Na Gideon Mwakanosya
WAZIRI Mkuu wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Mizengo  Pinda juzi alijikuta katika wakati mgumu baada ya wananchi wa Wilaya ya Tunduru kumtaka aondoke na baadhi ya vigogo wa halmashauri hiyo kutokana na utendaji wao wa kazi kuwa mbovu.

Wananchi hao waliyasema hayo juzi kwenye mkutano wa hadhara wakati waziri mkuu huyo aliporuhusu maswali kabla ya kuanza kuhutubia wananchi hao ambao walijitokeza kwa wingi kwenye kiwanja cha michezo wilayani hapo.

Wananchi hao walizitaja idara hizo kuwa ni maendeleo ya jamii, mifugo,biashara, mipango miji pamoja na idara ya ushirika ambazo zimekuwa kero kubwa ndani ya halmashauri hiyo na kwamba wamekaa muda mrefu bila kuhamishwa huku wakijifanya kuwa ni miungu watu.

Mwenyekiti wa mtaa wa Extended, Shaibu Mambula alimweleza Waziri Mkuu kuwa halimashauri hiyo haijawahi kufanya ukarabati wa barabara ndani ya miaka 4 cha kushangaza ukarabati umefanyika sikuchache zilizopita baada ya kusikia  ujio wako je ni kweli miaka hiyo mingine halmashauri  ilikuwa haina fedha ya kukarabati au umekuja nazo waziri mkuu? alihoji Mambula.

Mohamedi Nawanga alieleza kero yake juu ya upatikanaji wa viwanja ambapo alidai kuwa wanatozwa fedha bila kupewa stakabadhi nakwamba utaratibu wa uuzwaji wa viwanja umekuwa wa bei ya juu ikilinganishwa na hali za wananchi wa Wilaya hiyo ya Tunduru.

Naye Bakari Chimwaga aliomba bei ya pemebejeo za kilimo iwe na uwiyano sawa kati ya kijiji na kijiji kwani wananchi wengi wa Tunduru wanaishi kwa kutegemea kilimo hivyo mbolea inapouzwa bei ya juu wanashindwa kumudu gharama za manunuzi.

Kwa upande wake Halima Yassini alisema kuwa upande wa huduma ya afya katika wilaya hiyo imekuwa mbovu kutokana na kukosekana kwa madawa ambapo wakienda kutibiwa wanaambiwa dawa hakuna badala yake wanaelekezwa kwenda kununua kwenye maduka yao ambako zinapatikana.

Aidha kwa upande wake saidi Kihosa alimkabidhi waziri mkuu  taarifa ya mkaguzi mkuu wa hesabu za serikali (CAG) ambayo ilishawahi kujadiliwa kwenye baraza la madiwani la halmashauri hiyo ikibainisha ubadhilifu wa fedha unaofanywa na baadhi ya watumishi wa halmashauri ya Wilaya ya Tunduru ambapo alidai kuwa zaidi  ya sh. Milioni 60 zimeliwa huku serikali ikiwaacha bila kuwachukulia hatua yeyote.

Akijibu kero hizo Waziri mkuu Mizengo Pinda alisema kuwa atazifanyia kazi na endapo itathibitika kuwa za kweli atachukuwa hatua za kisheria pamoja na kuwaamisha watumishi ambao wamekaa kwa muda mrefu bila kuhamishwa kwenye halmashauri hiyo.

‘’Nawashukuru wazee na vijana waliojitokeza kutoa kero zao na nimefurahi sana  najuwa jinsi ya kuzitatua kwani  mnakiu kubwa ya maendeleo  ambayo yamechelewa kutokana na ukosefu wa miundombinu ya barabara pamoja na umeme wa uhakika .”alisema waziri mkuu.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top