Rais Jakaya Kikwete
Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete ametangaza kuwa mgogoro baina ya Tanzania na Rwanda sasa umemalizika rasmi.

Katika hotuba yake ya mwisho wa mwezi kwa raia wa nchi hiyo Rais Kikwete amesema hatua hiyo inafuatia mazunguzo baina ya viongozi hao wawili yaliyofanyika hivi karibuni nchini Uganda.

Kwa miezi kadhaa Tanzania na Rwanda zimekuwa katika mgogoro wa kidiplomasia baada ya Rais wa Tanzania Jakaya Kikwete kuishuri Rwanda pamoja na Uganda kuzungumza na waasi wa nchi zao waliopo nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
 
Japo hajataja ni kwa namna gani mgogoro huo uliokuwa umefukuta baina ya Tanzania na Rwanda na vipi umepa afumbuzi, Rais Jakaya Kikwete amesema hatua ya mazungumzo baina yake na Rais wa Rwanda Paul Kagame ndio chanzo cha mafanikio hayo yote.

Tanzania na Rwanda ziliingia katika mgogoro wa kidiplomasia hadi kufikia hatua ya kutunishiana misuli kisiri siri baada ya Rais Jakaya Kikwete kushauri nchi ya Rwanda na Uganda kuzungumza na waasi wa nchi zao waliopo nchini Jamuhuiri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Jambo hilo lililopingwa vikali na Rwanda kwa madai kwamba Rais Kikwete aliingilia mambo ya ndani ya Rwanda kwa kuwashauri kufanya mazungumzo na watu walioua raia wa nchi hiyo.

Mgogoro huu ulipamba moto na hata kukolezwa na zaidi na vyombo vya habari pamoja na mitandao ya kijamii. Sasa Rais anavyoomba vyombo vya habari Wanasiasa pamoja na mitandao ya kijamii kusaidia kwa upande mwingine kuziba ufa wa uhusiano uliobomolewa.

Aidha katika hotuba Rais Kikwete alitumia fursa hiyo kutoa ufafanuzi wa opereshi ya kuwaondoa wahamiaji haramu nchini humo iliyofanyika hivi karibuni ambapo amesema kuwa operesheni hiyo iliendeshwa kwa haki na hakuna uvunjifu wa haki za binadamu uliofanyika katika operesheni hiyo.

Hata hivyo Rais Kikwete ametoa agizo kama kuna mtu aliyenyanyaswa katika operesheni hiyo atoe taarifa kwa viongozi wa serikali.

Kuhusu wahamiaji waliokaa nchini Tanzania muda mrefu Rais Kikwete amesema watu hao sasa watapewa uraia rasmi wa Tanzania ili wafuate uratibu.

Mbali na suala la uhusiano wa Tanzania na Rwanda Rais Kikwete pia alizunguzia masuala mengine yaliyojitokeza hivi karibu ikiwa ni pamoja na muswada wa sheria ya katiba mpya kuhusu uundwaji wa bunge la katiba uliozua mtafaruku hivi karibuni ambapo alivialika vyama vya upinzani vilivyokuwa vikipinga sheria hiyo wakae naye katika meza ya mazungumzo kumaliza mgogoro huo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top