MBUNGE wa Karagwe, Gosbert Blandes
(CCM), amehoji lini serikali itapitisha Kiswahili kitumike kuanzia Shule
za Msingi hadi Vyuo Vikuu. Aidha, alisema mwaka 2004, Umoja wa Afrika
ulipitisha Kiswahili kiwe ni lugha ambayo itatumika katika mikutano na
shughuli mbalimbali.
“Je, serikali imejiandaa vipi kupeleka wakalimani wa kutosha kutoka Tanzania ili waweze kujipatia ajira?” alihoji.
Akijibu maswali hayo, Naibu Waziri wa
Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Amos Makala alisema jitihada
zinafanywa na taasisi hizo za kukuza Kiswahili mojawapo kuandika vitabu
vingi vya kufundishia na kuongeza wataalamu.
“Nasema wazo hilo tumelipokea na sisi
ndani ya serikali tunaendelea kulifanyia kazi na hata wakati
tunawasilisha bajeti yetu zilitoka hoja hizo za kuwa Kiswahili
kifundishwe madarasani,” alisema.
Aidha, Makala alikiri kupitishwa kwa azimio hilo na kuongeza kuwa:
“Kama Tanzania tumeona kuwa hii ni fursa
muhimu na tayari moja ya kazi zinazofanywa na Taasisi za kukuza
Kiswahili, BAKITA, BAKIZA ni kuongeza wataalamu zaidi ili waweze kupata
ajira hiyo.”
Aliongeza kuwa Tanzania kama Tanzania
mjini Addis Ababa kuna kituo cha kufundishia lugha ya Kiswahili. Awali
katika swali la msingi, Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM)
alitaka kufahamu kama nchini Tanzania kuna Sera ya Lugha.
Pia, alihoji kama ipo, je, sera hiyo ya Lugha imeipatia hadhi gani lugha ya Kiswahili.
Aidha, alitaka kujua kuna mkakati gani
mahsusi wa kuifanya Lugha ya Kiswahili kuwa ya kufundishia kwa viwango
vyote vya elimu hapa nchini.
Akijibu swali hilo, Makala alisema
Tanzania hakuna andiko mahususi au linalosimama pekee kama Sera ya
Lugha, bali suala la lugha limezingatiwa kama Sura maalumu muhimu ndani
ya Sera ya Utamaduni ya mwaka 1997.
Alisema katika andiko hilo la sera ya
Utamaduni, Kiswahili kimetambuliwa kuwa siyo tu lugha ya mawasiliano
mapana nchini bali pia ni lugha ya taifa na mojawapo ya lugha rasmi
mbili za Taifa.
Aidha, alisema miongoni mwa mikakati
mahsusi ya kuifanya lugha ya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia ni
jitihada zinazoendelea za wataalamu wa Asasi za ukuzaji wa Kiswahili
nchini ambazo ni kuboresha sarufi ya Kiswahili, kutunga Kamusi za
Kiswahili za masomo na taaluma mbalimbali.
Chanzo: HabariLeo
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
0 comments:
Post a Comment