Kamanda wa polisi mkoani Geita,Leonard Paulo  
Mauaji ya kikatili yanayodaiwa kufanywa na Kikundi cha Chinjachinja dhidi ya vikongwe, yamezidi kuutikisa Mkoa wa Geita baada ya kikongwe mwingine, kuuawa kwa kukatwa kwa mapanga akiwa nyumbani kwake.
Marehemu huyo ametajwa kuwa ni, Maua Ikoti (60) mkazi wa Kasang'hwa, wilayani Geita.
Mauaji hayo yamekuja huku takwimu zikionesha kuwa  vikongwe watatu, wameuawa na kikundi hicho katika kipindi cha wiki nne zilizopita.
Baadhi ya watu wanahusisha mauji hayo  na imani za kishirikina.
Tukio la mauaji hayo lilitokea saa 6 usiku wa kuamkia juzi  baada ya wauaji  kuvamia familia hiyo na kisha kuingia ndani ya chumba alimokuwa amekala kikongwe huyo.
Mwenyekiti wa Serikali ya Kijiji cha Kasang'hwa, Maganiko Ndiomali, alisema wauaji walimkata kwa mapanga kikongwe huyo kichwani, mikononi na kwenye matiti.
Alisema pamoja na mayowe yaliyopigwa na watoto wa marehemu ili kuomba msaada, juhudi za wananchi kuwasaka wauaji hazikuzaa matunda.
Kuna madai kuwa kikundi kinachohusishwa na mauaji hayo kimekuwa kikikodiwa na baadhi ya watu ili kulipiza kisasi baada ya kufiwa na ndugu zao wakiamini kwamba wamerogwa.
Kikundi hicho kinadaiwa kuhusika na mauaji ya kikatili dhidi ya Mondesta Nchambi (53) mkazi wa kitongoji cha Isabilo wilayani Chato kwa kumchinja mithili ya kuku.
Kamanda wa polisi mkoani Geita,Leonard Paulo alithibitisha kuwepo kwa matukio hayo lakini alisema hadi sasa hakuna mtu au watu waliokamatwa wakihusishwa na mauaji hayo.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top