Salaam wakuu,
Sina budi kumshukuru sana mwenyezi Mungu kwa kunitendea mema na zaidi ya yote kunipa uhai na afya hadi sasa.Wanasema “shukuruni katika yote” na mimi nalazimika kushukuru kwa yale yote niliyofunuliwa na kuwa sehemu ya ushuhuda wangu katika maisha niliyobakiza hapa duniani.
Namshukuru Mungu muweza wa yote kwa kunirejesha tena uraiani na kwa kuniunganisha na familia yangu,mke na watoto,wazazi ,ndugu,majirani na marafiki,viongozi wenzangu na wanachama wa chama kikubwa CHADEMA na zaidi ya yote watanzania walio wazalendo wanaoipenda na kuipigania nchi yao.
Ninapojikuta huru nje ya milango ya mninga uliowekewa makufuli makubwa,madirisha yenye nondo,ukuta uliowekewa waya wenye miiba mikali na ulinzi wa maaskari wanaonichunga saa 24,inanikumbusha wimbo mmoja wa mchakamchaka uliokuwa ukiimbwa gerezani kila siku saa 11:00 alfajiri tunapoamshwa uliokuwa na maneno;
“Kama raia!kama raia!kama raia!kama raia!
Iko siku moja nitarudi kwetu kwa baba na mama kama raia!
Iko siku moja nitarudi kwetu kwa ndugu na rafiki kama raia!
Kama raia…….”
Ni kweli kabisa na wala si hadithi kuwa ‘jela ni MBAYA, jela ni MATESO!’ Lakini zaidi ya hilo, kwangu mimi nimeyaona pia maisha ya gerezani ni mahala pa mafunzo ya kuijua jamii, kuyajua maisha, kuyaelewa mambo, kuifahamu nchi n.k.
Nimekubaliana mia kwa mia na maneno ya mwenyekiti wetu wa CHADEMA-Taifa Freeman Mbowe(MB) aliponitembelea gerezani Segerea na kuniambia; “hupaswi kulia na kujuta sana;now you are going to be a PRISON GRADUATE, uhitimu ambao kila mwanasiasa na mpigania haki mahiri duniani ameupitia.” Kipindi cha siku 92 nilichokaa ndani nikianzia polisi kituo cha kati, gereza la Keko na kisha kumalizia Segerea kimenipa uzoefu na ufahamu usio wa kawaida.
Ipo tofauti kubwa baina ya idara za polisi na magereza,jambo ambalo lilikuwa nje ya ufahamu wangu kabla.Nina uhakika magereza wakipewa kazi ya kuwasaka walipua mabomu ,watesaji,wapiga risasi mapadri watawakamata. Nilipata bahati ya kuitwa na kufanya mazungumzo na wakuu wa magereza ya Keko na Segerea .
Lakini pia, nilitembelewa na viongozi wakuu wengi wa jeshi la magereza nchini akiwemo kamishena mkuu Minja.Wakuu hawa wana weledi mkubwa wa kumpa mtu somo la ‘ushauri nasaha’(counselling). Wanakufutia fikra zote za uraiani (nyumbani,mitaani na ofisini) na kukurejesha mahala pa maisha yako mapya ya gerezani na kukujuza taratibu na kanuni unazopaswa kuzifuata na kuzitii.
Madaktari na manesi waliweza kuangalia kwa karibu sana afya yangu kiasi cha kulidhibiti kwa kiasi kikubwa tatizo langu la sukari ambalo limekuwa likinisumbua kwa miaka 14 sasa.
2: KESI YA UGAIDI.
Ni kesi ambayo imenifikisha hatua au ngazi nyingine ya maisha yangu kama mwanasiasa.Naamini wahusika walipoamua kuifungua bila shaka mwelekeo ulikuwa uleule ambao niliusoma nikiwa chuo kikuu na ninaousoma katika maandiko mbalimbali kuhusu historia za wanaharakati na wapigania haki,uhuru na ukombozi waliopita na tulio nao au tunaowasikia hivi sasa duniani;wakina Nelson Mandela, Martin Luther King Jr n.k. Wakiwa katika harakati za kuitafuta haki walifunguliwa kesi na wengine kufungwa jela kwa tuhuma za ugaidi,uhaini na kula njama.
Nilikubaliana na dhana ya kimtazamo iliyopo au waliyonayo viongozi /watawala wote wadhalimu duniani kuwa watu wote wanaojitokeza kupambana au kukabiliana na mfumo kandamizi bila woga, watu wote hao kwao ni magaidi,mahaini,wala njama au wasaliti.
Ni kipindi kifupi kilikuwa kimepita tangu timu teule maalumu ilipokuwa imemaliza kikao cha kujitathmini kama CHADEMA (RETREAT) kuona tumetoka wapi, tuko wapi na kwa mfumo upi na mazingira yapi ilikuyafikia malengo tuliyonayo.Nakumbuka miongoni mwa mambo niliyoyasema ni pamoja na nini tutarajie baada ya CHADEMA kuonekana na kuthibitika kwa watawala kwamba imekua,imeimarika na imejipanga vyema kiasi cha kuwatia hofu watawala (CCM) kwamba karibu wanaondolewa madarakani.
Niliwaambia washiriki wenzangu kwamba wajiandae kukamatwa na polisi mara kwa mara,kutiwa ndani,kufunguliwa kesi nyingi zisizo za kweli,kubambikiziwa kesi,kuchafuliwa mbele ya jamii,kutishiwa maisha, kupigwa, kuuwawa, kudhohofishwa kiuchumi n.k.
Nikasema, pindi tukiona hayo yamekamata kasi kila pembe ya nchi tujue CCM tumeanza kuwashika pabaya na ushindi utakuwa umekaribia.
Nilishauri tujipange kisawasawa kimbinu na kimkakati kukabiliana na mambo hayo kwa sababu ni lazima yatokee.Namshukuru Mungu yameanzia kwangu na kama nilivyomwambia mwenyekiti Mbowe aliponitembelea gerezani nilimwambia nimekipokea kikombe hiki na yaliyonitokea tusiyashangae bali yawe changamoto na gia ya kutusukuma kwenda mbele kwa kasi kubwa zaidi.Ni kukanyaga mafuta zaidi mpaka kieleweke na hiyo ndiyo itakuwa faraja yangu mimi na wengine watakaofungwa magerezani.
Tuhuma za ugaidi nilizobambikiziwa zilinirejesha nyuma mwaka 2002 nilipokuwa bungeni kama mbunge wa jimbo la Bukoba mjini (CUF) nikiiongoza kambi rasmi ya upinzani iliyokuwa ikijumuisha wabunge wote wa vyama vya upinzani TLP,NCCR-Mageuzi,CHADEMA,UDP na CUF.Muswada wa sheria hiyo ya ugaidi ukiwa ndio umeletwa bungeni kujadiliwa,niliongoza kambi yangu ambayo miongoni mwao walikuwamo Mh. Mbowe wakati huo akiwa waziri wangu kivuli wa biashara na viwanda na Dr. Willibroad Slaa akiwa waziri kivuli wa katiba na sheria kuupinga na kuukataa muswada huo kwa nguvu zote.
