Katibu Mkuu wa
Chama cha Mapinduzi (CCM), Abdulrahman Kinana
WAKATI rufaa ya kupinga ubunge wa Mbunge wa Singida Mashariki,
Tundu Lissu (CHADEMA) ikitarajiwa kuanza kusikilizwa katika Mahakama ya
Rufaa Dodoma, Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia Wakili wake, Godfrey
Wasonga, kimeiomba mahakama hiyo kuifuta kesi hiyo.
Kwa mujibu wa wakili huyo, sababu ya kuomba kufutwa kwa kesi hiyo ni
kutokana na walalamikaji wote kujitoa na kuapa mahakamani kuwa hawapo
tayari kuendelea na kesi hiyo.
Hata hivyo wakazi wawili wa Kijiji cha Makiungu mkoani Singida,
Shabani Selema na Paskali Hallu, ambao walifungua kesi ya msingi kupinga
ubunge wa Lissu, tayari walikwisha kuweka bayana kukubaliana na hukumu
ya Mahakama Kuu Kanda ya Dodoma Aprili, mwaka huu.
Mara kadhaa wananchi hao wamenukuliwa wakimlalamikia Katibu Mkuu wa
CCM, Abdulrahman Kinana, kuwa anawashinikiza kuendelea na rufaa hiyo
licha ya kwamba walikwisha kujitoa.
Akizungumza na gazeti hili jana, Wasonga ambaye alikuwa akiwatetea
wanachama hao katika kesi hiyo, alisema kuwa baada ya kuwasiliana na
wateja wake walimwambia hawapo tayari kuendelea na kesi hiyo.
“Ni kweli walalamikaji wote wamejitoa na mimi kama wakili sioni haja
ya kuendelea, nitakuwa namwakilisha nani? Nimeongea nao jana, hakuna
mwenye nia ya kuendelea na kesi,” alisema.
Wasonga alipoulizwa kama bado anadai malipo kutoka kwa walalamikaji
hao, alisema japokuwa wateja wake ni wanakijiji wasio na uwezo mkubwa wa
fedha walijitahidi kulipa madai yote.
Gazeti hili pia liliwatafuta Selema na Paskali wakiwa Muyanji
kijijini, ambapo walisema kuwa: “Sisi tulishatoa msimamo tangu mapema
hatuna mpango wa kuendelea na kesi.
“Tuliapa mahakamani lakini tulishangaa kuona kesi hiyo inapangiwa
majaji, sisi pia tumepata taarifa kuwa huyo wakili aliyekata rufaa bila
ridhaa yetu amepeleka ombi mahakamani ili kesi iondolewe, hayo ni
matakwa yake binafsi kama yeye alikuwa anafuata maneno ya Kinana,”
walidai.
Naye Lissu alilithibitishia gazeti hili kuwa tayari anao wito wa mahakama kesho kwa ajili ya kusikiliza kesi hiyo.
Alisema kuwa jana jioni alipata barua kutoka kwa wakili wa walalakaji kwenda Mahakama ya Rufaa, wakiomba kuifuta rufaa hiyo.
“Nimepokea samansi niende kusikiliza kesi hiyo siku ya Ijumaa na
tayari nilishaweka pingamizi kupinga rufaa hiyo. Hii taarifa ya
kuondolewa au kufutwa kesi wakati tayari nimeshaweka pingamizi nitatoa
msimamo siku hiyo palepale mahakamani kwa kutumia vigezo vya kisheria,”
alisema.
Rufaa hiyo imepangiwa kusikilizwa katika Mahakama ya Rufaa na jopo la
majaji watatu, Salumu Massati, Engela Kileo na Natalia Kimaro.
Kabla ya kuanza kusikilizwa kwa rufaa hiyo, mahakama ilitarajiwa
kusikiliza pingamizi zilizotolewa na upande wa walalamikiwa, ambao ni
Lissu na Jamhuri za kupinga rufaa hiyo na jopo hilo la majaji litatoa
uamuzi.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Dodoma jana, Lissu alitoa
hoja saba za kupinga rufaa hiyo, muda mfupi kabla hajapokea maombi hayo
ya kuiondoa kesi hiyo.
Lissu alisema hoja hizo ni mkata rufaa Selema ambaye ndiye mlalamikaji
namba moja kupinga kwamba hajakata rufaa kwa hati ya kiapo ya Mei 24,
mwaka huu.
Alisema hoja nyingine ni notisi ya kiapo kutopelekwa kwa mjibu rufaa,
ambaye ni yeye, kinyume cha masharti ya kanuni ya 84 (1) ya Kanuni za
Adhabu za Mahakama ya Rufaa Tanzania za mwaka 2009.
“Vilevile nakala zote rekodi ya rufaa hazijathibitishwa usahihi wao,
na wakata au wakili kinyume cha masharti ya Kanuni ya 96 (5) ya Kanuni
za Mahakama ya Rufaa Tanzania za mwaka 2009.
“Rufaa hii pia imepitwa na muda wake, kwa sababu hati ya ucheleweshaji
iliyotolewa na Msajili wa Mahakama Kuu haijasainiwa, haina tarehe wala
muhuri, kinyume cha Kanuni ya 90 (1) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa ya
Tanzania za mwaka 2009,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa walalamikaji walitakiwa kukata rufaa siku sitini
baada ya notisi ya rufaa kutolewa na kwamba tarehe ya mwisho ya kukata
rufaa ilikuwa Julai 3, mwaka jana, lakini rufaa hiyo ilikatwa Mei 7
mwaka huu.
“Hoja nyingine ni kwamba rufaa hiyo si halali kwa kuwa imeacha nyaraka
muhimu, ikiwamo maombi ya mwenendo wa shauri wa kusamehewa gharama za
dhamana,” alisema.
Lissu alisema pia katika rufaa hiyo, amri iliyomshindisha kesi si
halali, kwa kuwa haionyeshi tarehe ambayo amri hiyo ilitolewa, kinyume
cha kanuni ya 9 ya Kanuni za Masijala za Mahakama Kuu za mwaka 2005.
Alisema pia wakata rufaa wamesindwa kuwasilisha mahakamani hoja za
maandishi za kuunga mkono hoja za rufaa yao ndani ya siku 60 au kuomba
muda wa kuziwasilisha.
Pia hoja nyingine ni kushindwa kuwasilisha hoja hizo za maandishi
kinyume cha Kanuni ya 106 (1), (2) na (9) ya Kanuni za Mahakama ya Rufaa
ya Tanzania za mwaka 2009.
Kesi ya kupinga ubunge wa Lissu ilianza kusikilizwa Machi 12, 2012 na
Jaji wa Mahakama Kuu, Moses Mzuna, aliyetoa hukumu Aprili 27, mwaka huu
na kumtangaza Lissu kuwa mbunge halali wa Singida Mashariki, kwa kigezo
kuwa hoja zote zilizotolewa na wanachama hao wa CCM hazitoshi kutengua
au kubatilisha ubunge wake.
Kufuatia hukumu hiyo, wanachama hao wa CCM waliridhia hukumu ya
Mahakama Kuu, hivyo kuandika barua kwa Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya
Kati kuomba wapewe fedha walizokuwa wameweka kama dhamana yao sh milioni
15.
Lakini Ofisi ya Msajili wa Mahakama Kuu imekuwa ikisuasua kutoa majibu kurejesha fedha hizo kwa Selema na Halu.
0 comments:
Post a Comment