Kiongozi mkuu wa vuguvugu la Muslim Brotherhood
nchini Misri, Mohammed Badie amekamatwa na maafisa wa usalama kutoka
makaazi yake eneo la Nasr 'City', Mjini Cairo. Badie aliwekewa kibali
cha kumkamata kwa tuhuma za kuchochea ghasia na mauaji.
Hali ya hatari imetangazwa Misri huku serikali
ikiendelea kuwawinda wafuasi wa Brotherhood ambao wamepinga kuondolewa
madarakani kwa Rais Mohammed Mosri.
Karibu watu 900 wameuawa wakiwemo
mahabusu wa Brotherhood 37 ambao walifariki dunia wakipelekwa katika
jela moja nje ya mji wa Cairo.Mamia ya wafuasi wa vuguvugu hilo akiwemo
Naibu wake Badie, Khairat al-Shatir wamekamatwa tangu kuondolewa kwa
Mohammed Mosri hapo Julai Tatu.
Mohammed Badie amekua akiwaomba wafuasi wa
Muslim Brotherhood kuandamana na kuweka kambi zao mjini Cairo. Hata
hivyo alikwenda mafichoni tangu Julai 10. Jeshi lilivunja kambi hizo na
watu wengi waliuawa na kujeruhiwa.
Kiongozi huyo anakabiliwa na mashtaka ya
kuchochea ghasia na mauaji ya raia wanane mahasimu wa Muslim
Brotherhood.Kukamatwa kwa Badie kunajiri siku kadhaa baada ya mwanawe wa
kiume Ammar kupigwa risasi na kuuawa katika maandamano yaliyofanyika
medani ya Ramses.
Vuguvugu hilo limesema hatua ya kumkamata
kiongozi wao hazitakandamiza wafuasi wake na kwamba mamilioni
wataendelea kupinga mapinduzi dhidi ya utawala uliochaguliwa
kidemokrasia.Mrengo wa Brotherhood wa kisiasa, mbacho ni chama cha
Freedom And Justice umemtangaza Mahmoud Ezzat kuchukua nafasi ya
kiongozi mkuu.
Ezzat ni Naibu mwenyekiti wa chama hicho. Wakati
huo huo Misri imetangaza siku tatu za maombolezi ya kitaifa kufuatia
mauaji ya maafisa 25 wa polisi katika Rasi la Sinai, hapo Jumatatu.
Wanamgambo wa kiisilamu wamelaumiwa kutekeleza
mauaji hayo.Shambulio hilo lilifanyika katika mji wa Rafah ulioko mpaka
na Ukanda wa Gaza.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment