Katibu wa
Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye
Suala la kutimuliwa kwa madiwani wanane wa CCM katika Manispaa
ya Bukoba limeingia sura mpya baada ya Kamati Kuu kuwazuia Meya, Dk
Anatory Amani na Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamis Kagasheki
kushiriki katika siasa mkoani humo hadi mwaka 2015.
Habari zilizopatikana kutoka ndani ya kikao hicho
zinaeleza kuwa uamuzi huo umefikiwa baada ya kubainika mgogoro wa
viongozi hao, unakiumiza chama katika jimbo hilo.
Taarifa zilidai chanzo cha ugomvi kati ya Balozi
Kagasheki na Dk Amani, ni kwa kila mmoja kutaka kugombea nafasi ya
ubunge Jimbo la Bukoba mjini katika uchaguzi ujao. Na kwa uamuzi huo,
Kagasheki na Dk Amani hawatashiriki uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.
Hata hivyo, akitangaza uamuzi huo jana, Katibu wa
Halmashauri Kuu ya CCM, Itikadi na Uenezi, Nape Nnauye alisema viongozi
hao watakutana na Kamati Kuu leo na baada ya hapo utatangazwa uamuzi
uliofikiwa.
Mbali na meya na mbunge huyo ambaye pia ni Waziri
wa Maliasili na Utalii, wengine walioitwa katika kikao hicho cha leo ni
Mwenyekiti wa CCM mkoani humo, Costansia Buhinye, katibu wake, Averin
Mushi pamoja na mwenyekiti wa chama Wilaya ya Bukoba, Yusuph Ngaiza na
katibu wake, Janath Kayanda.
Kutokana na uamuzi huo, Kamati Kuu ambayo
ilimaliza kikao chake saa 8:30 usiku wa kuamkia jana italazimika kukaa
tena leo kuwaelezea uamuzi uliofikia.
Kumekuwapo na mgogoro mkubwa katika Baraza la
Madiwani wa Manispaa ya Bukoba, ukimuhusisha Kagasheki na baadhi ya
madiwani kwa upande mmoja; na Dk Amani na kundi jingine la madiwani kwa
upande mwingine.
Wakati wa mgogoro huo madiwani wamekuwa
wakituhumiana ufisadi, na CCM imekwishawatuma viongozi wake wa juu
kuingilia kati mgogoro huo akiwamo mwenyekiti wake, Rais Jakaya Kikwete,
lakini hakuna mafanikio yaliyopatikana.
Kufikishwa kwenye Kamati Kuu kwa suala hilo
kumekuja baada ya uongozi wa CCM Mkoa wa Kagera kuamua kuwatimua
uanachama madiwani hao, hatua ambayo ilikuwa inahatarisha nafasi zao na
hivyo kukiingiza chama hicho kwenye uchaguzi mdogo.
Habari kutoka ndani ya vikao hivyo zinasema kuwa
kuna uwezekano mkubwa kwa viongozi hao kuwajibishwa kwa kukiuka kanuni,
kwa kuwa upo uamuzi wa chama unaokataza viongozi waliochaguliwa katika
vyombo vya dola kuwajibishwa kwa staili hiyo.
Madiwani waliovuliwa uanachama na kata zao katika
mabano ni pamoja na Richard Gaspar (Miembeni ), Murungi Kichwabuta (Viti
Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe) na
Yusuf Ngaiza ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM wa Wilaya (Kashai).
Wengine ni Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert
Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro) na Dauda Kalumuna
(Ijuganyondo).
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Baada ya kutimuliwa Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape
Nnauye alisema chama Mkoa wa Kagera hawana uwezo wa kuvua uanachama na
kwamba wenye uwezo huo ni ngazi ya taifa.
Nape alisema kwa mujibu wa taratibu za CCM, Mkoa
wa Kagera walitakiwa kuwasilisha tuhuma hizo ngazi za juu ili zijadiliwe
na kuamuliwa na Kamati Kuu (CC).
Aliongeza kuwa kwa mujibu wa taratibu, viongozi wa
kuchaguliwa na wananchi kama wabunge na madiwani, hawawezi kuvuliwa
uanachama na vikao vya chini bali chombo chenye mamlaka hayo ni Kamati
Kuu.
Hata hivyo, siku moja baada ya tamko hilo la Nape,
CCM mkoani Kagera kilisisitiza kuwa uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao
ni halali, kwa kuwa ulifanywa na kikao halali kwa mujibu wa katiba na
kanuni za chama hicho.
Mwenyekiti wa CCM wa Mkoa wa Kagera, Costansia
Buhiye, alisema kwa mujibu wa katiba na kanuni za chama hicho, hakuna
kikao chochote ndani ya chama kinachoweza kukinzana na kikao kingine kwa
hivyo, bado madiwani hao wamefutiwa dhamana ya uanachama kama mkoa
ulivyoamua.
Buhiye alisema kikao cha Halmashauri Kuu ya Mkoa
ndicho kikao kikuu chenye uamuzi wa kumwajibisha mwanachama yeyote,
iwapo atabainika kwenda kinyume cha taratibu na kanuni za chama, kwa
mujibu wa katiba ya CCM.
Suala la Mansour
Katika hatua nyingine, Kamati Kuu imelipeleka
suala la kutimuliwa uanachama kwa Mwakilishi wa Kiembesamaki Zanzibar,
Mansour Yusuf Himid kwenye Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ambako
litajadiliwa leo na kutolewa uamuzi.
Nape alisema mamlaka ya mwisho ya kumteua mwakilishi ni NEC, hivyo lisingeweza kujadiliwa na Kamati Kuu.
Via Mwananchi
Via Mwananchi
0 comments:
Post a Comment