Kiongozi wa mashtaka nchini Misri, amependekeza kuwa aliyekuwa rais Mohammed Morsi afunguliwe mashtaka kwa kosa la kuchochea mauaji ya waandamanaji.

Tuhuma hizo zinahusiana na ghasia zilizotokea nje ya ikulu ya rais mjini Cairo Disemba mwaka jana ambapo angalau watu saba waliuawa kwenye makabiliano.

Wanachama wengine 14 wa vuguvugu la Muslim Brotherhood pia wanatarajiwa kufunguliwa mashtaka kuhusiana na makosa hayo hayo.

Bwana Morsi amekuwa akizuiliwa katika eneo lisilojulikana tangu kuondolewa mamlakani mwezi Julai.

Anakabiliwa na mashtaka kadhaa ingawa pendekezo hii la yeye kushtakiwa ni la kwanza tangu sokomoko kuanza Misri baada ya kuondolewa kwake mamlakani.

Tangu aondolewe mamlakani serikali ya sasa inayoungwa mkono na jeshi, imekuwa ikiwasaka wanachama wa vuguvugu la Brotherhood wanaotaka bwana Morsi arejeshwe mamlakani.

Mwezi jana mamia ya waandamanaji walifariki wakati vikosi vya usalama vilipovamia kambi zilizokuwa zimekaliwa na wafuasi wa Morsi.

Kwa mujibu wa vyombo vya habari, mnamo siku ya Jumapili mwendesha mkuu wa mashtaka alipendekeza kuwa Morsi afunguliwe mashtaka.

Walisema Morsi anashtakiwa kwa kuchochea mauaji na ghasia mnamo mwezi Disemba mwaka 2012.

Hata hivyo haijulikani ni lini kesi hiyo inayohusiana na makabiliano yaliyotokea nje ya Ikulu ya Rais Disemba mwaka 2012, itasikilizwa.

Maelfu ya waandamanaji walikuwa wakipiga kambi nje ya jengo hilo usiku wa kuamkia terehe 4 Disemba wakilalamika kuwa rais Morsi amejipa mamlaka makubwa kupita kiasi na pia wakipinga mpango wake wa kutaka kubadilisha katiba ya nchi.

Iliarifiwa kuwa Morsi aliwataka wafuasi wake kupitia kwa waziri anayesimamia idara ya polisi kukomesha maandamano ya kutaka aachiliwe huru lakini wakakataa.

Inaarifiwa walinzi wa Morsi waliwataka wafuasi wao kuja kuvunja maandamano hayo. Angalau watu saba waliuawa kwenye makabiliano hayo. 

Wafuasi wa Morsi wanasema kuwa walikuwa wanalinda eneo hilo baada ya kushambuliwa na wafuasi wa upinzani.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top