Sababu mojawapo ya kuupinga ikiwa ni mahudhui na malengo ya muswada huo kutoeleweka na kuwa wazi na kwamba ulilenga zaidi matakwa ya kijasusi ya nchi za magharibi zikiongozwa na Marekani na kwa hapa kwetu tulitamka bayana kwamba serikali ya CCM ililenga kuitumia sheria hiyo kuvidhibiti vyama vya upinzani. Hilo ndilo limetokea sasa na likaanzia kwangu.
Ukiachia mbali msongo mkali wa mawazo niliokuwa nao nikiwa gerezani juu ya ugonjwa wa baba yangu mzazi mzee Elias Lwakatare aliyeletwa Dar Es Salaam kwa ajili ya matibabu,athari za mke wangu kuathirika kimasomo huko chuo kikuu Mzumbe aliko,mshtuko kwa watoto wangu shuleni na ugumu wa karo zao za shule,kuwaweka roho juu kaka,dada na ndugu zangu,kuvurugika kwa kazi za chama ofisini kwangu na mkoani kwangu Kagera n.k,binafsi nililiona tukio hilo kama nafasi nyingine kwa chama chetu kujitambua na kujipima udhaifu tulionao,nguvu tulizonazo na fursa tulizonazo wakati tunapoelekea kuikamata dola.Niliisoma makala mojawapo ya Mwanakijiji katika toleo mojawapo la Tanzania Daima,niliipenda sana na niliguswa. Makala hiyo ilikuwa ikituasa CHADEMA kujitathmini. Ukweli wenyewe ni kama makala hiyo ya Mwanakijiji sisi kama CHADEMA ilituvua nguo na kutuacha uchi.
Kwanza tuhuma ya ugaidi niliiona kama kombora la mwisho la serikali ya CCM kukamilisha mkakati wao wa kuichimbia CHADEMA kaburi ambayo siku zote huwa ni ya pembe nne na katika kuichimba na kuifukia kawaida koleo lenye umbo la ‘U’ mbele na mpini wake hutumika.
“U” ya kwanza yenye kutubamkikizia tuhuma za ufamilia,Ukabila,Uchagga,Ukask azini alikuwa amebebeshwa mwenyekiti Mbowe zikashindwa. “U” ya pili yenye kuzoa tuhuma za Udini,Ukatoliki,Upadri alibebeshwa katibu mkuu Dr.Slaa nazo zikakwama CHADEMA ikapenya. “U” ya tatu yenye kulenga Uchonganishi,Umbea,Ufitinishaj i na Usongombingo, CCM wakalenga kumbebesha Naibu katibu mkuu kijana Zitto Kabwe lakini naye akawashtukia akawaumbua na kuwabwaga. Zitto ameendelea kuhimiza mshikamano mkubwa ndani ya chama na kuwaacha wapambe nuksi hoi. “U” ya mwisho yenye kubeba Ugaidi,Uuaji,Utekaji iliyolenga kukifuta kabisa chama vitabuni na kuwasweka viongozi gerezani, kabambikiziwa Wilfred Lwakatare Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama CHADEMA.Mungu mkubwa nayo hiyo mahakama kuu yenye baadhi ya majaji weledi wa sheria na wasiokubali mizengwe wameifutilia mbali.Hakika CHADEMA haizuiliki na kwa hakika lililobaki ni kulitumia koleo hilohilo na “U” hizo kuwafukia CCM humohumo kwenye kaburi walilojichimbia wenyewe. ‘Mchimba kaburi huingia yeye mwenyewe.’
Nashukuru CHADEMA hivi sasa imejipanga kama taasisi makini inayoongozwa na kusimamiwa kitaasisi na wala si kwa utashi wa mtu binafsi au kundi fulani la watu bali vikao vya kikatiba. Mshikamano wa pamoja na fikra zinazotuelekeza kulenga paala pamoja tulikodhamiria, hivi sasa ndiyo silaha kubwa na nusuru yetu kichama. Kama CHADEMA inavyoamini ; “TUNAANZA NA MUNGU, TUNAENDELEA NA MUNGU NA TUNAMALIZA NA MUNGU.”
I AM REALLY PROUD OF BEING IN CHADEMA FAMILY!!!
3: HALI NA TASWIRA YA POLISI MAGEREZA NA VYOMBO VYA KUSIMAMIA HAKI NA USALAMA.
Wakati nikihojiwa na jopo la maofisa wa makao makuu ya polisi la akina Mhigulu wakati huo akiwa Kaimu DCI na wenzake akina Obadia,Jonas,Simon Pasua,Beneth Kipasuka,Nyombi na wengineo baadhi yao niliwapa ujumbe wamfikishie ‘college mate’ wangu (IGP Said Mwema ) Chuo kikuu cha Dar es Salaam kuwa naziona jitihada na mbio zao za kuwatafuta hao watu wanaoitwa magaidi,wateka madaktari na waaandishi,wapiga risasi mapadri n.k mbio zao haziwezi kufaulu kutokana na namna wanavyoliendesha zoezi.
Niliwaambia ;wakati wao wako ndani ya land rover 109 kilomita arobaini nyuma yetu sisi tunaokimbizwa na kutuhumiwa kuhusu ugaidi na kupanga njama za kudhuru watu, wahusika halisi wa mambo hayo wako na Range Rover kilomita arobaini mbele yetu. Je,ni mwaka gani watawafikia na kuwaweka mbaroni hao jamaa?Hivi, kikosi cha IGP Mwema ambacho tumeelezwa ni maalum na kina makachero waliobobea kushindwa kurejesha mrejesho wa maana hadi sasa kwa angalau hata tukio moja, hivi watanzania hatushtuki tu? JK haushtuki ? Anyway,tuendelee kuwapa masurufu na kuwatengea mafungu tutaona! Sijui kama walinielewa au kumfikishia IGP Mwema huo ujumbe wangu.Na kwa kuwa asiyetaka kujua maana haambiwi maana basi tuendelee mambo ni kanyaga twende!
Wakili wangu Kichehere niliyekuwa naye katika mahojiano wakati nikihojiwa kituo cha kati alijaribu kuwapa changamoto japo chache za kupanua akili zao kuhusu huo unaoitwa ugaidi dhidi yangu na ‘ka-cd’ kao walikokachota kwenye mtandao wa “You Tube” (kama walivyotueleza) na kutuonyesha pale kwenye mahojiano. Hawakutaka kumsikiliza wala kumuelewa juu ya kasoro zilizojidhihirisha moja kwa moja . Hata pale alipowashauri kuwaita na kuwahoji baadhi ya watu muhimu walioonekana kuhitajika ili kuondoa walakini usio na sababu tangu mwanzo wa zoezi, hawakutaka kuuchukua ushauri huo. Wakaona waendelee kukimbia na hako ‘ka 109’ kao. Mimi naamini upo wakati ambapo mshtukiwa wa tukio linalochunguzwa aliye mzalendo na nchi yake anaweza kuwa msaada wa kuinusuru nchi yake anayoipenda endapo anapewa nafasi ya kutoa ushirikiano kwa njia za kuheshimiana kiutu .
