operesheni hiyo pamoja na kuwatesa wamiliki wasiotoa fedha zinazohitajika.

Kutokana na hoja hizo, Makinda alitoa fursa kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Khamis Kagasheki na Waziri wa Maendeleo ya Mifugo na Uvuvi, David Mathayo kuelezea Operesheni Tokomeza Ujangili na migogoro kati ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.  

Kagasheki ndiye aliyekuwa wa kwanza kueleza operesheni hiyo inaendelea. Alisema inalenga kutokomeza ujangili ulioshamiri hapa nchini kiasi cha kutishia sekta ya utalii na tembo.

Hata hivyo, Kagasheki alisema kutokana na malalamiko ya watu mbalimbali juu ya mwenendo wa operesheni hiyo, serikali imeamua kuisitisha ili kufanya tathmini.

Waziri huyo pia alisema mifugo yote iliyokamatwa ndani ya hifadhi kabla na baada ya operesheni hiyo iachiliwe bila gharama yoyote na watu wenye ushahidi wa ng’ombe wao waliouawa kwa risasi wawasilishe vielelezo ili achukue hatua zaidi.

Mara baada ya Kagasheki kutoa taarifa hiyo, Waziri Mathayo alitoa taarifa kuhusu migogoro kati ya wafugaji na wakulima. Aliwaomba radhi waliopata hasara ya kujeruhiwa, kupoteza mifugo au vifo katika operesheni hiyo.

Wabunge wacharuka
Mara baada ya mawaziri hao kumaliza kutoa taarifa zao, Spika Makinda alitoa fursa kwa wabunge kuchangia. Mbunge wa Kilolo, Peter Msolla (CCM), alitoa hoja ya Bunge liunde kamati teule kuchunguza migogoro ya wafugaji na watumiaji wengine wa ardhi.

Alifuata Lugola, ambaye alisema anashangazwa na mawaziri Nchimbi, Nahodha, Kagasheki na Mathayo kuendelea kuongoza wizara wakati damu za wananchi waliofariki katika operesheni zinazohusisha wizara wanazoziongoza zinawakabili.

Mbunge wa Busega, Dk. Titus Kamani (CCM), aliifananisha serikali na ugonjwa wa miguu na midomo kwenye mifugo, maarufu kama Sotoka, ambao miaka ya nyuma ulikuwa ukiua ng’ombe wengi.

“Hii serikali ya ajabu sana, yaani ukiwa na mifugo mingi ni kero kwao. Badala ya kuweka mazingira mazuri ya kukuza uchumi, wanaiua. Mimi naifananisha na Sotoka,” alisema.

Mbunge wa Maswa, Magharibi, John Shibuda (CHADEMA), aliwataka wabunge wa CCM waache unafiki na wamuondoe Waziri Mkuu, Pinda kwa kuwa hachukui hatua kila anapopelekewa matatizo.

“Wewe Waziri Mkuu, taarifa za kiintelijensia hazikufikii? Je, husomi magazeti kujua kinachotokea kwenye maeneo mbalimbali na mbona huchukui hatua? Nyinyi watu wa CCM msileane,” alisema.

Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Pauline Gekul (CHADEMA), alimtaka Rais Jakaya Kikwete awafukuze kazi mawaziri wake waliosababisha operesheni za kinyama zilizosababisha vifo vya binadamu, mifugo na unyanyasaji.

Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM), alisema serikali inatia aibu kwa kukamata meno ya tembo, lakini inashindwa kuwakamata majangili waliohusika.

Mbunge wa Viti Maalumu, Esther Bulaya (CCM), aliwataka mawaziri waache porojo za kisiasa wanapoambiwa matatizo ya wananchi na wabunge.

“Wabunge humu ndani tunaeleza matatizo ya wananchi, eti waziri anasema si mambo ya msingi…acheni porojo, fanyeni kazi, maana tuna ushahidi wa kile tunachokisema,” alisema.

Kamati teule
Akihitimisha mjadala huo, Makinda aliafiki wazo la kuundwa kwa kamati teule.

Hata hivyo kamati teule hizo kila zinapoundwa na ripoti yake kusomwa zimekuwa zikisababisha kuondoka madarakani kwa watendaji mbalimbali.

Februari 8, 2008, Waziri Mkuu, Edward Lowassa, alilazimika kujiuzulu baada ya kamati teule iliyoundwa na Bunge kuchunguza zabuni iliyoipa ushindi wa kuzalisha umeme wa dharura Kampuni ya Richmond kumgusa.

Mwaka juzi, Bunge liliunda kamati teule kuchunguza matumizi ya Wizara ya Nishati na Madini, ambayo ilidaiwa kuchangisha sh milioni 50 kwa idara na taasisi zilizo chini ya wizara, ili kufanikisha upitishwaji wa bajeti, na ripoti yake ilimng’oa Katibu wake, David Jairo.
Tanzania Daima 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

1 comments:

Anonymous said... November 2, 2013 at 10:12 AM

Ni kweli wawajibishwe maana hao watendaji wao wamegeuza hiyo operation kuwa mradi wa kujiongezea kipato maana wakiona una vijimalimali na pesa kidogo unaitwa Jangili unakamatwa na ili utoke ni milion mbili chap zikuchomoke.

 
Top