Profesa Mwesiga Baregu
MWANAZUONI na Mtaalamu wa Sayansi ya Siasa nchini, Profesa Mwesiga Baregu, ameitaka Serikali kutoa majibu iwapo Kamati ya Bunge ya Sheria, Katiba na Utawala imefuata utaratibu na kuwashirikisha Wazanzibari kutoa maoni yao katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.
Profesa Baregu pia ameitaka Serikali ya Zanzibar kuueleza umma msimamo wake ni upi katika malumbano yanayoendelea bungeni, kati ya Wabunge wa Kambi ya Upinzani na Serikali juu ya Wazanzibari kutoshirikishwa kutoa maoni mbele ya Kamati ya Sheria, Katiba na Utawala.

Profesa Baregu ambaye pia ni Kamishna wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, alisema hayo jana wakati akizungumza na MTANZANIA juu ya vurugu zilizozuka juzi na jana bungeni, ambapo wabunge wa kambi ya upinzani walisusia Bunge.

Madai ya wabunge hao yalikuwa ni kupuuzwa kwa mwongozo wao wa kutaka kuahirishwa kujadiliwa kwa Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, hadi pale wadau wa Zanzibar watakaposhirikishwa.

Mwongozo huo ulitolewa na Mbunge wa Mkanyageni, Habib Mohammed Mnyaa (CUF), akitaka muswada huo uondolewe, hadi hapo Wazanzibari watakaposikilizwa.

Akizungumzia hali hiyo, Profesa Baregu alisema Serikali inapaswa kutoa majibu iwapo Wazanzibari walipaswa kushirikishwa au vinginevyo na kuhoji kigugumizi cha Serikali juu ya suala hilo.

“Swali hili ni lazima linahitaji majibu, walipaswa kushirikishwa au laa, Serikali inawajibika moja kwa moja na kwanini Serikali ipate matatizo?


“Lakini nadhani Serikali haijaliweka sawa suala hili, kama hawakushirikishwa ichukuliwe hatua gani, lakini tuzungumzie Serikali ya Zanzibar nao msimamo wao ni nini, wanapaswa kujisemea.

“Kama kuna upungufu yatajwe waweze kurekebisha, lakini kuachwa bila tamko kamili watu wanataka kujua nini kinaendelea na lengo letu hasa ni kupata Katiba Mpya, turekebishe njia,” alisema Profesa Baregu.

Naye, Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bashir Ally alieleza kuwa matukio na malumbano yanayotokea bungeni hayana tija kwa umma, bali ni maslahi binafsi ya vyama vya siasa.

“Wabunge wote wa upinzani na chama tawala hawatutendei haki, wanadandia suala ambalo haliwahusu hata kidogo.

“Hakuna mbunge yeyote aliyechaguliwa na wananchi katika Bunge Maalumu la Katiba, mvutano wao ni wa kisiasa ambao unalenga nani atakuwa mshindi,” alisema Ally.

Aliongeza kuwa katika mvutano huo, wapinzani wasitarajie kushinda na pia wasilaumu chochote kwa sababu suala wanalolipigania haliwahusu wabunge bali ni la wananchi.

“Wabunge wetu wameacha kujadili masuala yao ya kibunge wanadandia yasiyowahusu, matokeo ya haya mambo yataishia kuwaburuza wananchi,” alisema.

Mwanazuoni mwingine Dk. Azavel Lwaitama alisema, ikiwa Katiba itatokana na chama kimoja au viwili, Rais Jakaya Kikwete hatakuwa ameandika historia, kwani dhamira ya kuwa na Katiba Mpya itokane na wananchi.

“Mimi si mshauri wa rais, kama rais angetumia hekima ya kuzungumza na wabunge wa chama chake, ili kuangalia upya suala la uwakilishi wa Zanzibar ingekuwa vizuri, lakini simwambii afanye hivyo kwa sababu sijui yeye yupo upande gani.

“Historia itakayoandikwa kama mambo yataendelea hivi, itakuwa chama tawala kiliwaburuza wananchi wake, na katika historia hiyo itaeleza wazi kuwa wabunge walifikia hatua ya kutolewa nje ya Bunge wakati wakitetea masuala ya msingi,” alisema.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top