Anyway,sijui mwisho wa mambo yote haya maana bado tuko safarini na bado nina kesi moja ya kujibu ya njama ya kumdhuru Denis Msacky kwa sumu (kwa mujibu wa maamuzi ya mahakama kuu ya jaji Kaduri).Sitaki kuingilia mwenendo wa kesi hiyo na nikajiibulia mengine.Lakini kaka yangu IGP Mwema endelea kutangaza bingo la mamilioni labda utafaulu,Inshallah!!
Ukiacha kesi yangu hiyo ya kutuhumiwa ugaidi, lakini kukaa kwangu pale polisi central (kituo cha kati),gerezani,keko na Segerea kumenithibitishia vituko na mambo chungu nzima niliyokuwa nikiyasikia nikiwa uraiani na kufikiria ni ya uongo. Vitendo vya watu kubambikiwa kesi viko njenje na wenyewe kwa lugha zao wanaita; “kumpa mtu kichwa! kumpiga mtu armed robbery! kumpeleka mtu mapumziko!n.k” Nafikiri watu wanaofanya vitendo hivi wanahitaji kufanyiwa ‘concelling…’ ( kupewa ushauri nasaha) kwani sio vitendo vya kiutu.
Hivi huu ni utamaduni gani na taifa tunalipeleka wapi? Hivi kweli inaingia akilini wakati mchezo kama huo ukiendelea na watu kibao kubambikiziwa kesi kwa ‘kupewa vichwa’ wakati huohuo mh.JK yuko ‘busy’ kuwatunuku watu nishani za utumishi uliotukuka? ‘This is a typical shame!!’ Sijui kama usalama wa Taifa wapo. Hivi wanafanya kazi gani kama hawamsaidii mheshimiwa Rais kumjuza kinachoendelea? Au ni ugonjwa uleule mchanganyiko wa ‘sisiemhosis’. Naanza kukubaliana na usemi wa mtu mmoja niliyeongea naye gerezani Segerea aliyesema vyombo vya kulinda usalama huenda ni vya kulinda usalama wa viongozi walaji,wahujumi wa nchi,mafisadi na mfumo aliouita ; “chukua chako mapema.”
Na ni vyombo vyenye weledi mkubwa wa kuchora michoro ya fitina,uongo,wizi,hujuma,kusam baratisha vyama vya upinzani kuiba kura kutisha watu kutengeneza kesi bandia,kuandaa mashahidi feki n.k. Matokeo yake watu ambao leo hii wamejaa na kurundikwa magerezani na mahabusu za polisi,asilimia kubwa wanakuwa hawana hatia wahalifu wakubwa wako nje wakiendelea kula nchi! Asilimia kubwa ya kesi zinazopelekwa mahakamani ni feki na ni za kuwachosha mahakimu na majaji bila sababu kwani kesi hizo huishia kufutwa.
Mrundikano mkubwa magerezani wa wafungwa na mahabusu unasababisha hata huduma ziwe mbovu. Wapo wafungwa hawana sare za gereza wanavaa kitu kinachoitwa ‘nusu mlingoti’, kauka nikuvae, sare zilizochanika kiasi cha kutia aibu.Na kwa kuwa hata sera za uendeshaji magereza nyingi ni zilezile za ‘vichwa vya ki-CCM’ (chama dhaifu,wabunge dhaifu na serikali dhaifu) hakuna akili inayoweza kubuni namna ya kuitumia kiufanisi nguvu kazi kubwa iliyojaa magerezani. Ndani ya gereza kuna kila aina ya fani na vipaji lakini vimelala tu. Kama vile CCM, hawazai na hawana watoto nyumbani, huwezi kuamini watoto lukuki waliorundikwa Segerea bila utaratibu mzuri wa kimalezi na kimakuzi hata kama baadhi yao ni wakorofi na wahalifu. Tutake, tusitake hawa ni taifa la leo na la kesho.Hawa ni nguvu kazi yetu ya nchi ,hawa wanahitaji kukunjwa wangali wabichi.
Watoto hawa ambao wengine ni wa umri wa miaka kumi wenye kesi za kuiba embe tano,kuiba simu, kudokoa pochi zenye elfu 30,000/=n.k,wamo gerezani wakinyweshwa uji asubuhi,ugali wa dona na mchuzi mwingi wenye maharage thelathini kwenye bakuli na muda unaobaki kuutumia kufundishana ngumi,kupiga ‘vice’, na mengine mengi. Kuna kitu kipya ambacho kimebuniwa na uongozi wa jiji la Dar es Salaam ‘kuusafisha mji’ kwa kuwaondoa barabarani na mitaani watu wote mafukara na wasio na uwezo mkubwa wa kipato. Hawa wote wanakusanywa kwa mamia kila siku na kurundikwa Segerea kwa shtaka moja tu linaloitwa “kesi ya kubughudhi abiria.”
Uwe umekamatwa unakojoa kichochoroni, unauza maji ya Uhai barabarani,machinga wa bidhaa,mpiga debe,unayemsubiri jamaa yako pembeni mwa barabara au kituo cha mabasi Ubungo, uwe ni mama lishe, ni ‘dada poa’ n.k,ukishashindwa kuwakatia elfu kumi au elfu tano jamaa hao wanaoitwa askari wa jiji au walinzi shirikishi, ujue wewe tayari unakwenda Segerea kwa kesi ileile inayoitwa ya ‘kubugudhi abiria’. Wakati huohuo bidhaa zako zote zinakwenda,masufuria na wali wa akina mama lishe unapelekwa kunusuru familia za wasafisha jiji hao,simu na pesa yoyote uliyonayo mfukoni inakwenda;yaani ni kiama! Jamani, waheshimiwa wabunge na madiwani wa jiji la Dar es Salaam hususani wa CHADEMA chukueni hatua za haraka.
Mzee kikwete upo hapo? Unakumbuka ahadi zako za hotuba yako ya kwanza bungeni Dodoma na wakati ulipomaliza ziara yako ya magereza ya Keko na Segerea mwaka 2007? Achana na hayo yote,sasa njoo gerezani upate picha ‘live’.
Nikiwa kwenye selo yangu,kwa bahati nzuri niliruhusiwa kuletewa magazeti na kusikiliza redio . Siku moja wakati nasikiliza kipindi cha Bunge, Naibu waziri wa mambo ya ndani akijibu hoja za wabunge kuhusiana na hotuba ya bajeti yao iliyokuwa imewasilishwa na bosi wake Dr.Nchimbi, nikamsikia akizungumzia swala hilo la upekuzi wa wafungwa na mahabusu kwa utaratibu unaoonekana kumdhalilisha binadamu. Naibu waziri anasema tatizo hilo lipo lakini kutokana na ufinyu wa bajeti hawawezi kununua vifaa vya kisasa vya kufanyia upekuzi. Akasema kutokana na hali hiyo,wataendelea kutumia njia hizohizo za ‘ubunifu’ mpaka hapo serikali ya CCM itakapokusanya mapato yanayokidhi bajeti inayoweza kuvinunua vifaa hivyo.
