MKURUGENZI wa Mashitaka nchini (DPP), Dk. Eliezer Feleshi,
amefuta kesi ya kuteka na kujaribu kumuua Mwenyekiti wa Jumuiya ya
Madaktari nchini, Dk. Steven Ulimboka, iliyokuwa ikimkabili raia wa
Kenya, Joshua Mulundi, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es
Salaam.
Hatua hiyo imeelezwa kuwa ni baada ya DPP kuona hana haja ya kuendelea
kumshitaki kwa makosa hayo ambayo yalikuwa hayana dhamana.
Hati hiyo ya DPP iliwasilishwa chini ya kifungu cha 91(1) cha Sheria
ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai ya mwaka 2002 kwa niaba yake na Wakili
Mwandamizi wa Serikali, Tumaini Kweka, jana mbele ya Hakimu Mkazi
Waliarwande Lema.
Kweka aliiambia mahakama kuwa kesi hiyo ilikuja kwa ajili ya kutajwa
lakini upande wa Jamhuri hauna nia tena ya kuendelea kumshitaki Mulundi
kwa kesi hiyo.
Hakimu Lema alikubaliana na hoja hiyo na akamfutia kesi hiyo Mulundi ambaye yupo gerezani tangu Julai 13, mwaka jana.
Hata hivyo muda mfupi baada ya Hakimu Lema kumfutia kesi hiyo Mulundi,
askari kanzu walimkamata tena na kumfikisha kwa Hakimu Mkazi, Alocye
Katemana na kisha Wakili Kweka akaiambia mahakama kuwa upande wa Jamhuri
umemfungulia kesi mpya ambayo itakuwa na shitaka moja tu.
Mbele ya Hakimu Katema, wakili huyo alidai kuwa Julai 3, mwaka jana,
Mulundi katika Kituo cha Polisi Oystebay alitoa taarifa za uongo kwa
ofisa wa polisi kuwa yeye na wenzake walikodiwa kwenda kumteka na
kumjeruhi Dk. Ulimboka, jambo ambalo si kweli.
Alidai kosa hilo ni kinyume cha kifungu cha 122 cha Sheria ya Kanuni
ya Adhabu ya mwaka 2002 na kuongeza kuwa upelelezi wa kesi hiyo mpya
umekamilika.
Wakili Kweka alidai licha ya kosa hilo kuwa na dhamana kwa mujibu wa
sheria, lakini upande wa Jamhuri unaomba Mulundi asipewe dhamana kwa
ajili ya usalama wake.
Hakimu Katemana aliiahirisha kesi hiyo kwa muda na kisha kuutaka
upande wa Jamhuri uende ukalete kwa maandishi hati ya kumfungia dhamana
mshitakiwa huyo.
Hata hivyo mshitakiwa huyo alikanusha shitaka hilo na akaomba apewe
dhamana kwani alikuwa na wadhamini. Pia alidai amesota muda mrefu
gerezani bila kosa.
“Ninajua wanataka kunifungia dhamana makusudi ili waweze kunyamazisha
Bunge na umma usiendelee kupiga kelele kuhusu tukio la kupigwa na
kuteswa kwa Dk. Ulimboka na kwa taarifa yenu mkinipeleka tena gerezani
naenda kuanza mgomo …nimechoka kuonewa,” alidai Mulundi.
Hata hivyo kesi hiyo iliporudi tena mchana, Wakili Kweka hakuweza kuja
na hati ya kuzuia dhamana, hali iliyosababisha Hakimu Katemana kutoa
masharti ya dhamana kwa mshitakiwa huyo.
Hata hivyo mshitakiwa huyo jana alishindwa kutimiza masharti hayo na
Hakimu Katemana aliahirisha kesi hiyo hadi Agosti 20, mwaka huu.
Katika kesi hiyo awali, Wakili wa Serikali, Ladslaus Komanya, mbele ya
Hakimu Agnes Mchome, alidai kuwa Mulundi Juni 26, mwaka jana, akiwa
eneo la Leaders Club alimteka Dk. Ulimboka.
Katika shtaka la pili, Komanya alidai kuwa Juni 26, mwaka huu, akiwa
katika eneo la Msitu wa Mabwepande, Tegeta, Dar es Salaam, kinyume cha
sheria, mshtakiwa huyo alijaribu kumsababishia kifo Dk. Ulimboka.
0 comments:
Post a Comment