Freeman Mbowe
CHAMA cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), kimemshauri Rais Jakaya Kikwete kutokubali kuyumbishwa na wabunge na mawaziri wachache wa CCM wasiolitakia mema Taifa la Tanzania.
Pia amemtaka awe Rais wa nchi, na atumie mamlaka yake kuhakikisha Sheria ya Mabadiliko ya Katiba ya Mwaka 2013 aliyotia saini, inarejeshwa bungeni kufanyiwa mabadiliko.

Hayo yalisemwa jijini hapa jana kabla ya kuanza kwa Mkutano wa Baraza la Uongozi-Kanda ya Kaskazini na Mwenyekiti wa Taifa wa CHADEMA, Freeman Mbowe.

Alisema ni imani yake sheria ya zamani waliyoigombea haitatumika tena bungeni na hivyo aliomba wabunge wa CCM wenye nia nzuri kuhakikisha wanakuwa na sauti moja ya kupigania Katiba yenye maslahi kwa wananchi wote.

“Nimtake Rais Kikwete asikubali kuyumbishwa na wanaodai eti watavunja bunge na kusababisha kuingia kwenye uchaguzi mwingine.

“Hakuna mbunge hata mmoja wa CCM aliyepo tayari kurudi kwenye uchaguzi wote ni waoga, unadhani hapo nani atakuwa na jeuri ya kulivunja bunge eti kwa sababu Rais karejesha bungeni Sheria,” alisema Mbowe na kuongeza:

“Namshangaa Rais Kikwete anatishiwa na watu aliowateua yeye wakati hana kitu cha kupoteza katika hili,” alisema.

Mbowe alisema taifa kwa sasa limekumbwa na hofu ya ama kufanyika uchaguzi mkuu au kutofanyika, ama kuwapo Serikali ya Tanganyika au la.

“Ninaenda Dodoma na kikao cha Bunge hakika hapatatosha. Sisi tulitoka Bungeni ili dunia ijue ubabe uliokuwa ukifanywa na CCM,” alisema Mbowe.

Naye muasisi wa Chama hicho, Mzee Edwin Mtei (81) aliwaambia wajumbe wa kikao hicho kwamba roho yake ina mdunda kwa kujawa na matumaini akiamini ipo siku atashuhudia wakishinda.

“Mimi ni Mzee wa Kitanzania, ninayesikia raha kutokana na vijana wangu kuimarisha Chama nilichokianzisha mwaka 1992,” alisema Mzee Mtei.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top