Wakati wa kupitisha mafungu,jamaa wakapitisha pesa ya kununua chai,vitumbua,maji ya kunywa,ziara za viongozi,ununuzi wa magari,semina,warsha,mafunzo ,motisha n.k. Nikajiuliza,hayo mambo ndiyo kipaumbele kweli hata kuliko kuyanunulia magereza mashine mojamoja za kufanyia upekuzi? Taasisi mbalimbali za haki za binaadamu ni kweli zinafanya kazi nzuri kwenye mitandao ,uitishaji semina,uandikaji ripoti nyingi nzuri zinazotumwa kwa wafadhili ili michuzi izidi kutoka n.k. lakini nasema haitoshi. Tembeleeni magerezani msiishie kwa bwana Jela , ombeni kutembelea maeneo yote na kuongea na wafungwa . Kwa njia hiyo mtaboresha kazi yenu kwa uzuri zaidi.
4: SALAAM TOKA MAHABUSU, POLISI NA GEREZANI.
Mwenyekiti Mbowe alipokuja gerezani Segerea kunitembelea akiwa na Mkurugenzi wa mambo ya Bunge na Halmashauri Bwana John Mrema alinipa kazi ya kukijenga chama humo humo ndani gerezani . Nitakua namkosea adabu nisipo fanya mrejesho wa kazi yake. Na kwa kuwa mengi ya yale niliyoyafanya na kuelezwa na wadau wangu yanatuhusu sisi wote kama viongozi wa CHADEMA, wanachama na hata wanachama watarajiwa, sio vibaya nikiyaweka hadharani. Ya Mbowe kama Mbowe nitamuwasilishia yeye mwenyewe kwa muda muafaka.
Wafungwa, mahabusu, baadhi ya watumishi wa gerezani, mapolisi na wengineo wanatoa salamu nyingi sana. Wengi wanaipongeza kazi inayofanywa na CHADEMA ndani na nje ya bunge. Wanasema karibu wote ni CHADEMA japo wengi hawana kadi. Ili upokelewe vyema gerezani lazima uwe ‘vidole viwili’ ukijitia ‘ukada’ utalijua gereza. Wanasema kamwe wabunge wa CHADEMA msitiwe woga na tambo za wabunge wa CCM ndani ya bunge kwa kujiona wako wengi wakifikiria huo wingi upo hata nje ya mjengo. Wanasema katika hilo ‘wamebugi meen!!’. Nje ya Bunge CHADEMA mna mashabiki na wafuasi nyomi!! Yaonekana kwa hivi sasa Bunge ni uwanja wa nyumbani anaoutumia CCM kimchezo na ninyi CHADEMA uwanja wenu uko huku uraiani kwa umma.
Wanasema vitendo vya dada Makinda na mwenzie Job Ndugai wameshavipigia hesabu. Mwisho wao hauko mbali , ninyi kazi yenu ni kukaza buti bila kulegeza. Wamenituma niwaambie, maana mjumbe huwa hauwawi!, eti CHADEMA nje ya Bunge tusiendelee kupoteza muda kuwahubiria watu ufisadi, wizi, manyanyaso ya vyombo vya dola vya serikali ya CCM, kushindwa uongozi kwa serikali nzima ya CCM, umaskini mizengwe ya CCM katika kuandikwa kwa katiba mpya n.k. Wanasema yote hayo wameshayaweka kichwani na wanajionea wao wenyewe kama waathirika namba moja wanatambua fika kwamba wamo ndani ya gereza kwa sababu ya mfumo uliosababishwa na kutengenezwa na CCM.
Wanasema katiba halisi ya watanzania itaandikwa baada ya CHADEMA kuingia ikulu kwani CCM ni mizengwe mitupu.CCM hawajaanza leo, kumbukeni yaliyompata Jaji Kisanga na Tume yake walipoambiwa na Mkapa kwamba wamewasilisha taarifa ya mambo ambayo hakuwatuma. Wanasegerea wanasema elekezeni nguvu zote kwa kipindi hiki kilichobaki kabla ya chaguzi za 2014 za serikali za mitaa na ule mkuu wa 2015 kuwapanga wapiga kura kiuchaguzi .
Lipigwe jaramba na kuwekwa mpango mahususi utakaowezesha kila aitwaye mtanzania mwenye umri wa kupiga kura apate uhalali wa kupiga kura. Uwekwe mfumo wa kubanana kuhakikisha watu wanajipatia vitambulisho vya uraia wanatunza shahada zao au vitambulisho na wanakwenda kupiga kura. Wanaamini kwa hali ilivyo hivi sasa, ni binadamu ‘asiye majaliwa’ au wale wachache wasiojaa kiganjani waitwao ‘CCM maslahi’ watakaothubutu kuelekeza kura zao kwenye rangi ya kijani- mchicha, kisamvu!
Wamo baadhi ya wafungwa na mahabusu walionieleza kwamba walikua CCM kufa mtu na walishiriki kwenye hujuma mbalimbali na hata kuiba kura, lakini hivi sasa wamekoma kwani wametumika kama karai na kisha kutelekezwa nje ya jumba walilosaidia kulijenga na ndio maaana wanaozea jela. Baadhi ya mbinu walizokua wakizitumia kutuibia kura wamenieleza na nimetoka nazo kibindoni.
Wamenituma niwaeleze, kwa kipindi kilichobaki, ‘chonde! Chonde! acheni kugombana, kurumbana na kufukuzana. Tumieni kipindi hiki kujenga mshikamano utakaowezesha kukisuka kikosi cha ‘Real Madrid’ au ‘Manchester United’ ya siasa za Tanzania ili uchaguzi ujao CCM walazwe chali-mwanguko wa kifo cha mende! Wanasema CCM ni wepesi kama nyama ya maini, wakibanwa kwenye kumi na nane hawana ujanja wataachia tu , tatu bila!!!
Wameniambia hivi sasa CHADEMA ni chama kikubwa chenye uwezo wa kubuni njia mbalimbali mbadala zinazoweza kutumika kuwadhibiti viongozi wowote au wanachama wanaodiriki kukivuruga chama makusudi au kukihujumu badala ya kuchukua hatua za kuwafukuza.
Wanampongeza na kumpa heko Mwenyekiti wa chama kwa umahiri na ubunifu wake uliokifanya chama kikue na kupanuka kwa haraka. Kwa lugha zao wanasema Mbowe ni jembe na ni kichwa,anafanya kazi nzuri ya kutengeneza timu kwa lengo la kushinda mechi. Wanamshauri ajitahidi kuona namna ya kuumudu mchezo ulioko mbele yetu 2014 na 2015. Iangaliwe karata zitachangwaje? Wanasema ni vyema tukajifunze namna mchezo wa siasa za Kenya ulivyochezwa dakika za lala salama za uchaguzi wao. Wanatambua na kupongeza namna CHADEMA ilivyomuunga mkono Kamarade Odinga na muungano wake wa ACCORD, lakini kwa msingi wa kujifunza mbinu za kuusaka ushindi , tuangalie na kujifunza namna Kenyatta alivyoubadili mchezo. Kwanza kwa kumudu kuunda chama kipya na kukijengea mtandao ndani ya muda mfupi.
