Spika wa bunge wa Zamani, Samuel sitta
Wiki moja baada ya kukaririwa akisema baadhi ya wabunge wa CCM
ni mizigo na kwamba hawana mchango wowote bungeni na wala hawatembelei
majimbo yao wakisubiri kubebwa na chama, Spika wa Bunge wa zamani,
Samuel Sitta amewageukia wabunge wa Viti Maalumu akisema hawana umuhimu
wowote.
Akizungumza kwa simu juzi, Sitta ambaye sasa ni
Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki alisema: “Ninakerwa sana na
mfumo wa Viti Maalumu, kwanza sioni umuhimu wa mfumo huu kuendelea
kuwepo katika Katiba Mpya. Hawana umuhimu wowote.”
Katika mkutano wake wa hadhara uliofanyika Uwanja
wa Shule ya Msingi Nyamikoma, Kata ya Busega Mkoa wa Simiyu Julai 29,
mwaka huu ikiwa ni sehemu ya kampeni za kuimarisha uhai wa chama, Sitta
aliwajia juu bila ya kuwataja baadhi ya wabunge wa CCM.
“Wanakwenda bungeni hawachangii, hawana hata hoja
za kuchachafya upinzani, hawachangii, hawa ni mzigo,” alisema Sitta na
kuongeza: “Wapo baadhi ya wabunge, hawajawahi hata siku moja kwenda
kwenye majimbo yao kuwatembelea wananchi waliowachagua... Inawezekana
hata wapiga kura wakawa wamewasahau. Hawa hawafai hata kuchaguliwa
wakiomba tena kura.”
“Rais Jakaya Kikwete amejitahidi sana kuleta
mabadiliko, ameleta mafanikio ya uchumi na mambo mengi. Inatakiwa
wabunge waende wakawaeleze wananchi maendeleo haya, inawezekana
hawayajui lakini watu hawaendi jimboni, wananchi watayafahamu vipi haya
maendeleo?”
Juzi, akizungumzia wabunge wa Viti Maalumu, Sitta
alisema... “Wengi wao hawachangii chochote na mbaya zaidi hakuna wa
kuwahoji chochote kama wabunge wanavyorudi jimboni.
“Ikifika wakati wa posho wapo. Sisemi kama naumia
wao kuchukua posho.... hawa wanachukua posho wanawajibika kwa nani? Nani
anahoji utendaji wao na zaidi itakapokuja Katiba Mpya ya kuwawajibisha
wabunge wazembe, hawa watawajibishwa wapi?”
“Rasimu ya Katiba Mpya isiwaruhusu hawa... hawa
nao ni mzigo mwingine. Wakifika bungeni hawachangii chochote, hawawezi
kuwajibishwa na yeyote kwa mfumo uliopo na pia hawawajibiki popote, sasa
huu si mzigo?”
Walikwishaanza mkakati
Hata hivyo, Juni 9, mwaka huu, ikiwa ni wiki moja
baada ya Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba
kutangaza Rasimu ya Katiba huku ikifuta Viti Maalumu, wabunge wanawake
walianza kuweka mikakati ya Uchaguzi Mkuu wa 2015 kwa lengo la kukamata
majimbo.
Kwa mara ya kwanza, wabunge hao wa Viti Maalumu
walikutana kwa siku mbili kwenye Ukumbi wa Pius Msekwa, Dodoma lengo
likiwa ni kujadili mikakati mbalimbali ya kupambana jimboni.
Mwenyekiti wa Wabunge Wanawake, Anna Abdallah
alisema wanaweka mikakati kuwawezesha kusimama wenyewe kwenye majimbo
mwaka 2015 hasa baada ya kufutwa kwa Viti Maalumu katika rasimu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mbunge huyo alikiri kuwa Viti Maalum haviwapi sifa stahiki kama
wabunge kwa kuwa hawana uwakilishi wa moja kwa moja kwa wananchi.
Alisema bila kuangalia nafasi za vyama, suala la Viti Maalumu
linawabagua na wabunge wa majimbo.
Msimamo wa wabunge wa Viti Maalumu
Baada ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba kutangaza
rasimu, baadhi ya wabunge wa Viti Maalumu walizungumzia hatima ya nafasi
hiyo huku wengi wakionekana kuunga mkono kufutwa kwake.
Mmoja wao ni Grace Kihwelu (Chadema), ambaye
alisema: “Ninachotaka wabunge twende hukohuko jimboni tukapambane kwani
inaleta heshima. Hii ya kuteuliwa inatunyima raha.”
Mbunge mwingine wa Chadema kutoka Zanzibar, Mariam
Msabaha alisema: “Mimi nilikuwa wa kwanza kupingana na haya ya Viti
Maalumu ndiyo maana nikasimama moja kwa moja Jimbo la Jang’ombe
kupigana. Sikutaka kuteuliwa.”
Catherine Magige (CCM), alisema: “Viti Maalumu
havionyeshi ufanisi wa moja kwa moja na sehemu kubwa mbunge ndiye
anayeonekana kwa wananchi.”
Mbunge mwingine wa Viti Maalumu (CCM), Martha
Mlata alisema mfumo wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba utarudisha heshima
kwa wabunge wanawake kwa kuwa wanakwenda kupambana katika majimbo.
Ritha Kabati wa CCM alielezea kufurahishwa kwake
na Tume ya Warioba kuondoa Viti Maalumu... “Vilikuwa vinatudhalilisha,
watu walikuwa hawatupi thamani halisi kama wabunge.”
Suzan Lyimo wa Chadema alisema: “Nimeupenda uamuzi
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba. Wakati mwingine Viti Maalumu vilikuwa
vinatolewa kwa rushwa na sisi wanawake ndiyo ilikuwa inasemwa vibaya.
Sasa ni bora huko katika majimbo tukapambane.”
Mwananchi
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment