Agnes Gerald (Masogange)
Mtanzania Agnes Gerald, maarufu Masogange, ameachiwa huru na
Mahakama ya Kempton ya jijini Johannesburg, baada ya kulipa faini ya
R30,000 (Sh4.8 milioni) kwa kosa la kubeba kemikali zinazotumika
kutengeneza dawa za kulevya.
Wakati Masogange akitozwa faini hiyo mwenzake,
Melissa Edward ameachiwa huru na mahakama hiyo, baada ya kukosekana
ushahidi wa kumtia hatiani.
Msemaji wa Kitengo cha Uchunguzi wa Makosa ya
Jinai cha Afrika Kusini(Hawk), Kapteni Paul Ramaloko alisema Watanzania
hao wameachiwa huru baada ya kuonekana kuwa hawakubeba dawa za kulevya,
bali kemikali aina ya ephedrine.
Hata hivyo, Mahakama ilibaini kuwa, Melissa hana
hatia kwa kuwa ilionekana kuwa amemsindikiza Masogange, ambaye alimwomba
amsaidie kubeba mzigo huo.
“Mahakama iliona kuwa Melissa aliombwa tu
kumsaidia kubeba baadhi ya mabegi, lakini hayakuwa yake. Mizigo yote
iliandikwa jina la Agness Gerald na si Melissa,” alisema Kapteni
Ramaloko.
Kapteni Ramaloko alisema, Melissa alijitetea kuwa
hakuwa amesafiri pamoja na Masogange bali walikutana ndani ya ndege na
Masogange alimwomba amsaidie kubeba mizigo hiyo, kwani ilikuwa mikubwa.
Kwa sheria za Afrika Kusini kubeba kemikali zozote
ambazo zimepigwa marufuku ni kosa la jinai kisheria, hivyo mahakama
iliamuru Masogange ahukumiwe kwenda jela kwa miezi 30 (miaka miwili na
miezi mitano) au alipe faini ya R30, 000 (sawa na Sh4.8 milioni).
Hata hivyo, Kapteni Ramaloko alisema mdhamini wa Masogange alilipa nusu ya fedha na kwamba zinazobaki amalizie baadaye.
Alisema kutokana na kutomalizia kulipa fedha hizo
ataendelea kubaki nchini humo hadi atakapomaliza kulipa nusu ya faini
iliyobaki.
Masogange na mwenzake walipokamatwa na SARS ilielezwa walikuwa wamebeba dawa za kulevya aina ya Methamphetamine, lakini Mahakama juzi ilithibitisha walikamatwa na kemikali aina ya Ephedrine, ambayo siyo dawa za kulevya.
Wakati Kamishna Mkuu wa Kitengo cha Kudhibiti Dawa
za Kulevya nchini, Geofrey Nzowa alipoulizwa na Mwananchi Jumamosi juzi
alisema mzigo walioubeba Masogange na mwenzake haukuwa ni dawa za
kulevya bali ni kemikali za dawa za kulevya, lakini Msemaji wa Mamlaka
ya Mapato ya Afrika Kusini, (SARS), Marika Muller alieleza kuwa timu ya
SARS ina uhakika kuwa mabegi sita yaliyokamatwa Julai 5 ni dawa za
kulevya aina ya Methamphetamine.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Jana, Muller alipoambiwa kuwa Watanzania hao wameachiwa huru
baada ya kulipa faini na mmoja kuachiwa huru kwa kuwa Mahakama
imeridhika kuwa hazikuwa methamphetamine bali kemikali aina ya
Ephedrine, alirudia tena na kueleza kuwa, mamlaka hiyo ina uhakika na
kazi yake na iwapo mahakama imewaachia huru basi yeye hana la kusema
zaidi.
“Kazi yetu kubwa ni kukamata mizigo haramu
inayopitishwa uwanja wa ndege, kama Mahakama imeona kuwa si dawa za
kulevya, hatuna la kuongeza. Kikubwa tumemaliza kazi yetu,” alisema
Muller kwa kujiamini.