Pili alivyoweza kuwavuta na kuwashawishi waliokuwa mahasimu wake walio muhimu (kama vile Ruto) ambao bila ya kuwa nao asingeweza kufua dafu kwa Odinga. Tatu , namna Kenyatta alivyocheza mchezo wa kisiasa kwa kuzingatia na kutumia kanuni isemayo ‘siasa hazina rafiki wala adui wa kudumu’ bali ni kuangalia nani anawezesha kupenya vikwazo ili kuwezesha kufika salama ninakokwenda (kwa maana ya kuingia Ikulu). Ukishaingia ndani ya mjengo mambo mengine ni akili kichwani, utajua unachemsha vipi kichwa lakini muhimu kuliko yote si tayari umo ndani na unachezea ndani? Wanamuomba Mbowe azidi kuzamisha akilli na kuupanga mchezo kwa “formation” ileile ya Kenyatta, lakini kwa kuongezea na mbinu nyingine zinazozingatia mazingira yanayotunzunguka KICHADEMA.
5: NIMEKUTANA NA SHEIKH PONDA
Milima huwa haikutani lakini binadamu wanakutana. Ndivyo sakata la ugaidi lilivyonifikisha gereza la Segerea na huko nikajikuta nawekwa selo moja na ‘mjukuu wangu’ Issa Ponda mtoto kutoka Kigoma. Issa Ponda ni kiumbe wa mwenyezi Mungu wa aina ya pekee. Kwa nchi za wenzetu zilizoendelea mtu mithiri ya Ponda si mtu wa kuchukulia mzaa kama ninaouona ukichezwa hapa kwetu. Ni mtu ambaye fikra zake, ubunifu alionao kichwani na katika vitendo, hulka zake, nasaha zake, ushawishi wake, ujengaji hoja zake, uchaji wa Mungu wake, uswalihina wake na vingine vingi ni watu wachache sana unaoweza kukutana nao wakiwa navyo vyote kwa mpigo.
Ponda tofauti na namna mfumo unavyomchukulia, ni mtu ambaye angetumika vyema kwa kusikilizwa sehemu kubwa ya mawazo yake na yakafanyiwa kazi ipasavyo, nina uhakika mambo mengi tunayoyaona yana mitafaruku ya kidini yasingelikuwepo.
Tatizo wakubwa wanamuangalia kwa taswira ya upande mmoja ya kumuona ‘mkorofi, mchochezi’. Sijui na ndio maana nauliza, hivi ni mamlaka gani ya juu na yenye kauli ndani ya nchi hii imewahi kukaa na Ponda kwa karibu katika misingi ya kuheshimiana kwa dhati na kusikilizana ili kujua ana mawazo na mitizamo gani kwa masuala mbalimbali yaliyolalamikiwa na baadhi ya waislamu walio wengi?
Nimeishi naye zaidi ya siku 60 selo moja kwa masaa 24 karibu kila siku na masaa mengi tukiwa wawili tu, mimi na yeye. Ni mdadisi wa kupenda kujua, na ukisha mwelewesha ni mwepesi wa kuelewa na kujenga fikra mpya. Hivyohivyo siyo mchoyo wa kuyabania maarifa aliyonayo na elimu kubwa ya kidini aliyobahatika kuipata.
Alinielewesha kuwa kwenye dini ya kiislamu mtu anapokuwa amefikia kiwango cha kuitwa U-Ustadhi kwa lugha ya haraka inayoeleweka na wengi ni sawa na U-profesa.Hakika Sheikh Ponda ni ‘profesa’.
Nilipata fursa ya kujadiliana naye pia mambo ya msingi yanayolikabili hivi sasa Taifa letu. Moja wapo ni nguvu nyingi zisizo na sababu zinazotumiwa na polisi kushughulika na watu kama sisi ambao hata rungu hatuna. Nguvu kubwa inayotumika ya kumpeleka Ponda au Lwakatare mahakamani ili kesi itajwe tu na kurudi Segerea kulala ni sawa na kumlipa daktari wa muhimbili mishahara mizuri ya miezi miwili. Magari nane na mapikipiki kujazwa mafuta,ving’ora barabarani,askari polisi zaidi ya hamsini kuvunja shughuli nyinginezo kwa siku nzima, barabara kufungwa na mengine kuzuiwa wakati wa kupita n.k Mikwara yote hiyo ya nini?
Mfungwa mmoja aliyesoma kwa kiwango fulani alipoletwa kulala kwenye selo yetu na kuikuta mada hiyo, alichangia hivi, “kawaida ya mtu yeyote anayelazimisha aonekane mbele ya wakubwa zake kwamba anafanya kazi ni lazima atengeneze mazingira yanayomfanya aonekane kweli anafanya kazi”. Kisha kasema hivi “nyie waheshimiwa ili wale waliowafungulia tuhuma za ugaidi na uchochezi lazima watoe taswira ya nje kwa umma kuonesha kuwa ninyi ni watu hatari sana na mkipewa upenyo wowote mnaweza kusababisha maafa makubwa sana wakati wowote kwa taifa. Kwa ufupi wanataka umma uwahukumu kinadharia kwamba mnahusika na tuhuma mlizoshtakiwa nazo hata kama mahakama haijazipitia tuhuma zenyewe kuona zina uzito gani.”
Nilimuelewa vizuri sana na kukubaliana na huyo mfungwa maana vyombo vyetu hivi vya dola wakati mwingine vinapenda kutumia nguvu nyingi sana katika jambo dogo sana kwa sababu tu za kuridhishana na makundi fulani au kulinda nafasi zao za kazi ambazo hawazimudu.
Jambo jingine lililoangukia katika mijadala yetu ni hii migogoro ya makundi ya kijamii na hata mauaji na maumizano yanayojitokeza mara kwa mara. Sheikh Ponda alitoa changamoto moja muhimu ambayo naona ina mashiko sana. Alisema hivi; huko uswazi (mitaani wanakoishi watu wengi kwa kubanana) ambako nyumba moja wanapanga na kuishi zaidi ya watu hamsini, mchanganyiko wa waislamu kwa wakristo, mbona hakuna ugomvi? Mbona akina mama humo ndani waislamu kwa wakristo wanaachiana watoto kwenda sokoni? Mbona wanaazimana vijiko na masufuria? Mbona wanapeana mboga bila kuulizana? Ponda akatumbukiza na utani pia kuwa “mbona humu selo ukileta chakula alichopika mama Frank siulizi na wala wewe chakula anachoniletea mama Mariam naona unabugia tu bila maswali yoyote?
Na mimi nikamwambia mbona ukiamka saa tisa usiku ukaanza swala zako za sunna mpaka alfajiri wakati wa ‘Azanna’ na kisha swala zote tano za ‘faradhi’ za siku nzima na lakhai zake mbilimbili humu humu ndani ya selo havijaingiliana na ibada zangu za ‘Tumwabudu Mungu wetu?’ Selo yetu ndio msikiti wetu na ndilo kanisa letu. Haya mambo chanzo na chimbuko lake ni nini? Hayawezi kuwa yanatengenezwa na kundi maalum la watu kwa malengo maalum?
Swali hili la mwisho likanikumbusha somo moja tulilowahi kufundishwa kipindi fulani nilipokwenda Ujerumani kwa mafunzo ya ‘Strategic Planning’. Katika kipengele kimojawapo cha mafunzo hayo nakumbuka kuna kitu mwalimu alikiita ‘Power Winning and Maintaining Strategy’, kwa tafsiri nyepesi ‘mkakati wa kuupata utawala na kuulinda’.
Katika mkakati huo nakumbuka alitwambia, kuna wakati watawala fulani wanapoelemewa na mambo au jambo wakakosa majibu mbele ya watawaliwa wanaotaka kujua kulikoni ili kuzima mambo hayo aidha ni kutumia nguvu na fursa zilizopo kumshughulikia kinara mmoja anayeonekana kimbelembele kuhoji.
Mkisha mziba mdomo kwa njia zozote zinazowezekana walio nyuma yake wataufyata tu! Njia nyingine ni kuibua au kufanya jambo fulani kubwa bila kujulikana linaloweza kusaidia kuwahamisha watu kifikra toka jambo jingine lililopo ambalo ni hatarishi zaidi kiutawala.
Njia nyingine ni ile iliyotumika tangu ukoloni ya ‘watawanye uwatawale’ (Divide and rule policy).
Ukiwapa nafasi au fursa watawaliwa wakakaa, wakapanga wakaelewana na nyie mpompo tu mkiwaangalia, jua siku watakapozua ajenda ya kushughulika na wewe, ujue umekwenda. Dawa ni kuwafanya siku zote wasielewane kwa kuwagonganisha vichwa wenyewe kwa wenyewe tena kwa mambo madogo yasiyo hitaji gharama kubwa na nguvu nyingi. Tulijadiliana sana na kwa urefu na Sheikh Ponda juu ya mambo haya lakini hatukupata jibu la mwisho na kwa bahati mbaya au nzuri Mungu akawa amezisikia dua zake na sala zake za masaa zaidi ya 18 kila siku akawa amechomolewa Segerea na kuniachia Sello No. 3. Najua Mungu atatukutanisha tena Inshallah! Ila, isiwe tena Segerea au Keko ili tuhitimishe mada hiyo.
Siku moja kabla ya kusomewa hukumu yake na Hakimu Nongwa (9/5/2013) tulijadili sana hukumu yake kwamba inaweza kuwa ya mwelekeo gani na maamuzi yapi. Panga pangua ilishindikana kueleweka mambo yatakuwaje kutokana na mazingira yaliyokuwa yakiizunguka kesi yenyewe. Mawakili wake walikuwa wameifanya kazi yao vyema bila kubakiza punje ya shaka. Lililokuwa likimpa faraja zaidi na kesi yake ni kusikia kwamba huyo hakimu ni mama mlokole, ameokoka. Hiyo ilikua ikimpa moyo sana kwamba atahukumiwa na kupewa haki yake sawa na lile lililozungumzwa na kuwasilishwa mbele ya hakimu Nongwa.
Nilimuuliza endapo hukumu itamuweka katika mazingira ya kumkata makali yake ya kazi ya utetezi anayoifanya na wakati huohuo upande wa pili wa ‘system’ ukamtaka aanze kutoa ‘Ushirikiano’ atafanyaje? Sheikh Ponda aliniambia kuwa haki huwa hainunuliwi wala kuombwa bali hudaiwa. Alisema atakuwa tayari kutoa ushirikiano kwa yeyote yule anayezungumzia utoaji na upatakanaji haki.Na akasema mdomo na nafsi vilivyodhamiria kuzungumzia na kuitafuta haki huwa havifungiki kwani vikifungika hata hiyo amani haiwezi kuwepo.
Nikiwa ndani ya selo nilimsikia Sheikh Ponda akimwaga mistari yake redioni baada ya kuhukumiwa. Kwa mara nyingine nikazidi kumuaminia Sheikh Ponda kwamba ni mmojawapo ya watu wachache tulio nao hivi sasa nchini wanaoweza kutembea na kuishi ndani ya maneno yao.
Lipo jambo moja muhimu ambalo tulikubaliana na Sheikh Ponda tulijadili na kulifanyia kazi kwa nia ya kuwanusuru watu wanaosota jela bila sababu endapo tungeliachiwa na kuwa huru uraiani. Namtafuta kwenye simu hayuko ‘reachable’. Nikishampata tukashauriana na likaonekana linatekelezeka, nitalitoa hadharani.
6: USHAURI WANGU MDOGO KWA VIONGOZI WETU WA DINI.
Mimi ni mtu mdogo sana na muumini wa kawaida ndani ya dhehebu la KKKT. Lakini natambua kanisa ni waumini na wajibu mkubwa wa kila muumini ni kuhakikisha anatimiza wajibu wake kama kanisa la Mungu linavyoelekezwa kupitia maandiko matakatifu ya Biblia. Wajibu mmojawapo sisi kama waumini ni kuonyana ( Ebr. 10:24 – 25).
Nawaombeni viongozi wetu wa dini zote wakristo kwa waislamu mtimize wajibu wenu mliokabidhiwa na Mungu, Imeandikwa kwa dini zote kwamba kila mmoja bila kujali wadhifa wake atahukumiwa sawa na matendo yake. Nawaomba simamieni na kuuzungumza ukweli(hata kama ni mchungu) mbele ya watawala na hata watawala watarajiwa.Ninyi mmepewa mamlaka na Mungu ya kuonya, kukemea, kuelekeza na kubariki na ndio maana watawala wote wanawaogopa na kuwaheshimu. Wengine huenda ninyi bila ya kuwatambua hutafuta njia za kujikomba kwenu ili wakipate wanachokitafuta.Yasemeni wazi na kuyahoji hata yale machache yanayoonekana au kusikika pasipo kificho.
Muulizeni Mheshimiwa Rais huyo waziri wake anayezungumzwa kila siku kwamba mchana kweupe alisema anao maadui zake wawili ambao ni waandishi wa habari na angewashughulikia, Rais analisemaje hilo? Maadam ni ninyi, nina uhakika Mheshimiwa Rais atajibu na atachukua hatua stahiki.
Binafsi nawaombeni kwa heshima na taadhima muache kuwa vuguvugu (si moto si baridi-Ufunuo wa Yohana 3:15-16) Baadhi yenu acheni kuogopa vivuli vyenu kwa maana ya kuhofia kunyimwa upendeleo au misaada ya serikali (i.e misamaha ya kodi) na baadhi kuutumia mwanya huo vibaya. Kama maandiko yanavyosema JIKANENI WENYEWE.
Lazima mtambue hawa jamaa wakati mwingine huenda wanaitumia fursa hiyo kama chambo cha kuwanasia pindi wanapokua wana taarifa zenu zote za fursa ya misamaha iliyotumika vibaya. “Mnapaswa kushuhudiwa mema na watu walio nje…” (1 Tim 3:2-9)
Binafsi nawaomba msiwalee wala kuwabeba wale wote wenye dhamira chafu na nia mbaya ya kutaka kuyatumia madhehebu yenu kukidhi matakwa binafsi kwani wanachafua taswira zenu nzuri za madhehebu yenu mbele ya waumini wenu na umma kwa ujumla.
Lakini zaidi ya yote ni imani yangu mimi binafsi kwamba madhehebu yenu ni makubwa na yana mtandao mkubwa na wenye nguvu ndani na hata nje ya nchi.Kama inawezekana tumieni mtandao wenu kuisaidia serikali ambayo vyombo vyake vinaelekea kushindwa kuwabaini wahalifu wachache wanaoelekea kuchafua na kuivuruga amani tuliyoizoea ndani ya nchi yetu. Kwa bahati nzuri nimesoma na kusikia kwenye vyombo vya habari kwamba IGP Mwema amezishauri taasisi za kidini kuanzisha ‘ulinzi shirikishi ndani ya misikiti na makanisa’. Kama mambo serikali ya CCM imeyafikisha hapo, tumieni fursa hiyo kuziomba taasisi makini mnazozifikia nje na ndani ya nchi.
