SERIKALI bado inaendelea kupoteza mapato makubwa kutokana na
misamaha ya kodi inayotolewa kwa makampuni makubwa, hususan yale ya
migodi, ambayo yanachuma madini na kudai kuwa yanapata hasara.
Mgodi wa almasi wa Mwadui mkoani Shinyanga ambao ulianza kuchimbwa
miaka mingi iliyopita chini ya umiliki wa Kampuni ya Williamson ni
mojawapo ya migodi ambayo imejichotea madini bila kulipia kodi wala
gawiwo kwa serikali.
Kwa miaka yoto ya uchimbaji, wamiliki wa mgodi huo walikuwa wakidai
kupata hasara, hivyo kutolipa kodi ya mapato hadi mwaka 1994 mgodi huo
uliponunuliwa na Kampuni Petra ambayo nayo inauendesha hadi leo bila
kulipia kodi.
Chini ya umiliki wa Williamson, almasi iliyokuwa inachimbwa ilikuwa
ikichambuliwa nchini Uingereza pasipo kuwepo na watendaji wa Wizara ya
Nishati na Madini, kujua kiasi cha madini yaliyopatikana.
Kwa mujibu wa vyanzo vyetu, taarifa za mapato ya mgodi huo
zimeendelea kuwa siri kiasi kwamba hata ripoti ya uchunguzi uliofanywa
na kamati ya Bunge mwaka 2004, katika mazingira ya kushangaza haikuwahi
kujadiliwa hadi leo.
Ili kuhakikisha serikali inayabana makampuni hayo ya migodi na simu,
mwaka 2010, Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lilitunga sheria ya
madini na sheria ya Mawasiliano.
Lengo likiwa ni kuhakikisha makampuni hayo yanajiorodhesha katika
soko la mitaji ili taarifa za mapato yake kuhakikisha zinakuwa wazi na
kuwawezesha wananchi kununua hisa.
Hata hivyo, serikali imeendelea kuwa na kigugumizi cha kutengeneza
kanuni za kuendesha utaratibu huo licha ya sheria kuagiza jambo hilo
lifanyike ndani ya miaka mitatu tangu kutungwa kwa sheria hizo.
Hivi karibuni akijibu suala hilo bungeni, Naibu Waziri wa Fedha,
Saada Mkuya, alisema serikali inachukua hatua ili kuhakikisha
utekelezaji wa sheria hiyo unafanikiwa.
Alisema kuwa wameunda vikosi kazi viwili, kimoja kikiwa ni kwa
makampuni ya simu na kingine cha makampuni ya migodi ili kutengeneza
kanuni ambazo zitahusisha Sheria ya Mawasiliano na Sheria ya Madini za
mwaka 2010.
Alisema kwa sababu ni sheria mbili zinazosimamia sekta tofauti ndiyo
maana wameunda vikosi kazi viwili tofauti ili kulitekeleza jambo hilo
ambapo kwa makampuni ya simu kinaratibiwa na TCRA na kingine cha migodi
kinaratibiwa na Wizara ya Nishati na Madini.
Alisema katika mwaka wa fedha 2013/14, kanuni hizo zitakuwa
zimekamilika, hivyo kuwezesha Watanzania kupata umiliki kwenye kampuni
za madini kupitia uuzaji wa hisa za umma.
Mkuya alisema kuwa kanuni hizo
zitawekewa kipengele cha adhabu kwa yale makampuni yatakayoshindwa
kutimiza matakwa ambayo yamewekwa kwenye hizo taratibu.
Wakati serikali ikiendelea kuzembea, Tanzania Daima ilidokezwa kuwa
taarifa ya uchunguzi kuhusu mgodi huo iliwasilishwa bungeni Juni 6,
2004, asubuhi kama hati za kuwasilishwa mezani.
Wakati huo, Spika wa Bunge akiwa Pius Msekwa, taarifa hiyo
iliwasilishwa na aliyekuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Hamad Rashid
Mohamed (CUF).
Lakini kwa fununu zilizopo ni kwamba vigogo wa Mwadui waliteka Bunge
na kuhakikisha ripoti hiyo haijadiliwi, mpaka leo imekuwa ikipigwa
danadana.
Akizungumza na gazeti hili, Hamad alisema kuwa ripoti hiyo ilikuwa
inapigwa vita hata kabla ya kuwasilishwa bungeni na kwamba hata baada ya
kuiwasilisha mezani alielezwa kuwa itapangiwa siku ya kuwasilishwa.
“Hadi tunamaliza Bunge, ripoti hiyo haikupangiwa nafasi ya kujadiliwa na wabunge,” alisema.
Hamadi alisema katika uchunguzi wao walijiegemeza kujua sababu za
serikali kuuza asilimia 25 ya hisa zake kutoka asilimia 50, hivyo kumpa
Williamson uhalali wa kumiliki hisa asilimia 75.
