Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova
JESHI la Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam linawashikilia watu wawili kwa tuhuma za kukutwa na vifaa mbalimbali vya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na Polisi kinyume cha sheria za nchi.

Tukio hilo limekuja wakati ambapo matukio ya ujambazi yameshamiri nchini huku watuhumiwa wa ujambazi wakitumia sare na silaha za majeshi hayo kufanikisha mikakati yao.

Akizungumzia kukamatwa kwa watuhumiwa hao jana, Kamishna wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova, alisema kuwa Agosti 31, mwaka huu, saa 4:00 asubuhi maeneo ya Mwasonga Kigamboni alikamatwa Saida Mohamed (30) akiwa na vifaa vya JWTZ.

Kamishna Kova alisema kuwa Saida alikamatwa na askari waliokuwa doria akiwa na suruali saba za kombati za JWTZ, mashati saba, kofia 10 za kombati, na viatu jozi tatu.

Alivitaja vitu vingine kuwa ni ponjoo moja, koti, begi la kuweka nguo za jeshi, shati mbili nyepesi, fulana, kofia aina ya bareti, cheo kimoja cha koplo na mikanda miwili.

Kamishna Kova aliongeza kuwa katika tukio jingine, mkazi mmoja wa Gongo la Mboto, Hussein Mkondoa (25) alikamatwa na kofia ya sare ya Jeshi la Polisi.

Alisema kuwa mtuhumiwa huyo alikamatwa Septemba mosi mwaka huu akiendesha pikipiki akiwa amevalia kofia hiyo iliyopauka nembo.

Kova aliwataka wale wote wenye sare za majeshi wazisalimishe kwani msako huu unaendelea.

Alisema pamoja na kubadilisha uongozi katika Kituo cha Ubungo, jeshi limejipanga vema kukabiliana na utapeli eneo hilo ambalo watu hujifanya askari.

Katika kamata kamata hiyo, ndugu wawili Shadrack Mwangwi (27) na Mwangwi Samweli (38) wanashikiliwa kwa kosa la utapeli.

Kova alisema kuwa watu hao walikamatwa na mihuri 27 ya idara mbalimbali za serikali na taasisi, kumbukumbu za Jeshi la Polisi, vitabu vya mapato, namba za usajili wa magari, leseni za biashara, bima na karatasi za ukaguzi wa magari.

Fastjet wanusurika
Katika tukio jingine, Kamishna Kova alisema watu wanne wanashikiliwa na Jeshi la Polisi kwa kosa la kula njama na kujaribu kufanya tukio la uporaji katika Kampuni ya Ndege ya Fastjet.

Alisema kuwa tukio hilo limehusisha mmoja wa wafanyakazi, Enea Dawson (29) ambaye alikuwa anawasiliana na majambazi hao kwa njia ya simu.

Kova aliwataja watuhumiwa waliokamatwa kuwa ni Issa Karimu (40), mkazi wa Buguruni, Paulo Baltazary (38) mkazi wa Buza na Rajabu Shaaban (40).

Alisema kuwa Agosti 30, mwaka huu, Mtaa wa Samora katika ofisi za shirika hilo, watuhumiwa hao walikamatwa baada ya kuwa na mawasiliano na Enea, ambaye ni tarishi aliyekuwa akiwapa taarifa zote za fedha katika kampuni hiyo.

“Baada ya kuwakamata majambazi hao polisi walifuatilia namba ya simu waliyokuwa wakiwasiliana nayo ambayo iliita huku sauti ikitokea sehemu za siri katika nguo za mtumishi huyo,” alisema.

Kova alisema kuwa katika tukio hilo fedha zaidi ya sh milioni 60 zilizokuwa ziibiwe ziliokolewa.
Alisema kuwa pia walikamata dawa za kulevya aina ya bangi kete 805, puli 56, misokoto 196 na gongo lita 330, ambapo watuhumiwa 120 wanashikiliwa na jeshi hilo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top