Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Issa Bin
Simba
HARAKATI za wanasiasa kutumia nyumba za ibada kufanikisha
malengo yao zimemkera Sheikh Mkuu wa Tanzania, Mufti Shaaban Issa Bin
Simba, ambapo amewataka viongozi wa misikiti (Maimamu) wasizibebe njaa
zao kichwani bali waziache tumboni.
Mufti Simba alisema athari za maimamu kuzibeba njaa kichwani ni
kuzigeuza nyumba za ibada kuwa majukwaa ya siasa ili kuwafurahisha
wanasiasa wanaowatumia.
Licha ya Mufti Simba kutowataja wanasiasa hao, siku za hivi karibuni
baadhi ya wanasiasa wanaotajwa kutaka kuwania urais wamekuwa wakiendesha
shughuli zao kwenye nyumba hizo wakidai kushirikiana na waumini wenzao.
Miongoni mwa wanasiasa hao ni Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF),
Profesa Ibrahim Lipumba, aliyeonekana kwenye video misikitini
akiwaelekeza Waislamu wenzake wajipange kumchagua mgombea atakayejali
masilahi yao ili waishi kama watu wa daraja la kwanza.
Waziri mkuu aliyejiuzulu, Edward Lowassa, naye anashutumiwa kutumia
makanisa kutafuta uungwaji mkono katika kile kinachoelezwa harakati zake
za kuwania urais mwaka 2015.
Onyo la Mufti Simba
Mufti Simba amesema viongozi wa dini wanaotumiwa na viongozi wa siasa
kuzitumia nyumba za ibada kufanya siasa wamefilisika kiimani na
wanaendekeza njaa.
Kiongozi huyo alitoa kauli hiyo juzi jijini Dar es Salaam katika hafla
ya kufuturisha, iliyoandaliwa na familia ya Mwenyekiti wa Taasisi ya
Kiislamu ya Imamu Bukhary, Sheikh Khalifa Khamis, ambapo mgeni rasmi
alikuwa Rais mstaafu, Alhaj Ali Hassan Mwinyi.
Mufti Simba alisema maimamu wanatakiwa kutambua kuwa misikiti ni tiba
ya kiroho, hivyo si vema kuwaruhusu wanasiasa kujitakasa na kujenga
makundi kwa waumini wenyewe kwa wenyewe.
Alisema kunahitajika kuwa na amani katika nyumba za ibada hivyo
Waislamu wana wajibu wa kulinda dini yao, si kuingia misikitini na kutoa
mada zinaloleta shida na migawanyiko kwenye jamii.
“Kama wewe ni mwanasiasa nenda huko bungeni ndiko eneo lako,
misikitini si eneo la siasa, msiingie na kuanza kutoa maneno ya
kujitakasa. Unaizungumza Bakwata vibaya kwakuwa unataka uiteke, wewe
nani? Nenda zako bungeni kafanye hiyo siasa yako,” alisema Mufti Simba.
Mufti alisema kutokana na fujo za mara kwa mara na kuvunjika kwa amani
misikitini kutasambazwa waraka maalumu kwa ajili ya kuanzisha kamati za
ulinzi misikitini ili kudhibiti fujo hizo zinazotokea kwa mgongo wa
dini.
Alisema waraka huo unatokana na kongamano la amani lililofanyika kati
ya viongozi wa dini na Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) Said Mwema, kwa
ajili ya kudhibiti matukio mabaya misikitini yanayoashiria uvunjifu wa
amani.
Alisema kwa sasa kila msikiti utakuwa na kamati ya ulinzi na kama
kutakuwa na yeyote anayefikiria ama kufanya vurugu atadhibitiwa na
kukamatwa kama mhalifu wa makosa ya jinai na atashitakiwa kama
watuhumiwa wengine.
Naye Sheikh Khalifa aliwashukuru wananchi mbalimbali na masheikh kwa
kujumuika nao lakini alisisitiza kuwa katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu
ujao maimamu wanatakiwa kujitambua na kuacha kutumika kwa wanasiasa
waliofilisika.
Alisema ni aibu kwa kiongozi wa dini kufikia hatua ya kuwa na mgombea
wake msikitini, hivyo kuwagawa waumini wake wasiomtaka mgombea husika.
“Katika chaguzi mbalimbali hali imekuwa mbaya, kwa kuwa chaguzi sasa
zimegeuka pesa, mtu anatoa pesa zake na kuwatumia viongozi wa dini, hali
hii haitavumiliwa kabisa, utakuta wanasiasa mufilisi wanatoa fedha na
viwanja kwa ajili ya kujineemesha wao wenyewe,” alisema Sheikh Khalifa.
Naye Rais mstaafu Mwinyi, aliwashukuru watu wote waliohudhuria futari
hiyo huku akisisitiza umoja, amani na utuvuli ambavyo vinawafanya watu
waishi na kufanya shughuli zao bila hofu yoyote.
0 comments:
Post a Comment