Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe akiwaongoza wenzake, Profesa
Ibrahim Lipumba wa CUF na James Mbatia wa NCCR-Mageuzi, kuingia katika
Ukumbi wa Hoteli ya Courtyard, Dar es Salaam jana, kwa ajili ya mkutano
na waandishi wa habari.
Mshikamano wa vyama vya upinzani katika kupinga Muswada wa
Marekebisho ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba wa 2013 umehamia nje ya
Bunge na sasa vyama hivyo vimetangaza kuanza kampeni ya kuuhamasisha
umma kudai maridhiano kabla ya kuendelea na mchakato wa Katiba Mpya.
Jana wenyeviti wa vyama hivyo; James Mbatia
(NCCR-Mageuzi), Freeman Mbowe (Chadema) na Profesa Ibrahim Lipumba (CUF)
walikutana na waandishi wa habari na kumtaka Rais Jakaya Kikwete
kutosaini muswada huo kuwa sheria, hadi pale kutakapokuwa na maridhiano
ya pande zote husika.
Walisema muungano wao ni mwanzo wa kuunganisha
umma wa Watanzania kufanya uamuzi wa kunusuru walichokiita “utekaji
madaraka na mamlaka ya nchi kutoka kwa wananchi” hivyo wanaitaka
Serikali kurekebisha kasoro zinazojitokeza katika mchakato huo.
Akitoa tamko la pamoja kwa niaba ya viongozi
wenzake, Profesa Lipumba alisema wanachopigania ni kuurejesha mchakato
wa Katiba Mpya mikononi mwa umma, kwa maelezo kwamba suala hilo kwa sasa
limehodhiwa na CCM.
“Rais Kikwete asisaini muswada huu, aurejeshe
bungeni ufanyiwe marekebisho yenye kujenga kuaminiana na mwafaka wa
kitaifa kwenye mchakato wa mabadiliko ya Katiba. Hatutakwenda kumwona
ila aurejeshe bungeni,”alisema Lipumba na kuongeza:
“Mchakato huu unahitaji uvumilivu, staha na hekima
na usitawaliwe na nia mbaya, ubabe, mabavu, kejeli na dharau hasa
kutoka kwa watawala. Misingi hii ikipuuzwa mchakato mzima unaweza
kutumbukiza taifa letu katika mpasuko, migogoro na hata machafuko.”
Mwenyekiti huyo wa CUF alisema nchi ni mali ya
watu, hivyo mchakato huo haupaswi kuhodhiwa na chama kimoja, badala
yake unapaswa kuwa shirikishi na jumuishi ili kuwezesha kuandikwa kwa
Katiba katika msingi wa maridhiano.
Kuna madai kwamba muswada ulipitishwa ukiwa na
marekebisho ambayo yalifanyika kinyume na maoni ya wadau na kinyume hata
na makubaliano ya awali ya Kamati ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala
kuhusu mamlaka ya Rais kuteua wajumbe Bunge Maalumu la Katiba.
Madai mengine ni kwamba wabunge wa CCM waliongeza
baadhi ya mambo kupitia majedwali ya marekebisho, hivyo kutoa mwanya kwa
Serikali inayoongozwa na chama hicho kupitia kwa Rais kuwa na mamlaka
zaidi ya uteuzi wa wajumbe husika.
Itakumbukwa kuwa Septemba 6 mwaka huu, wabunge wa
CCM walitumia wingi wao kupitisha muswada huo katika mkutano wa Bunge
ambao ulisababisha tafrani kiasi cha Mbowe na Mbunge wa Mbeya Mjini,
Joseph Mbilinyi kutolewa nje ya Bunge kwa amri ya Naibu Spika, Job
Ndugai.
Katika tafrani hiyo, baadhi ya wabunge wa upinzani
walirushiana makonde na maofisa usalama, huku wabunge wote wa upinzani,
isipokuwa Mbunge wa Vunjo (TLP), Augustine Mrema, wakiususia.
Mbowe na Mbatia
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Kwa upande wake, Mbowe alisema: “Amani itavurugwa kama mchakato
wa Katiba Mpya utahodhiwa na chama kimoja cha siasa, ikiwa hivyo sisi
hatutakubali kuwa kondoo. Wanaohubiri amani watambue kuwa kuna misingi
ya kuipata amani ni lazima haki iwepo.”
Alisema fursa ya kupata Katiba Mpya inapotezwa na
watu wachache ndani ya CCM, na kwamba wapinzani watatumia kila aina ya
mbinu kuwaelewesha Watanzania kinachoendelea, ili washiriki katika
kuidai Katiba iliyotokana na mawazo yao.
Mbowe alisema wapinzani hawatarudi nyuma na hawatakubali nchi kurejeshwa chini ya uongozi wa Katiba ya sasa.
“Mwalimu Nyerere aliwahi kuandika katika kitabu
chake kwamba, ‘kuna siku wananchi watachagua kifo kama viongozi
hawatakuwa makini’. Amani itaharibiwa na wale wenye dola, sio vyama vya
upinzani” alisema Mbowe.
Kwa upande wake, Mbatia alisema: “CCM ndio nini…
Wanatakiwa kujua kuwa Tanzania kwanza vyama baadaye, vyama vya siasa
vilivyokuwa vikitawala nchini Kenya, Zambia vimekufa, lakini nchi hizo
bado zipo. CCM inaweza kufa, lakini Tanzania itaendelea kubaki.”
“CCM wakisema wapinzani tunafanya vurugu
wanakosea, katika taifa hili Watanzania hawajawahi kuandika Katiba
iliyotokana na mawazo yao. Katiba Mpya ni tendo la maridhiano na kisiasa
sio kisheria, sisi tuna tofauti, lakini tumeziweka pembeni.”
Mbatia alimtaka Rais Kikwete kusimamia kikamilifu
mchakato wa Katiba ili historia isije ikamhukumu. “Yeye ndio ameanzisha
mchakato huu wa kupata Katiba Mpya, aweke masilahi ya taifa mbele sio
masilahi ya chama chake cha siasa, CCM haiwezi kuwa juu ya dola na
Serikali, asisaini marekebisho ya Katiba yaliyofanyika bungeni,”alisema
Mbatia na kuongeza: “Mkono wa Rais usilitumbukize taifa la Tanzania
katika machafuko, kwanza hagombei tena urais wala uongozi ndani ya chama
chake, sasa anamwogopa nani.”
Vyama hivyo pia vimetangaza kuanza rasmi mikutano
nchi nzima kwa lengo la kuushawishi umma kupinga kile walichokiita kuwa
ni ‘hujuma dhidi ya upatikaji wa Katiba Mpya’.
Mikutano hiyo itaanzia Septemba 21 mwaka huu,
katika Viwanja vya Jangwani, Dar es Salaam na baadaye viongozi hao
watakutana na makundi mbalimbali yakiwamo asasi za kiraia, taasisi za
dini, vyama vingine vya siasa, wasomi na taasisi za elimu.
Makundi mengine ni pamoja na vyama vya
wafanyakazi, jumuiya za wakulima, wafugaji, wavuvi, sekta binafsi, watu
wenye ulemavu, jumuiya za wanawake, vijana na wastaafu.
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment