Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Jakaya Mrisho Kikwete.
CHAMA cha Mapinduzi (CCM) kimeingia katika mzozo mpya wa vikao
vya chini kupinga uamuzi wa vikao vya juu, ikiwa ni mara ya kwanza
katika historia ya chama hicho.
Mzozo huo umehusisha Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Kagera, Constancia
Buhiye, na Katibu wa Halmashauri Kuu Taifa (NEC) wa Itikadi na Uenezi,
Nape Nnauye, ambaye kikatiba ndiye msemaji wa chama.
Baada ya Nape juzi kusitisha uamuzi wa NEC Mkoa wa Kagera kufukuza
madiwani wanane, jana Buhiye aliita waandishi wa habari mjini Bukoba na
kuwaeleza kuwa hatambui kauli ya Nape.
Alisisitiza kuwa hata kama Nape alitangaza kusitisha uamuzi wa mkoa
kuwavua uanachama wa CCM madiwani hao, na kuwataka waendelee na kazi zao
hadi vikao vya juu vitakapojadili suala lao na kutoa uamuzi, msimamo wa
NEC Kagera ni kwamba waliofukuzwa wamefukuzwa, si madiwani tena.
Akizungumza na waandishi wa habari juzi, Nape alisema CCM Taifa
imeagiza madiwani hao wanane waendelee na kazi zao za udiwani kama
kawaida, huku wakisubiri uamuzi wa Kamati Kuu ambayo imeamua kuweka
ajenda yao kwenye kikao hicho kitakachofanyika Dodoma Agosti 23.
Nape alifafanua kuwa utaratibu wa kutoa adhabu kwa viongozi wa CCM
walio kwenye vyombo vya dola hasa wabunge na madiwani, uamuzi wa NEC
mkoa si wa mwisho, kwani unapaswa kupata baraka za Kamati Kuu ndipo
utekelezwe.
Hata hivyo, Buhiye alisema kuwa chama hicho kinaongozwa kwa mujibu wa
taratibu, miiko, kanuni, katiba na miongozo, hivyo uamuzi uliotolewa na
NEC mkoa juzi ulikuwa halali kwa sababu ulitolewa kwenye kikao halali.
Alipoulizwa kama haoni msimamo wake unapingana na wa chama makao
makuu, Buhiye alidai kuwa hakumsikia Nape akitoa kauli hiyo, na kwamba
hawezi kuitoa. Alisisitiza kuwa hata kama ni kweli Nape alitoa kauli
hiyo, msimamo ni kwamba madiwani wameshafukuzwa.
Buhiye alisisitiza kuwa hajapata barua ya Nape kumweleza uamuzi wa
taifa na wala hajamsikia kwa masikio yake kupitia kwenye vyombo vya
habari akitengua uamuzi wao.
“Kwa mujibu wa ibara ya 14 ya katiba ya chama ni kuwafukuza uanachama
wanaokihujumu kwa namna yoyote na ibara ya 15 kuwavua uongozi ndani ya
chama huku,” alisema.
Aliongeza kuwa mkoa unayo haki ya kusimamisha mwanachama yeyote kwa
kufuata muongozo wa vikao kuanzia ngazi ya chini kwa wale walioteuliwa
na NEC.
“Anayozungumza Nape ni yake na mimi nazungumza kwa niaba ya kikao cha
NEC mkoa wa Kagera,” alitamba na kuongeza kuwa uamuzi wa mkoa hauwezi
kutenguliwa na kikao chochote kwa mujibu wa katiba ya chama hicho
isipokuwa kutolewa ushauri na uongozi wa juu.
Alisema walitarajiwa kuifikisha taarifa ya uamuzi wao makao makuu ya chama jana kutokana wao kuchelewa kuituma.
Uamuzi wa kufukuza madiwani ulifikiwa katika kikao cha NEC mkoa
kilichoketi Jumanne jioni Agosti 14, lakini ulisitishwa siku moja
baadaye kwa kigezo kuwa utaratibu wa kuwafukuza ulikuwa umekiukwa.
