Kamati Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CC-CCM) kimeiomba Serikali kumtuma Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Ludovick Utouh kwenda Bukoba, Kagera kuchunguza tuhuma dhidi ya Meya wa Manispaa hiyo, Dk Anatory Aman.
 
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini Dodoma, Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Nape Nnauye alisema kamati hiyo imewaagiza Mbunge wa Bukoba Mjini, Khamis Kagasheki na Dk Aman kurudisha utulivu wa kisiasa katika Manispaa hiyo ambayo katika siku za karibuni imekuwa na mgogoro mkubwa.
Alisema Kamati Kuu inaamini kuwa kwa CAG kwenda Bukoba kutasaidia kujulikana kwa mambo anayolalamikiwa ili ukweli ujulikane na hatua stahiki zichukuliwe.
Alisema CAG ametakiwa kwenda haraka Bukoba na uchunguzi unatakiwa kufanyika katika kipindi cha muda mfupi kuanzia jana.
“Hivi ninavyozungumza ama CAG ameondoka kuelekea Bukoba au yuko katika maandalizi ya kwenda Bukoba kufanya uchunguzi huo na ukweli utajulikana. Hatuna hofu juu ya kwenda CAG maana katika kikao hiki yupo Waziri Mkuu na vyombo vingine kwa hiyo wamewasiliana naye,” alisema Nape.
Nape alisema wamelazimika kuitaka Serikali kumtuma CAG kwa kuwa tume iliyotangulia iliyomhusisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Abbas Kandoro na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Dk. Rehema Nchimbi haikuwa ya kiuchunguzi, bali ilishughulikia suala la migogoro.
Alisema kuwa taarifa ya uchunguzi huo inapaswa kupelekwa katika kikao cha Baraza la Madiwani wa Manispaa ya Bukoba ili waijadili na kuchukua hatua stahiki kwa mujibu wa kanuni za uendeshaji wa halmashauri hiyo.
Dk Aman anapingwa kutokana na hatua yake ya kuanzisha miradi ya kupima viwanja vya Mji wa Bukoba, ukarabati wa soko na ujenzi wa stendi kuu ya mabasi ambayo inadaiwa kuwa na harufu ya ufisadi.
Madiwani wapeta
Akizungumzia kubatilishwa kwa uamuzi wa Halmashauri Kuu ya CCM ya Mkoa wa Kagera wa kuwafukuza uanachama madiwani wanane wa Manispaa ya Bukoba, Nape alisema uamuzi huo ulikiuka Katiba ya CCM ya mwaka 1977 iliyofanyiwa marekebisho mwaka 2012.
Alitaja kifungu kilichokiukwa kuwa ni Ibara ya 93 (15) ambacho kinataka CC kujulishwa uamuzi huo kabla ya kuchukuliwa kwa hatua hiyo.
“Kamati Kuu inawataka madiwani wa CCM wa Manispaa ya Bukoba, Mbunge wa Bukoba na Meya wa Manispaa hiyo kurudisha utulivu katika halmashauri yao. Pia kurudisha mshikamano katika chama ili Ilani ya CCM itekelezwe kama ilivyokusudiwa,” alisema Nape.

Mgogoro katika halmashauri hiyo ulikiweka njiapanda CCM baada ya kutoa uamuzi wa kuwafukuza madiwani hao Agosti 13, mwaka huu hali iliyoilazimu Kamati Kuu kuingilia kati na kuwahoji viongozi wote waliohusika akiwamo Mbunge wa Bukoba Mjini, Balozi Khamisi Kagasheki, Dk Aman na viongozi wa mkoa wa wilaya.
Madiwani waliokuwa wamefukuzwa ni Richard Gaspar (Miembeni), Murungi Kichwabuta (Viti Maalumu), Alexander Ngalinda ambaye pia ni Naibu Meya (Buhembe) na Deusdedit Mutakyahwa (Nyanga), Robert Katunzi (Hamugembe), Samwel Ruhangisa (Kitendaguro), Dauda Kalumuna (Ijuganyondo) na Yussuf Ngaiza (Kashai).
 Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top