7: MTIZAMO WANGU WA MBELE BAADA YA SAKATA LA UGAIDI.
Mimi kama mimi na wakati huohuo Mkurugenzi wa ulinzi na Usalama wa CHADEMA, kanuni yangu ya maisha ya kila siku huwa ni kutoangalia yale yaliyokwisha kuniumiza bali ni kuangalia yanayoweza kuniumiza kuanzia leo na kwenda mbele.
Ushauri wangu wa namna gani twende katika kukilinda chama kwa ujumla wake nitawasilisha mbele ya mamlaka na vyombo husika vya Chama.Lakini rahi kwa wanachama wa CHADEMA na wapenda mabadiliko ya kweli wote nchini, ni kulichukua jukumu la kuzilinda harakati hizi zinazoendelea kama jukumu letu wote na kila mmoja kujiona anahusika na anaguswa. Chukua hatua kuyadhibiti yale unayoweza palepale ulipo na yanayokushinda toa taarifa au tafuta msaada kwa mtandao wa chama chetu ambao hivi sasa unaendelea kujikita maeneo yote nchini.Asiye na Uongozi wowote ndani ya chama wala kadi lakini anajisikia kwenye nafsi kuipenda na kutaka kuitumikia CHADEMA, naomba achukue cheo cha u-volunteer na aingie kazini kuanzia dakika hii na sisi tutaitambua na kuienzi kazi yake.
Kwa viongozi wangu wakuu na wale wote waliopewa dhamana ya kukisimamia na kukiongoza chama katika ngazi na nyadhifa zozote, Sioni njia ya kutuvusha na kutufikisha haraka tunakokwenda zaidi ya kuziendesha kazi zetu kwa falsafa ya USIMAMIZI LAZIMISHI (Lwakatare Theory). Ni kheri ya fedheha kuliko lawama. Tujitahidi kuyafanyia tafsiri ya kutekelezeka mambo yote tunayoazimia au kuyapanga kufanyika. Kwa njia hiyo nina uhakika rasilimali zetu tulizonazo (fedha kidogo watu wengi) zitaweza kutuvusha na kuyashinda mapambano yaliyo mbele yetu.
Kukaa kwangu mahabusu siku 92 kumenipa fursa ya kuyatafakari mambo mengi kwa kina yanayonizunguka.Nimeamua NIFUNGUKE. Kufunguka kwangu ni pamoja na kujitokeza hadharani kwenye mitandao ya kijamii kama hivi sasa nilivyoamua kufanya jambo ambalo nilikuwa nalikwepa kutokana na watu wengi kutumia vibaya fursa hii ambayo binadamu ameigundua.
Nilipojiunga CHADEMA, nilimuuliza mwenyekiti angependa niifanyie nini CHADEMA kama sehemu ya mchango wangu katika harakati za kutafuta ukombozi zinazoendelea.Aliniambia kama naweza nitumie uzoefu mdogo niliokuwa nao kuanzia CUF wa kutengeneza mfumo wa ulinzi na usalama wa chama. Mimi sijawahi kusomea upolisi, ushushushu wala uanajeshi labda jeshi la kujenga Taifa mwaka 1982 Makutopora JKT Operesheni wajibu kwa mwaka mmoja. Lakini pia japo kidogo ujumbe wangu wa muda mrefu ndani ya kamati ya ulinzi na usalama ya CUF-Taifa, nao unaweza kuwa ulinisaidia kunitoa tongotongo kwa kiasi Fulani.
Nikiwa gerezani Segerea nilimshangaa sana ‘bwana mdogo’ Julius Mtatiro-Naibu Katibu mkuu wa CUF alipozungumza kwenye vyombo vya habari kuwa ;”Lwakatare akiwa CUF hatukumfundisha ugaidi.” Sikumuelewa hayo maneno alikuwa na maana gani na alitumwa na nani. Kwanza sijui kipindi hicho nikiwa CUF yeye alikuwa wapi na sidhani kama kwa wakati huo alifikiria hata kujiunga na hiyo CUF.Awaulize CUF ‘Original’ kama wapo, Lwakatare alikuwa ni nani ndani ya CUF.
Hata siku moja haitatokea nibeze uzoefu na msingi wa kisiasa nilioujenga ndani ya akili zangu na nafsi yangu kutoka CUF. CUF iliniweka katika ramani ya kisiasa ninayoitumia kutamba hadi leo hii. CUF ilinijengea nguzo moja kubwa iliyonipaisha kisiasa na inayoendelea kunisaidia katika kazi niliyokabidhiwa CHADEMA ya ulinzi wa chama hadi leo ambayo ni UJASIRI WA KUJITOA KWA NAFSI YANGU NA KWA AKILI ZANGU ZOTE KUIPIGANIA NA KUITAFUTA HAKI BILA KUCHOKA NA KUTOKUBALI DHULUMA NA UONEVU. ‘HAKI HUWA HULETEWI KWENYE KISAHANI CHA KIKOMBE CHA CHAI, HAKI HUDAIWA NA KUTAFUTWA.’
Ukisha kuwa na nguzo hiyo, ni silaha tosha inayoweza kumsaidia mtu yeyote Yule kuyaongoza au kushiriki ipasavyo katika harakati za kimapambano. Ndio maana leo hii, wapo wanajeshi, mapolisi, usalama wa Taifa wengi mno ambao serikali ya CCM imewadhulumu na kuwanyanyasa isivyo kawaida lakini kwa sababu ya kukosa nguzo hiyo niliyoisema hawathubutu kujitokeza hadharani. Ganzi la CCM la kuwafanya wawe waoga au wasijitambue limewakolea kwelikweli, hawathubutu kufurukuta.
Wachache wanaojaribu na kuthubutu kujitokeza wanapenda wafanye hivyo kwa kutokea mafichoni. Binafsi nawapongeza angalau hata kwa hilo maana najua ipo siku ambayo haiko mbali, ngoma itakapokolea watajitokeza hadharani kucheza. Kitendo hiki cha kuvishwa tuhuma za ugaidi na kikosi cha Mwigulu na CCM wenzake kilitukatisha sana ‘stimu’ ya kazi nyingi tulizokuwa bado tukizipanga. Kwa wahaya wanasema, “Bampeya ntakamazile…”kwa maana ya kukatishiwa safari kabla ya kufika mwisho wa safari. Makamanda tukaze buti, tushirikiane kwa dhati tusonge mbele mpaka kieleweke, neema inakuja.
Afya yangu nikiwa gerezani imeathirika kidogo na kunilazimisha kufanya vipimo ambavyo wataalam wamenieleza vinampunguzia mtu maisha yake ya kuishi. Siliogopi hilo najua tunaye Mungu, hata nikiondoka mimi kesho makamanda wengine wanaendelea na kazi na kusonga mbele.
Nikiwa gerezani nimezitumia siku zangu 92 kutengeneza andiko la toleo langu la kwanza la kitabu nilichokipa jina;
“USHINDANI NDANI YA MFUMO KANDAMIZI (SAFARI YANGU KISIASA HADI KUTUHUMIWA KUWA GAIDI ASIYE GAIDI).
