MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imedai aliyekuwa Mhariri Mtendaji wa gazeti la Tanzania Daima Absalom Kibanda na wenzake wawili waliokuwa wakikabiliwa na kesi ya uchochezi wana kesi ya kujibu na hivyo kutakiwa kujitetea.

Mbali ya Kibanda, washtakiwa wengine ni Meneja Uendelezaji Bi a s h a r a wa Kamp u n i y a Mwananchi Communications (MCL), Theophil Makunga na mwandishi wa Tanzania Daima Samson Mwigamba. 
 
Washtakiwa hao walikutwa wana kesi ya kujibu jana na Hakimu Mkazi Warialwande Lema, muda mfupi baada ya upande wa Jamhuri kufunga ushahidi wao na Wakili wa Serikali Beata Kitau kudai kuwa hawana mashahidi wengine. 
 
Baada ya kusema hayo, Wakili wa utetezi Issaya Matambo, aliomba wapewe nafasi ya kuweza kuwasilisha hoja za kisheria iwapo wanaona washtakiwa wana kesi ya kujibu au la. 
 
Hata hivyo, Hakimu Lema alisema kuwa ameshapitia ushahidi wa upande wa Jamhuri na kuwaona washtakiwa wana kesi ya kujibu na hivyo wanatakiwa kutoa utetezi wao. 
 
"Baada ya upande wa mashtaka kufunga ushahidi wao na kwa kuzingatia ushahidi uliopo mahakamani, mahakama inaona washtakiwa wote wana kesi ya kujibu hivyo waje kutoa utetezi wao," alisema Hakimu Lema. 
 
Hakimu Lema amepanga washtakiwa hao waanze kujitetea Septemba 3, mwaka huu. Katika hatua, nyingine mshtakiwa wa kwanza Mwigamba jana hakuwepo mahakamani ambapo mzamini wake Rose Moshi alisema kuwa anaumwa.
 
Alisema kuwa, mshtakiwa huyo amelazwa katika Hospitali ya Mtakatifu Thomas Arusha ambapo Hakimu Lema alimtaka mzamini huyo kuja na vielelezo vya kulazwa kwake tarehe ijayo ya kesi la sivyo atatoa amri akamatwe. 
 
Washtakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo mwaka jana, wakikabiliwa na mashtaka ya kuandika na kuruhusu kuchapisha makala ya uchochezi. 
 
Makunga, ambaye ni mshtakiwa wa tatu aliunganishwa katika kesi hiyo kutokana na kampuni yake kuchapisha gazeti la Tanzania Daima likiwa na makala hiyo inayodaiwa kuwa ya uchochezi, wakati alipokuwa akikaimu nafasi ya Mkurugenzi Mtendaji wa MCL. 
 
Washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi hiyo, kutokana na makala inayodaiwa ya uchochezi iliyochapishwa katika gazeti la Tanzania Daima la Novemba 30, 2011, iliyokuwa na kichwa cha habari kisemacho 'Waraka Maalumu kwa askari wote'. 
 
Makala hiyo inadaiwa kuandikwa na Mwandishi wa Safu ya Kalamu ya Mwigamba, Samson Mwigamba ambaye ni mshtakiwa wa kwanza. 
 
Kwa pamoja washtakiwa hao wanakabiliwa na kesi hiyo, wakidaiwa kuandika na kuruhusu kuchapisha makala yenye uchochezi dhidi ya askari wa majeshi mbalimbali nchini.
Chanzo: Majira
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top