Madiwani hao wanatuhumiwa kukisaliti chama kwa uamuzi wao wa kuungana
na wenzao wa upinzani kusaini hati ya tuhuma za Meya wa Manispaa ya
Bukoba, Anatory Amani, wakitaka ang’olewe kutokana na kuiingiza
halmashauri kwenye mikataba mitatu ya kifisadi.
Miradi hiyo ni upimaji wa viwanja 5,000 unaodaiwa mkopo wake wa sh
bilioni 2.9 kutoka Mfuko wa Dhama ya Uwekezaji (UTT) haukufuata taratibu
na wananchi hawakushirikishwa ipasavyo.
Tuhuma nyingine ni mradi wa ujenzi wa soko. Meya anadaiwa kusitisha
malipo ya ushuru na kutaka kuwaondoa wafanyabiashara bila kufuata
utaratibu.
Anatuhumiwa pia kukopa sh milioni 200 kutoka Benki ya Rasilimali Tanzania (TIB) bila kibali cha Baraza la Madiwani.
Vile vile alitoa taarifa kwenye kikao cha baraza hilo kuwa TIB iliwapa ruzuku ya sh milioni 90, lakini hakueleza misingi yake.
Upo pia mradi wa kuosha magari ambao unadaiwa kutumia kiasi cha sh
milioni 297 zinazotiliwa shaka. Ameshindwa pia kutoa mchanganuo wa
mapato na matumizi ya mradi wa kiasi cha sh milioni 134, za ujenzi wa
kituo cha mabasi.
Nape atoa msimamo
Alipotafutwa kuzungumzia msimamo wa chama mkoa wa Kagera kupinga
maamuzi ya taifa, Nape alisema hili si suala la kubishana kwenye vyombo
vya habari sasa.
“Nilichosema mimi ndio utaratibu wa chama unaopaswa kufuatwa wala si
utaratibu wa Nape. Anayebisha anabishia katiba na kanuni za CCM
hambishii Nape, na mimi ndiye msemaji wa chama,” alisema.
Alipoulizwa kuhusu uvumi ulionezwa mjini Bukoba kuwa Makamu Mwenyekiti
wa sasa, Philip Mangula, na mstaafu Pius Msekwa hawajapendezwa na
uamuzi wake wa kubatilisha maamuzi ya NEC Kagera, Nape alisema, “Mangula
na Msekwa ni wazee, wao ndio waliotunga kanuni na taratibu ambazo mimi
nazitumia kuongoza, hawawezi kuzipinga kanuni walizozitengeneza wao.”
Kuhusu msimamo upi sasa unapaswa kufuatwa na madiwani hao, Nape
alisema kuwa msemaji wa chama ni yeye na kwamba maamuzi ya CCM Taifa
yanapaswa yaheshimiwe.
Katika hatua nyingine, madiwani hao nane walisema kuwa pamoja na makao
makuu kutengua maamuzi ya awali, uongozi wa mkoa juzi jioni
uliwakabidhi barua za kuwafukuza uanachama.
Chanzo chetu kutoka ndani ya CCM zilidai kuwa mwenyekiti Buhiye
amekuwa na visasi dhidi ya uongozi wa chama makao makuu baada ya
kuondolewa kwenye nafasi ya ujumbe wa Kamati Kuu ya Taifa ambayo sasa
inashikiliwa na Prof. Anna Tibaijuka.
Hivi karibuni akiwa mjini Bukoba, Rais Jakaya Kikwete alijaribu
kuingilia kati mgogoro huo kwa kuwataka meya Amani na mbunge wa Bukoba
mjini, Balozi Khamis Kagasheki, kumaliza tofauti zao ili miradi hiyo
iendelee kutekelezwa.
Hata hivyo, ushauri wake ulipuuzwa na madiwani hao pamoja na wenzao wa
CHADEMA na CUF wakisema tatizo si ugomvi kati ya wawili hao bali
wanapinga ufisadi wa meya wao kuingia mikataba ya miradi bila
kuwashirikisha.
0 comments:
Post a Comment