Hata hivyo, Nzowa jana akizungumzia kuachiwa huru
kwa Watanzania hao, alionyesha kushangazwa jinsi Mahakama ilivyotoa
adhabu ndogo.
“Hii ni ajabu sana. Kama watu wamebeba mzigo wenye
thamani ya Sh6.8 bilioni wanapigwa faini ya milioni nne, hawataogopa
kufanya hiyo biashara. Hao watu ni hatari sana,” alisema Nzowa.
Alipoulizwa iwapo wakirudi Tanzania wanaweza
kushtakiwa, Nzowa alisema kitengo chake hakitaweza kuwashtaki tena kwa
sababu wanaweza kujitetea kuwa tayari walishahukumiwa, isipokuwa
Mwendesha Mashtaka aliyekuwa akisimamia kesi yao anaweza kukata rufaa.
“Iwapo Mwendesha Mashtaka wa huko akikata rufaa
kwa kuona adhabu aliyopewa mhalifu huyo ni ndogo, anaweza kufanya
hivyo,” alisema Nzowa.
Nzowa alisema, inasikitisha kuwa wakati mapambano ya biashara hiyo yakiwa yanaendelea Tanzania, watuhumiwa hao wanaachiwa.
“Adhabu waliyopewa ni ndogo hasa wakati huu ambao
Tanzania tunachafuka kwa tuhuma hizi. Lazima kitu kifanyike kubadili
hali halisi hapa nchini,” alisema.
Nzowa alieleza kuwa alikwenda Afrika Kusini tangu
Septemba Mosi kuwahoji wasichana hao ambao hata hivyo hawakuweza kusema
lolote la kuisaidia polisi.
Masogange aliandika kwa maandishi kuwa ni kweli
mzigo ulikuwa wa kwake, lakini akasema mdogo wake, ambaye ni Melissa,
hajui lolote na alikuwa amemsaidia.
Julai 5, mwaka huu Masogange na Melissa
walikamatwa katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Oliver Tambo
wakidaiwa wamebeba kilo 150 zilizodaiwa kuwa ni dawa za kulevya aina ya
Methamphetamine zenye thamani ya Sh6.8 bilioni.
Dawa hizo zilizokuwa zimepakiwa katika mabegi
makubwa sita, zinatajwa kuwa ni kiwango kikubwa kukamatwa katika
historia ya SARS ndani ya uwanja huo unaotumiwa na mataifa makubwa
duniani.
Taarifa za kukamatwa kwa wasichana hao zilipamba kurasa
mbalimbali za magazeti ndani na nje ya Tanzania, jambo lililosababisha
Waziri wa Uchukuzi, Dk Harrison Mwakyembe kuchukua hatua za kuusafisha
Uwanja wa Ndege wa Julius Nyerere.
Baada ya uchunguzi wa Dk Mwakyembe ambao ulibaini
kuwapo mchezo mzima uliochezwa wakati Masogange na Melissa walipokuwa
uwanja wa ndege.
Agosti 17 alitoa agizo la kufukuzwa kazi, Koplo
Juliana Thadei, Jackson Manyoni, Yusuph Daniel Issa, Koplo Ernest na
Mohamed Kalugwan.
Mwakyembe alisema katika hali isiyokuwa ya kawaida
mfanyabiashara ambaye hakuwa na tiketi ya kusafiri siku hiyo, baadaye
alibadili mawazo hapohapo na kuamua kuondoka siku hiyo kwenda Afrika
Kusini na kulipia faini ya dola 60 (Sh96, 000) ili kupata tiketi.
Pia Mwakyembe aliliagiza Jeshi la Polisi
kushirikiana na Polisi wa Kimataifa (Interpol) kumkamata mfanyabiashara
anayedaiwa kumsaidia Masogange kusafirisha dawa za kulevya ambaye
alitoweka na mabegi matatu ya dawa hizo huko Afrika Kusini.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment