Mama Maria Nyerere
SERIKALI imeshtushwa na taarifa za Mjane wa Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, Mama Maria, kudhulumiwa viwanja vitatu vilivyopo maeneo tofauti jijini Dar es Salaam. Viwanja hivyo vipo maeneo tofauti ambapo kimoja kipo Mikocheni ‘B’ Plot 402 Block C na kingine kipo Msasani Beach Namba 778, ambacho kinadaiwa kugawanywa kwa watu wawili.

Taarifa ilizolifikia MTANZANIA jana ni kwamba watendaji wa Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, kwa siku ya jana walikuwa na kazi ya kupekua nyaraka mbalimbali ili kujua ukweli kuhusu viwanja hivyo.

Hata hivyo mwandishi wa gazeti hili alipofika wizarani humo kufuatilia suala hilo, alielezwa kuwa asingeweza kuonana na kiongozi yeyote, kwani viongozi walikuwa katika kikao kizito wakijadili suala hilo.

Chanzo hicho cha habari kilimtaka mwandishi kwenda ofisi ya uhusiano ili aweze kupata taarifa kuhusu suala hilo, ambalo limegonga vichwa vya watu juu ya utapeli huo.

Ofisa Habari wa wizara hiyo, Rehema Isango, hakutaka kuzungumzia suala hilo kwa undani zaidi ya kumweleza mwandishi kuwa wizara yake inashughulikia mgogoro huo.

“Taarifa hii tumeipata kupitia vyombo vya habari, lakini ninachoweza kukuambia viongozi wanaohusika wanaendelea kutafuta ukweli, naomba uje kesho (leo) nitakuwa na kitu cha kukujibu,” alisema kwa ufupi.

Hata hivyo, chanzo kingine kilidokeza kuwa, baada ya upekuzi huo ilibainika kwamba viwanja hivyo vimefanyiwa utapeli na watu wengi na kwa muda tofauti.

“Kwa kweli sakata hili linaigusa wizara yetu moja kwa moja kwa sababu ndio yenye dhamana ya ardhi, na kwambia baada ya taarifa kuripotiwa jana, kazi ya kutafuta ukweli ilianza.

Chanzo hicho kilieleza kuwa kazi ya upekuzi wa nyaraka ilimhusisha Katibu Mkuu, Alphayo Kidata, ambaye mara kwa mara alikuwa akiitisha nyaraka za viwanja vilivyotajwa kutoka kwa Kaimu Kamishna wa Ardhi, Gasper Luanda.

Hata hivyo MTANZANIA ilifanya juhudi za kuwasiliana kwa simu na Katibu Mkuu, Kidata pamoja na Waziri wake, Profesa Anna Tibaijuka, lakini simu zao hazikujibiwa.

Viwanja hivyo vimesababisha kuwapo na mgogoro mkubwa kati ya familia ya Nyerere na watu ambao wanadai wameuziwa viwanja hivyo miaka kadhaa iliyopita.

Viwanja hivyo, vinadaiwa kuvamiwa na mfanyabiashara maarufu Dar es Salaam, Paul Mushi na mkwe wa Hayati Rashid Kawawa, aliyetajwa kwa kwa jina la Issa Majura Mshangama.

Habari za uhakika kutoka ndani ya familia ya Nyerere zinasema mjane huyo amelazimika kuiandikia Serikali barua akitaka msaada wa kurudishwa viwanja vyake.

Baadhi ya nyaraka zilizoandikwa zinaonyesha viwanja hivyo ni mali halali ya mtoto wa tatu wa Mwalimu, John Nyerere.

Moja ya barua yake ya malalamiko kwa Kamishina wa Ardhi ambayo Mama Nyerere aliiandika Mei 28, mwaka huu inasema “Kijana wangu John Nyerere ni mmiliki halali na kwamba ana vielelezo kamili vya kisheria,

“Ofisi yako ilimpa Letter of Offer ambayo anayo mpaka sasa. Lakini ameshindwa kujenga katika eneo hilo kwa sababu ya uvamizi wa nguvu wa mtu aitwaye Paul Mushi, ambaye ameweza kuhodhi kiwanja hicho kwa miaka mingi, bila kujali au kuogopa sheria za nchi,

“Kwa vile mwanangu John anaumwa na hawezi kutetea haki yake dhidi ya mvamizi huyo, nathibitisha kuwa John amemuomba na kumteua George Francis Mlawa ambaye ni mwanasheria, amsaidie kupigania haki hiyo iliyo wazi, lakini anazuiwa kuipata”.

Nyaraka nyingine zinaonyesha kuwa Machi 12, mwaka huu, John alimuandikia barua Mkurugenzi wa Manispaa ya Kinondoni, akikana kufanya mauziano ya kiwanja Na.778 kwa Issa Majura.

Sehemu ya barua hiyo inseam: “Kwanza kabisa nakana kufanya mauziano na ndugu (Issa Majura), kiwanja changu sijakiuza kwa mtu yeyote yule, kama kuna mtu anadai kuwa nimemuuzia anadanganya, naomba aitwe na mimi nije mbele yako athibitishe jinsi nilivyomuuzia kiwanja hicho.

“Ninachokumbuka, ndugu Majura alivamia kiwanja changu baada ya kumuondoa kwenye kiwanja hicho, hajarudi tena mpaka ninapopata taarifa kutoka kwenye ofisi yako kwamba kauziwa kiwanja changu,” ilieleza barua hiyo.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top