Wakati matukio ya baadhi ya vigogo na wasanii maarufu
wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya hayajapoa,
imebainika kuwa mtambo maalumu wa kuchanganya na kuziongezea thamani
dawa hizo upo hapa nchini.
Taarifa zilizolifikia gazeti hili zimeeleza kuwa
mtambo huo ambao awali ulikuwa unapatikana Mombasa, Kenya, pekee,
unatumika kuchanganya dawa za kulevya na kemikali nyingine ambapo nusu
kilo ya heroine huongezwa hadi kufikia kilo mbili.
Uchunguzi unaonyesha kuwa mtambo huo
ulioingizwa mwaka huu na kigogo mmoja wa dawa hizo, upo katika nyumba
moja iliyopo eneo la Mbezi Beach.
Mmoja wa watumiaji wa dawa hizo ambaye hakutaka
kutajwa gazetini kwa kuhofia usalama wake, alisema mtambo huo
umerahisisha upatikanaji wa heroine nchini maarufu ‘white sugar’ kama
inavyojulikana mitaani.
“Zamani ‘white sugar’ ikitoka shamba (nchi
inakotengenezwa yaani Pakistan na nchi nyingine) ilikuwa inapelekwa
Mombasa, Kenya, ambako kuna mtambo wa kuchanganya na dawa nyingine ili
iongezeke wingi wake, lakini kazi hiyo inafanyika hapa hapa nchini kwa
sasa,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu uwepo wa mtambo huo hapa
nchini, Mkuu wa Kitengo cha Kuzuia Dawa za Kulevya, Godfrey Nzowa
alisema kuwa kuna taarifa alizonazo ambazo bado anazifanyia kazi.
“Hata kama nikiwa nazo nazifanyia kazi, za kwangu mimi nazifanyia kazi na hata za kwako nazifanyia kazi,” alisema Nzowa.
Hata hivyo, Nzowa akizungumza katika kipindi cha
Malumbano ya Hoja kilichorushwa na Televisheni ya ITV juzi, alisema kuwa
katika siku za hivi karibuni wafanyabiashara wa heroine wamekuwa
wakiingiza nchini malighafi za dawa hizo, tofauti na awali ambapo
walikuwa wakiingiza dawa hizo zikiwa tayari kwa matumizi.
Akitoa mfano alisema kuna raia wa kigeni
alikamatwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere jijini Dar es
Salaam, akiwa na malighafi hizo zilizokuwa zikifanana na sukari na
kwamba Mamlaka ya Chakula na Dawa (TFDA) na Mkemia Mkuu wa Serikali,
ndiyo waliobaini kuwa haikuwa sukari kama ilivyodhaniwa.
Alisema kutokana na uhaba wa dawa hizo bei ya kete
imepanda ambapo hivi sasa hakuna kete ya gramu 0.11 inayouzwa chini ya
Sh 3,000.
Hii ni mara ya pili kubainika kuwepo kwa mtambo wa
kutengenezea dawa za kulevya nchini. Miaka ya hivi karibuni jeshi la
polisi lilikamata mtambo wa kutengenezea dawa za kulevya katika nyumba
moja iliyopo eneo la Mbezi Beach jijini Dar es Salaam.
Uchunguzi uliofanywa unaonyesha kuwa mbali ya
kuwepo mtambo huo kuna nyumba tano katika eneo la Tandika jijini Dar es
Salaam karibu na soko, ambazo zinatumika kuuza dawa za kulevya huku
baadhi ya polisi wa Mkoa wa Kipolisi wa Temeke, wakiwalinda wauzaji wake
kwa kuwapa taarifa ya mipango inayopangwa na jeshi la kuwatia mbaroni.
Alisema kuna wakati askari huonekana wakirandaranda katika mitaa
hiyo, kitu kinachowafanya wakazi wa maeneo hayo kuamini kuwa wamefika
kukamata, lakini badala yake huishia kuingia katika nyumba hizo kuchukua
hongo na kutoka.
“Hata askari wenyewe wakija kukagua hubaki
wakishangaa na kushindwa kuamini kama kweli nyumba waliyoambiwa inauza
unga ndiyo hiyo waliyoikagua. Ndiyo ‘madili’ hayo watu wanavyoishi mjini
hapa,” alisema. Akizungumzia suala hilo, Kamanda wa Polisi Wilaya ya
Temeke, Engelbert Kiondo alisema hawezi kusema ndiyo au hapana kwa kuwa
jambo hilo linahusisha vitendo vya rushwa.
“Kuhusu askari kuwalinda wahalifu siwezi kusema
ndiyo au hapana kwa sababu hili ni suala la rushwa,” alisema Kiondo na
kuongeza kuwa: “Lakini kuhusu kuwakamata vijana wanaojihusisha na dawa
za kulevya hao tunawakamata kila siku, wengi wameshafikishwa mahakamani
kesi zao zipo katika hatua tofauti.”
Kwa upande wake Nzowa, alisema kwamba Jumatano
wiki hii walifanikiwa kuwakamata watu watatu wakijihusisha na dawa hizo,
akiwamo mwanafunzi wa kike na kwamba wote walifikishwa mahakamani.
Taarifa zaidi ziliendelea kueleza kuwa dawa aina
ya heroin au ‘white sugar’ ndiyo inayopatikana kwa wingi nchini huku
ikifuatiwa na ‘cleck’ inayojulikana mitaani kama ‘pele’ kwa kuwa inatoka
nchini Brazil.
“Bei ya unga hutegemea aina na kiwango mteja
anachokihitaji kwani kipo kipimo cha Sh 1,000 na Sh 2,000 huku kipimo
maarufu kama pointi kikiuzwa kati ya Sh3,000 na Sh3,500. Lakini pele
huuzwa bei kubwa zaidi, kwani ukubwa wa punje ya mtama tunanunua kwa
Sh10, 000,” alifafanua.
Mwananchi
3 comments:
Hizi habari hazina maana yoyote kwa mtanzamo wangu. Sasa kama nyumba zenye mtambo huo zinajulikana na ziliko si wawasake na kuwapeleka kwenye vyombo vya sheria? Inatusaidia nini sisi kama hakuna linalofanyika kuokoa nchi yetu. Huu ni sawa na umbea,mtu anakwambia habari hafu anasema siwezi kukwambia nimezitoa wapi. Ebu tutumie nafasi hii kuongelea mambo yanayojenga si kuleta hofu na umbea!!
Kweli huu umbea tu
Big up!gudi news!
Post a Comment