Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe
WIMBI la biashara ya dawa za kulevya linaonekana kuivuruga
serikali baada ya Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa,
Bernard Membe, kuwaangukia wagombea urais 2015.
Membe aliwataka wanasiasa wenye ndoto hizo za kuwania kiti hicho
kupambana na biashara hiyo kwa vitendo badala ya kutoa maneno matupu.
Waziri Membe alitoa kauli hiyo juzi wakati akihojiwa katika kipindi
cha ‘Jenerali on Manday’ kinachorushwa na kituo cha Channel Ten
alipotakiwa kutoa kauli ya serikali katika kukomesha biashara hiyo.
Alisema kuwa tatizo la dawa za kulevya limekuwa likiifedhehesha
serikali, tena ni aibu kwa taifa, hivyo wale walio na nia ya kuwania
urais wanapaswa kupigania suala hilo kwa vitendo.
“Mimi sijaoteshwa bado kuwania urais na wala nia haipo lakini kwa wale
walio na nia ya kutaka urais wasitoe maneno matupu badala yake wafanye
kwa vitendo kukabiliana na tatizo hilo,” alisema.
Alisema kuwa ni lazima vita hiyo ipiganiwe na wale wenye nia ya
kuwania urais ili kuondoa taswira ya nchi kuonekana kuwa kisiwa cha
kuwezesha kusafirisha na kuingiza dawa hizo.
Membe aliongeza kuwa kama kuna ulazima ni muhimu kuagiza wataalamu
kutoka nje ili taifa liepuke kuwa kisiwa cha watu wanaotumia dawa hizo.
Akionesha takwimu za vijana kupoteza maisha, Membe alisema kuwa katika
kipindi cha miezi mitatu Watanzania watatu walipoteza maisha katika
nchi mbalimbali zikiwamo Brazil, Uarabuni na Oman, ambao dawa
ziliwapasukia tumboni.
“Katika kipindi cha miezi tisa Watanzania wanane walikamatwa Marekani,
hii ilitutisha sana, miezi minne wengine walikamatwa Nampula, Afrika
Kusini wakijaribu kuvusha dawa hizo,” alisema.
Alisema kuwa kutokana na tatizo hilo kuwa kubwa wamelazimika
kuliingiza katika ajenda za Jumuiya ya Ustawi ya nchi za Kusini mwa
Afrika (SADC) badala ya kuachia nchi moja moja.
Membe alisema kuwa lazima Watanzania wawe wakweli kueleza wahusika wa
dawa hizo na wale watakaohusika wakamatwe na kupewa adhabu inayostahili.
Alisema kuwa suala hilo limeathiri nchi kidiplomasia hasa kwa vijana
wa Kitanzania kukataliwa kuingia katika nchi za Ulaya ikiwamo Marekani
ambayo ina urafiki mkubwa na Tanzania.
Alisema kuwa vyombo vya ulinzi na usalama vinao wajibu wa kuwabaini
wale wanaohusika na uingizaji na usafirishaji wa dawa hizo.
Waziri huyo alisema kuwa vyombo hivyo visijenge mtandao kwa kuwakamata
wale wanaokula pekee, bali pia wafanyabiashara wanaojificha ambao
hawataki kujulikana.
0 comments:
Post a Comment