Nchi ya India imefanikisha jaribio lake la kufyatua kombora la nyuklia la masafa marefu kwa mara ya pili, safari hii likiwa na uwezo wa kufika katika mji wa Beijing, China na maeneo kadha wa kadha ya barani Ulaya.

Jaribio hilo linaiweka India katika nafasi imara zaidi ya kuzalisha silaha zenye tishio la nyuklia.

Msemaji wa kituo cha utafiti cha nchini humo (Defence Research and Development Organisation - DRDO), Ravi K. Gupta akikaririwa na vyombo vya habari siku ya Jumapili, alithibitisha kwa kusema, "Jaribio lilifanikiwa. Lililenga na kufanikiwa kufikia shabaha katika uelekeo uliopangwa. Imekidhi malengo yote."

Majaribio ya kombora kama hilo katika siku zilizopita, yalifanikiwa kuyafikia maeneo ya Pakistani na magharibi ya China. Inasimuliwa kuwa India inajitahidi kuimarika kisilaha kwa nia ya kuwa sawa na nchi ya China na pia kujihami dhidi ya majirani zake ambao wanasadikiwa kuwa na silaha za nguvu na hatari za vita.

Nchi hizo mbili zina ushirikiano mwema ila zina historia ya mgogoro wa mpaka wa kuigombea Himalaya uliosababisha zikatwangana kidogo mnamo mwaka 1962.

India pia inajidhatiti kutokana na tetesi kuwa mahasimu majirani zao, Pakistani, wamejilimbikizia silaha za kivita zenye uwezo wa nyuklia ambazo zina uwezo wa kufyatuka kwa masafa mafupi ambayo yakilengwa vizuri yanaweza kusababisha madhara katika maeneo ya nchi za kusini mwa bara la Asia.

Hadi sasa, mataifa yanayotambuliwa rasmi na shirika la Umoja wa Mataifa kuwa na hifadhi ya silaha za nyuklia ni nchi 5 wanachama wa kudumu wa Baraza la umoja huo yaani - Uchina, Ufaransa, Urusi, Marekani na Uingereza (na Israeli)
.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top