Juni 26 mwaka huu ilikuwa ni siku ya maadhimisho ya siku ya kupiga vita dawa za kulevya duniani. Maadhimisho hayo yalifanyika mjini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa Serikali na wadau wa janga hilo. 
Akizungumza katika maadhimisho hayo, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi aliyemwakilisha Waziri Mkuu Mizengo Pinda alisema wafanyabiashara wa dawa za kulevya ni watu hatari na kwamba, wanaweza kuingilia misingi ya kiutawala, hivyo Watanzania hawana budi kuipiga vita kwa nguvu zote.
Alisema iwapo biashara hiyo haitadhibitiwa kikamilifu na kuachwa ikaendelea moja ya athari zitakazojitokeza ni kuingiliwa kwa misingi ya utawala na ongezeko kubwa la rushwa.
Kauli hii inaonyesha kuwa Serikali imekata tamaa katika mapambano ya dawa za kulevya nchini. Tulitarajia Serikali ingetangaza mafanikio ya mapambano hayo, siyo takwimu tu za tatizo. Kwa mfano kama Lukuvi anakiri kwamba biashara hiyo inawagusa watendaji wa Serikali, basi watajwe na wachukuliwe hatua hadharani.
Hali hiyo inajitokeza wakati kukiwa na ongezeko la Watanzania wanaokamatwa kwa kujihusisha na biashara hiyo.
Kwa mfano katika kipindi cha mwaka 2008 hadi 2012, watuhumiwa 10,799 walitiwa mbaroni kwa kujihusisha na biashara hiyo nchini, huku Watanzania 240 wakikamatwa katika nchi za Brazil, Pakistan na Afrika Kusini na baadhi wamefungwa.
Taarifa ya Serikali inaonyesha pia kuongezeka kwa tatizo hilo hadi ilipofika mwaka 2010 ambapo kilo 914 za dawa za kulevya aina ya heroin, zilikamatwa na kikosi kazi cha kuzuia uharamia nchini.
Tumeshuhudia pia viashiria vya matumizi ya dawa za kulevya nchini hasa kwa wasanii wa muziki na michezo mingine. Ni hivi karibuni tu kulikuwa na kifo cha utata cha msanii Albert Mangwair aliyefia nchini Afrika Kusini huku ikidaiwa kuwa alikuwa na ‘mzigo’ tumboni.
Kifo chake kilifuatiwa na msanii mwingine wa muziki wa kizazi kipya, Langa Kileo ambaye naye aliathirika na dawa hizo.
Msanii mwingine aliyeathirika na dawa za kulevya na sasa anapatiwa matibabu kwa ufadhili wa Rais Jakaya Kikwete ni Rehema Chalamila.
Kama hiyo haitoshi, tumeshuhudia hukumu ya miaka 15 aliyopewa mwanamichezo wa ndondi, Petro Mtagwa na watu wengine watatu waliokamatwa na dawa za kulevya aina ya Heroin nchini Mauritius.
Hao pamoja na wengine wengi wanaonyesha kuwa janga hili ni kubwa mno. Hata hivyo nina wasiwasi na hatua zinazochukuliwa na Serikali yetu.

Ni kweli kwamba kuna kikosi maalumu cha Jeshi la Polisi cha kupambana na dawa za kulevya. Lakini hatuoni hatua kali zikichukuliwa kwa wahusika kama nchi nyingine.
Zipo baadhi ya nchi ambazo mtu akikamatwa, ama anashtakiwa na kupata kifungo mara moja, nchi nyingine watu wanahukumiwa kunyongwa hadi kufa. Hiyo yote ni kuonyesha jinsi wenzetu walivyo makini na mapambano hayo.  Lakini nchi yetu, tunasikia tu watu wanakamatwa, lakini mwenendo wa kesi zao hausikiki tena. 

Ninamaanisha kwamba hatuna hatua kali kwa wahusika hao. Nadhani kuna haja ya sheria za kudhibiti dawa za kulevya zingepitiwa upya ili kuongezwa makali.
Kama takwimu zinaonyesha kuwa uingizaji umekuwa mkubwa na watu wanakamatwa, huwa wanapelekwa wapi? Dawa zilizokamatwa zinapelekwa wapi?
Mambo haya yote yanapaswa kufanyika kwa uwazi ili kutoa onyo kwa wengine wanaoweza kushawishika kujiingiza kwenye biashara hiyo.
Hatua nyingine ambayo Serikali ingetilia mkazo ni kwa wasanii na wanamichezo ambao kwa kiasi kikubwa wanaonekana kuathirika ni kuweka walau kanuni za kuwadhibiti.
Baraza la Sanaa Tanzania (Basata) linapaswa kuwasajili wasanii wote nchini na ikiwezekana kuwapima mara kwa mara kama wanatumia dawa za kulevya, kama vinavyofanya vyama vya michezo kwa wachezaji.
Wasanii wanaokutwa na hatia wachukuliwe hatua kali ikiwa pamoja na kifungo gerezani na kufutiwa usajili wa kufanya kazi za sanaa nchini. Tusingoje hadi vijana hawa waathirike ndiyo waanzishiwe matibabu.
Hatua nyingine ambayo ni ya kutibu ni Serikali kufadhili au kuanzisha vituo vya kuwatibu walioathirika. Hatua hii isiwe kwa watu maarufu tu, bali hata wa hali ya chini ili kuwakwamua katika janga hilo.
Hatua hizi zinapaswa kuchukuliwa mapema huku Serikali pia ikiimarisha ulinzi kwa njia zinazotumika kuingiza dawa hizo.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top