Nimeona ni wakati muafaka kwa baadhi ya watu wenye nia nzuri na hata mbaya wasionijua Wilfred Lwakatare ni nani wanijue maana nikiwa gerezani yuko mwandishi mmoja wa gazeti la TAZAMA aliandika makala yenye mtazamo wa kubeza akiuliza, “kwani Lwakatare ni nani?” Maneno yaleyale aliyoyatumia Waziri Steven Wassira kwa mwandishi Absalom Kibanda.
Naamini kazi na uzoefu nilioupitia wa uanafunzi hadi chuo kikuu, uafisa utawala na utumishi serikalini, ujasiliamali, ukulima, ufugaji, uenyekiti wa mtaa Omukituli Kibeta, uenyekiti wa CUF na CHADEMA mkoa, ubunge wa jimbo, ukuu wa upinzani Bungeni,uratibu mkuu wa ushirikiano wa vyama vya CHADEMA, NCCR-Mageuzi, TLP na CUF, unaibu katibu mkuu wa CUF, ukurugenzi wa ulinzi na usalama CHADEMA, ukuu wa familia ya mke na watoto wanne na HATIMAYE kujikuta mahabusu nikituhumiwa kuwa GAIDI ASIYE GAIDI – sio kazi za mchezo. YATAKA MOYO.
Lakini pia nimeona si vibaya nikaonyesha uzoefu niliopitia kisiasa kwa wengine ili pale nilipokosea basi wengine wasitumbukie katika makosa yaleyale niliyoingia. Na kama yapo mazuri ya kujifunza, basi wayachukue na pengine kuyaboresha zaidi ili yawe chachu ya kuwatengenezea njia katika kufanikisha malengo yao na hasa ya harakati za kisiasa.Kwa wale watakaohitaji toleo la kitabu hicho wasisite kuwasiliana nami kwa kunipigia simu au kutuma ujumbe wa maandishi 0713 237869, 0758 417169, 0786 774697 au barua pepe lwaks62@hotmail.com. Kwa wale wanaotaka kunisaidia kwa namna moja au nyingine kuhakikisha toleo hilo linatoka kwa haraka na kwa viwango, nitawashukuru kwa mikono miwili.
8: USHAURI WANGU WA BURE KWA CCM NA WATANZANIA KWA UJUMLA.
Waswahili husema ukishikwa, shikamana. Maana tunakoelekea sio siri CCM wameshashikwa pabaya . CCM hawana namna ya kuyakwepa mabadiliko ya nyakati. Kukunjwa ni kuzuri kuliko kuvunjwa. “If they can’t change, changes will change them.”
Watanzania ambao bado wamesinzia tokeni usingizini. Acheni kugeuzwa mazezeta na CCM kiasi cha kushindwa kujitambua utu wenu kama watu na ubinadamu wenu kama binadamu wanaoishi katika Taifa huru. Waache ushamba wa kuendelea kufikiria kwamba bila kuilamba miguu CCM hawawezi kufanikiwa katika shughuli zao. Ukombozi wa kifikra ni mkubwa zaidi kuliko ukombozi wa kutoka utumwani.
Wajiulize wataendelea kuishi maisha ya kila kitu ‘deal’ na uchakachuaji mpaka lini? Hawaoni kuwa ni utumwa wa kujitakia wenyewe? Naona hata baadhi ya hizi kesi zinazofunguliwa ni zenye msukumo wa ‘DEAL’. Wafanyakazi na watendaji ndani ya serikali na taasisi zake nawashauri anzeni kubadilika na kujipanga kifikra tayari kutumika chini ya utawala wa chama chochote. Anzeni kujiunga na chama chenu cha AGIP (Any Government In Power) ambacho sio lazima kisajiliwe wala kutoa kadi.
9: SHUKRANI.
Kipindi cha kukaa kwangu gerezani kililikua cha mtihani mkubwa kwangu ambacho kimenipa mafunzo tosha katika maisha. Gerezani sio mahala pa kumuombea au kuombea mtu kupelekwa . Ni mahala ambapo kwa wengine panakua chanzo cha familia kugombana, kufarakana, kusambaratika, ndoa kuvunjika na uadui kujengeka baina ya mtu na mtu, na mengine mengi. Baadhi nimeyashuhudia mimi mwenyewe kwa macho yangu.
Binafsi nashukuru kwa ukaribu niliopewa na familia, ndugu, jamaa, marafiki, viongozi wa chama, wanachama na wanajela wenzangu. Ukaribu wao wa muda wote uliifanya siku iwe fupi.Sio siri ndugu zangu, unapotembelea ndugu yako aliyeko gerezani furaha unayomuachia mule ndani haipimiki.
Namshukuru sana mke wangu Angel Mercy kwa kukikabili kipindi chote hicho kigumu kwa kunipa huduma, kufuatilia afya yangu, kuiangalia na kuitunza familia iliyopo nyumbani na watoto walioko mashuleni licha ya yeye mwenyewe kukabiliwa na masomo chuoni,Mzumbe-Mbeya.
Nawashukuru sana ndugu zangu kaka, dada zangu, ndugu, marafiki, majirani na watoto wetu wote kwa misaada waliyonipa kupitia kwa mke wangu lakini kubwa kuliko yote kitendo chao cha kuja kuniona gerezani. Nikishukuru chama, (CHADEMA) kwa kunipigania na kunitolea misaada isiyohesabika. Kipekee nimshukuru sana Katibu Mkuu Dr. Slaa kwa ufuatiliaji mkubwa alioufanya.
Pongezi na shukrani nyingi kwa jopo zima la mawakili mahiri. Peter Kibatala, Tindu Lissu, Mabere Marando, Prof. Abdallah Safari na Nyoronyo kichehere, ambao najua bado tuko pamoja katika ngwe ya pili ya kesi ya shitaka moja ambalo bado linanikabili na huenda na mazagazaga mengine yanayoweza kujitokeza.
Nivishukuru kwa namna ya pekee vyombo vya habari vilivyofuatilia na vinavyoendelea kufuatilia sakata zima la kesi yangu na kuifahamisha jamii kujua kinachoendelea. Niwape pole na shukrani nyingi wale wote waliofika gerezani na kushindwa kuniona kutokana na idadi kuwa kubwa kuliko idadi ya watu walioruhusiwa kuniona.
Kipekee nimshukuru sana Baba Mchungaji wa usharika wetu wa King’ong’o Kimara na mke wake. Mr & Mrs Rev Joseph Kyaka walionitembelea na kunijengea moyo wa imani, matumaini na faraja. Niwashukuru wote waliokuwa pamoja nami kifikra na kimaombi na ninasema kwa maombi yenu, yote yamewezekana. Mungu anasikiliza maombi na haachi kujibu.
Nimuombe Mungu azidi kututangulia na kutupa ujasiri wa kukabiliana na adui na kumshinda shetani huku tukidumu katika imani.

IN GOD I TRUST.
IMEANDALIWA NA:
WILFRED MUGANYIZI LWAKATARE
MKURUGENZI WA ULINZI NA USALAMA CHADEMA.

VIA CHADEMA DIASPORA TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top