MAUAJI
ya watu watatu wa familia moja yaliyotokea jijini Mwanza hivi karibuni
yameibua maswali mengi lakini mwisho wa yote, imebainika kuwa
kilichoiponza familia hiyo kukumbwa na mauti hayo ni hiki, Uwazi
limechimba mwanzo mwisho.
Mauaji hayo yalitokea saa 10 alfajiri ya Septemba 21, mwaka huu katika Kijiji cha Ihila, Kata ya Buhongwa, Wilaya ya Nyamagana jijini Mwanza ambapo inaaminika kuwa mgeni aliyekaribishwa kwenye familia hiyo ndiye aliyetekeleza mauaji hayo na alikaribishwa nyumbani hapo bila kujulikana tabia.
Debora Jonas Luhinga, mtoto wa marehemu ambaye alinusurika katika tukio hilo, alisema kuwa mgeni huyo aliyemfahamu kwa jina moja la Lameck alifika nyumbani hapo Septemba 18, mwaka huu lakini baada ya kutekeleza mauaji hayo alitokomea kusikojulikana.
Debora mwenye umri wa miaka 12, alidai kuwa siku ya tukio, usiku akiwa amelala, mdogo wake aitwaye Eliudi aliyekuwa amelala naye aliamka na kuanza kulia sana.
Alisema alichukua jukumu la kumbembeleza mdogo wake huyo lakini ilishindikana, ghafla Lameck aliingia chumbani humo na kumwomba mtoto huyo ili ampeleke chumbani kwa wazazi wake akabembelezwe.
“Kilio cha mdogo wangu kilikuwa kikubwa, mara nikaona mlango unafunguliwa, Lameck akaingia, akasema kwa kuwa mtoto analia sana nimpe ampeleke kwa mama ili akambembeleze,” alisema Debora.
Akaongeza kuwa alikubali kumpa Lameck mtoto huyo na kwa vile yeye alikuwa na usingizi mzito aliendelea kulala fofofo.
Debora alisema alipoamka kulikuwa kumekucha, akashuka kitandani ili aende nje lakini akakuta mlango umefungwa kwa nje.
“Nilipiga kelele baada ya kukuta mlango wa chumba changu umefungwa kwa nje, majirani walifika kunifungulia lakini nilipigwa na mshangao kukuta maiti ya baba ikiwa sakafuni sebuleni tena imetapakaa damu.
“Nikiwa nimechanganyikiwa niliingia chumbani kwa wazazi wangu, nikashangaa kumuona mama yangu na mdogo wangu Eliudi wakiwa wameuawa kwa kunyongwa na miili yao imelazwa chini,” alisema Debora.
Debora alisema anaamini Lameck ambaye mara nyingi alikuwa akimwona akizungumza na baba yake ndiye aliyetenda unyama huo.
Alisema anaamini mtu huyo wakati anaingia
chumbani kwake kumchukua mdogo wake alikuwa ameshawaua wazazi wake na
aliamua kumtwaa mtoto huyo kwenda kumnyonga ili kilio chake kisiwafanye
majirani wakafika nyumbani hapo kutaka kujua kulikoni na hivyo
kugundulika alichokifanya kwa muda huo.
Alikwenda mbele zaidi kwa kusema anaamini baba yake ndiye aliyeanza kuchinjwa kabla ya mama yake kunyongwa.
Baadhi ya majirani waliozungumza na gazeti hili huku wakiomba majina yao kuhifadhiwa baada ya tukio hilo, walisema kwa nyakati tofauti kuwa huenda mauaji hayo ni ya kulipiza kisasi kwa mwanaume huyo ila mkewe na mtoto waliingizwa kwenye mkumbo tu.
Walisema haiwezekani watu wa familia moja wakauawa kikatili namna hiyo bila ya wauaji kuanika sababu.
Waliongeza kwa kudai kuwa siku zote tatu alizoishi hapo, Lameck alikuwa akitafuta njia mwafaka ya kutekeleza ukatili huo.
Walisema mauaji mengi ya aina hiyo yanayotokea katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mwanza huhusishwa na imani za kishirikina, migogoro ya ardhi au mirathi.
Majirani hao waliongeza kuwa awali walikuwa wakimwona Lameck nyumbani kwa marehemu bila kujua uhusiano wao, wakaonya kuwa ni hatari sana kumkaribisha nyumbani mtu usiyemjua kwa undani kama ilivyokuwa kwa Lameck.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, ACP Ernest Mangu alithibitisha kutokea kwa mauaji hayo huku akisema hakuna aliyekamatwa ambapo aliwataja marehemu kuwa ni Jonas Luhinga, Rusia Jonas (Mke wa Jonas) na mtoto wao Eliud Jonas.
0 comments:
Post a Comment