
Rais Barack Obama wa Marekani amewasili nchini leo tayari kwa ziara ya
kikazi ya siku mbili ambapo amelakiwa na mwenyeji wake Rais Jakaya Mrisho
Kikwete katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Mwalimu Nyerere jijini Dar es
Salaam.
Baada ya kuwasili akitokea Afrika Kusini ,Rais
Obama alipigiwa mizinga 21 na vikosi vya jeshi la wananchi wa Tanzania na kisha
kukagua gwaride na kuangalia vikundi vya
ngoma na burudani mbalimbali kutoka Tanzania.
Rais Obama ameambatana na mkewe Michelle Obama na
watoto wao huku msafara wake ukiwa na ujumbe wa watu 700 wakiwemo viongozi,wafanyabiashara, wataalam
wa kada mbalimbali na waandishi wa habari.
Wananchi wa jiji la Dar es Salaam na viunga vyake
wamejitokeza kwa wingi katika barabara ya Nyerere na barabara nyingine
alizopitia Rais Obama na msafara wake
kwa lengo la kumkaribisha.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na ofisi ya mkuu
wa mkoa wa Dar es Salaam inaonesha kuwa Rais Kikwete atakuwa na mazungumzo na
mgeni wake Ikulu ambapo pia amemuandalia dhifa ya kitaifa.
Hapo Kesho Rais Obama anataraji kuhitimisha ziara
yake ya siku mbili kwa kutembelea
Mitambo ya kufua umeme ya kampuni ya Symbion kabla ya kuondoka na kurejea
nchini Marekani.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment