Samuel Sitta
WAZIRI wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Samuel Sitta,
amebadili kauli yake ya awali, kwamba katiba mpya iondoe viti maalumu
kwa kuwa wabunge wa viti maalumu hawana umuhimu wowote.
Kauli hiyo ambayo aliitolea Busega mkoani Simiyu, na kunukuliwa na
vyombo kadhaa vya habari, imekuwa ikipingwa na wananchi kadhaa, hasa
wabunge hao wa viti maalumu.
Juzi akiwa mjini Tabora, Sitta alikanusha habari hizo akisema
zinalenga kumchonganisha na wabunge wenzake ambapo a lienda mbali na kudai
vyombo hivyo vinaathiriwa na washindani wake kisiasa, hasa wanaotafuta
urais.
“Nimebaini kuwa upotoshwaji huo ni sehemu ya mkakati wa kundi la
kisiasa ambalo kinara wake anatafuta urais huku akibebwa na marafiki
matajiri,” alisema.
Kauli hii mpya ya Sitta inaweza kulinganishwa na kilichomtokea mke wa
Lutu kwenye simulizi za Kibiblia, aliyegeuka jiwe la chumvi baada ya
kugeuka nyuma kutazama mji wa Sodoma ukiungua, kinyume cha ushauri wa
malaika na msimamo wake wa awali.
Sitta ambaye pia ni Spika wa Bunge wa zamani na mbunge wa Urambo
Mashariki, alisema kuwa amebaini upotoshwaji huo ni sehemu ya mkakati wa
kundi la kisiasa ambalo kinara wake anatafuta urais wa nchi kwa udi na
uvumba.
Waziri huyo machachari ambaye amekuwa na kauli nzito dhidi ya
wapinzani wake kisiasa, alisema kuwa katika uchunguzi wake amebaini
upotoshaji mkubwa na wa makusudi juu ya mambo aliyotamka na kunukuliwa
kuhusu wabunge kutotembelea majimbo na yale yaliyohusu hatima ya wabunge
wa viti maalumu katika katiba mpya.
Kwamba amebaini kuwa mhariri wa gazeti hilo lililomnukuu anapokea
malipo ya kila mwezi pamoja na bonasi kwa kazi maalumu kutoka kwa
mwanasiasa mmoja japo ambaye hata hivyo hakumtaja jina.
“Njama hizi ni mwendelezo wa vita dhidi yangu kutoka kundi la
wanasiasa nililolitaja ambalo limepania kununua urais wa nchi yetu,”
alisema.
Alisema kuwa chanzo cha upotoshaji huu ni kauli yake kwa mwandishi
mmoja kwamba anaunga mkono mapendekezo ya Tume ya Jaji Warioba kuwa
wanawake na wanaume wagombee ubunge kwa kuchaguliwa katika majimbo, na
kwamba utaratibu huo utawajengea wanawake uzoefu mkubwa.
Sitta alifafanua kuwa pamoja na kuchafuliwa hatachoka kupinga jitihada za kundi hilo linalotaka kuiteka dola ya nchi.
Katika hatua nyingine, Sitta amesema kuwa kutokana na uzoefu wake wa
muda mrefu, amebaini kwamba wanasiasa wanaopenda kujitajirisha na
wafanyabiashara wanaojilimbikizia utajiri kwa kuvunja sheria ni kikwazo
cha maendeleo.
Alisema kuwa wafanyabiashara hao kupitia wanasiasa hukwepa kodi,
hupata upendeleo katika zabuni na kuinyonya nchi kwa kutumia mikataba ya
kiswahiba.
0 comments:
Post a Comment