SIRI za kumwagiwa tindikali Padri wa Kanisa Katoliki Parokia ya Cheju, Mkoa wa Kusini Unguja, Joseph Magamba, zimeanza kuvuja.

Tanzania Daima Jumapili limedokezwa kuwa kabla ya tukio la juzi, kiongozi huyo alitishiwa kuuawa na watu, ambapo mpaka sasa si yeye wala polisi waliokuwa tayari kuwataja.

Kwa mujibu wa baadhi ya watu walio karibu na kiongozi huyo alitishiwa jambo hilo zaidi ya miezi minne iliyopita na hakuna hatua zozote zilizochukuliwa juu ya jambo hilo.

Tanzania Daima Jumapili liliwasiliana na Kamishna wa Polisi Zanzibar, Mussa Alli Mussa, kujua ukweli wa jambo hilo ambapo aligoma kuthibitisha.

Kamishna Mussa alisema hana uwezo wa kulizungumzia jambo hilo huku akilitaka gazeti hili liwasiliane na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini, Saidi Mwema, ambaye hata hivyo simu zake ziliita bila kupokewa.

Alisema kuwa msemaji mkuu wa masuala ya polisi ni IGP Mwema, huku akibainisha kuwa yeye anao uwezo wa kuzungumzia hali ya majeruhi huyo.

Kamishana huyo alilidokeza Tanzania Daima Jumapili kuwa Padri Magamba amehamishiwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH) kwa matibabu zaidi akitokea katika Hospitali ya Mnazi Mmoja iliyopo visiwani humo.

Alisema hali ya kiongozi huyo inaendelea vizuri licha ya kupata majeraha makubwa usoni, kifuani na mikononi.

Wakati kiongozi huyo akipelekwa Dar es Salaam kwa matibabu zaidi, Rais wa Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein, amewashukia polisi kwa kushindwa kudhibiti matukio ya kumwagiwa tindikali viongozi wa dini waliopo visiwani humo.

Padri Magamba, juzi alimwagiwa tindikali na watu wasiojulikana wakati akitoka kupata huduma ya internet visiwani humo.

Akizungumza wakati amekwenda kumjulia hali padri huyo jana katika Hospitali ya Mnazi Mmoja, Zanzibar, Dk. Shein alilitaka Jeshi la Polisi kuhakikisha wanawatia mbaroni wahusika wote waliofanya kitendo hicho.

Dk. Shein alisema Jeshi la Polisi linapaswa kufanya uchunguzi wa kina na kutumia vikosi vyake vya interejensia ili kukabiliana na matukio ya umwagiaji watu tindikali ambayo yanazidi kushamiri visiwani humo.

Alisema vitendo hivyo haviwezi vikaachwa viendelee kwa kuwa vinazidi kutia doa taifa na lazima wahusika wa matukio hayo wapatikane na kuchukuliwa hatua kali za kisheria.

Kiongozi huyo wa dini aliyejeruhiwa maeneo ya usoni, mikononi na kifuani baada ya kumwagiwa tindikali hiyo alisafirishwa jana hadi Dar es Salaam kwa matibabu zaidi.

Padri huyo alifikwa na mkasa huo wakati akitoka katika duka linalotoa huduma za mawasiliano ya mtandao lijulikanalo kwa jina la Sun Shine Internet Cafe, lililopo eneo la Mlandege, Wilaya ya Mjini Unguja.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top