“Hawa watu hawakuwahi kulipa kodi wala gawiwo kwa muda wote waliokaa
nchini kwa madai kuwa wanapata hasara, sasa tulitaka kujua kwanini
waendelee na uwekezaji wakati wanapata hasara,” alihoji.
Alisema kuwa katika uchunguzi wao waligundua kuwa mgodi huo unaweza
kufanyakazi miaka 100 ijayo, hivyo wakashangaa kusikia wamiliki wanadai
kupata hasara.
Hamad aliongeza kuwa wamiliki hao katika hatua ya kushangaza
walinunua mtambo wa kusafisha dhahabu nchini Australia badala ya mtambo
wa kusafisha almasi.
Alisema kuwa hata sehemu ya kuhifadhiwa dhahabu alikuwa haingii mtu
yeyote kwa kisingizio kwamba zinafanya kazi mashine tu lakini wao
walipoingia walibaini kuwa Wazungu hao wanaingia ila watendaji wa wizara
wanazuiwa, hivyo hawajui kiasi cha almasi kinachochukuliwa.
“Wakati huo kituo cha kusafisha almasi cha Tansort kilikuwa nchini
Uingereza kabla ya kuletwa hapa nchini baada ya mapendekezo ya kamati
yetu.
Hivyo almasi ilikuwa inafikia mikononi mwao kisha ndipo inapelekwa Tansort,” alisema.
Aliongeza kuwa wakiwa nchini Uingereza, Tansort walishangazwa na
hatua ya mgodi huo kutolipa kodi kwa kisingizio cha kupata hasara,
wakisema kuwa hata jiwe moja la almasi hiyo lilitosha kulipa kodi hiyo.
Mbunge wa Kigoma Kusini, David Kafulila (NCCR-Mageuzi) naye
alilidokeza gazeti hili kuwa baada ya kuifuma ripoti hiyo, mwaka
2012/2013 wakati akichangia bajeti ya Wizara ya Nishati alizungumzia kwa
kirefu namna mgodi huo usivyolipa kodi.
“Ripoti hiyo niliipata kwa bahati baada ya kutafuta kwa muda mrefu
bila mafanikio mpaka nilijaribu kumwomba kijana mmoja aliyekuwa mgeni
katika maktaba ya Bunge Dodoma ambaye alinipatia.
“Na nikaitumia kuihoji serikali kwa kina mwaka jana ila baada ya
kuchangia Waziri Sospeter Muhongo aliomba kupata ripoti ile, nilipeleka
ofisi zao za Dodoma na kumkabidhi naibu wake, Boniface Simbachawene,
ambaye alielekeza nitoe nakala, wakahidi kushughulikia,” alisema.
Kafulila alisema kuwa ripoti ile ilionesha kuwa almasi
inayochambuliwa na Tansort ili kupanga madaraja ni asilimia 10 tu, na
asilimia 90 inakadiriwa, hivyo kuwa mwanya wa hasara kwa kukadiria
mapato kidogo.
“Kuna mapungufu mengi sana yaliripotiwa kwenye taarifa ile,
yalitosha kabisa kutaifisha mgodi ule, bahati mbaya baada ya kuonesha
ripoti ile bungeni iliibiwa katika mazingira ya utata hotelini kwangu,”
alisema.
Kafulila alisema kuwa wawekezaji hao wa Mwadui walikuwa pia nchini
Lesotho, walikowekeza muda mfupi wakaona hawapati faida wakarudi kwao na
kuhoji ni kwanini wamendelea kuwekeza Tanzania kama wanatangaza
hasara.“Juni 10, 2013 tukiwa bungeni waziri aliitisha bodi ya Kampuni ya
Petra Diamond ambayo inamiliki Mwadui kuanzia mwaka 1994.
Kamati ya Nishati na Madini imekubaliana na waziri kwenda Mwadui hivi karibuni kuanza uchunguzi,” alisema.
Naye Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu (CHADEMA), katika
mkutano wa Bunge uliopita alionesha jinsi makampuni ya madini
yanavyolipa kodi kidogo wakati wafanyakazi walioajiriwa katika makampuni
hayo wanalipa kodi kubwa zaidi.
Alisema kati ya mwaka 1999 hadi 2004, makampuni ya madini yalilipa
kodi sh sifuri kama kodi ya mapato wakati wafanyakazi wa makampuni hayo
walilipa sh bilioni 51.82.
Lissu aliongeza kuwa katika kipindi hicho cha mwaka 1999 hadi 2012,
makampuni hayo yalilipa kodi ya mapato sh bilioni 467.98 na wafanyakazi
walilipa kodi za sh bilioni 505.4.
“Mwaka 2001 hadi 2012, makampuni ya madini yalipata mapato ya dola za
Marekani bilioni 11.9 sawa na sh trilioni 19.635 na kipindi hicho
yalilipa kodi sh trilioni 1.216 au asilimia sita ya mapato yao.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment