TUKIO la kumwagiwa tindikali kwa wasichana wawili raia wa
Uingereza limeiweka Tanzania katika sura chafu baada ya kituo maarufu
duniani cha runinga (CNN) kulitangaza kwa uzito mkubwa.
CNN kupitia kipindi chake cha Out Front imeonesha kuwa Tanzania sio
salama tena na kwamba watu wanaotaka kutembelea nchini humo, lazima
wachukue hatua za tahadhari.
Wasichana hao walimwagiwa tindikali juzi saa 1:15 usiku mtaa wa Shangani eneo la mji Mkongwe, Zanzibar ambako walikuwa wakijitolea kufundisha somo la
Kiingereza katika shule ya msingi ya St. Monica inayomilikiwa na Kanisa
la Angilikana Zanzibar.
Akizungumza na Tanzania Daima Jumamosi mmoja wa Watanzania waishio
nchini Norway alisema kuwa majira ya usiku kituo hicho kilitangaza kwa
kina tukio la kutisha la wasichana hao kuvamiwa na kumwagiwa tindikali
hatua ambayo imeiweka Tanzania katika sura mbaya duniani.
“Sio siri ndugu yangu matukio hayo kwa sasa yanatisha maana hata hapa
nchini kwetu watu wanaotaka kutembelea huko wameanza kuchukua taadhali
na kuna uwezekano wa kupungua kwa watalii baada ya tukio hili,” alisema.
Alisema kuwa pamoja na kuwepo kwa baadhi ya Wazungu walioolewa na
Wazanzibari, akitolea mfano jirani yake (jina linahifadhiwa) alisema
tukio hilo limepokelewa na raia wengi kwa hofu kubwa kiasi cha kumfanya
jirani yake kugoma kuzuru Tanzania kwa kuwa ana hofu watoto aliozaa
kudhuriwa.
Mbali na kituo hicho, baadhi ya magazeti ya Marekani na yale ya
Uingereza yameiandika habari hiyo na kuipa uzito wa juu mno, hasa wengi
wakishangazwa na ‘ukarimu’ wao wa kwenda kujitolea kufundisha Zanzibar
huku wakiambulia kumwagiwa tindikali.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mjini Magharibi, Mkadam Khamis Mkadam,
aliwataja mabinti hao waliojeruhiwa kuwa ni Katie Gee (18) na Kirstie
Trup (18) ambao walifika Zanzibar wiki mbili zilizopita kwa mwaliko wa
taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Arts in Tanzania.
Alisema raia hao wa Uingereza walipatwa na mkasa huo wakati wametoka kunywa kahawa katika Jaws Corner, mtaa wa Sokomhogo.
“Walimu hao walipofika makutano ya mitaa ya Shangani na Vuga
wakielekea Hoteli ya Pagoda kwa ajili ya kupata chakula cha jioni ndipo
vijana wawili wasiojulikana waliokuwa kwenye pikipiki aina ya Vespa
waliwamwagia tindikali na kutokomea kusikojulikana,” alisema.
Mkadam alisema raia hao baada ya kumwagiwa tindikali walikimbilia
baharini kunawa, lakini walipoona hali ni mbaya walipata msaada kutoka
kwa raia wema ambao waliwachukua na kuwapeleka Hospitali ya Afya Medical
iliyoko Vuga na baadaye kuhamishiwa hospitali ya Mnazi Mmoja iliyoko
mjini Zanzibar.
Alisema Katie amejeruhiwa vibaya sehemu ya usoni wakati Kirstie
amejeruhiwa kifuani na mgongoni. Wasichana hao kwa sasa wamelazwa katika
Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es Salaam na kuna uwezekano wa
kusafirishwa leo kwenda Uingereza kwa matibabu zaidi.
0 comments:
Post a Comment