NIMEKUWA nikisoma mashairi kwa miaka kadhaa ambapo awali
niliamini kuwa kila mtu anaweza kuyatunga kwa sababu tu anao uhuru wa
kufanya hivyo, lakini shairi lenyewe likawa ni lake likamridhisha yeye
na matakwa yake binafsi na si vinginevyo.
Mashairi mengi ya miaka ya nyuma yalivutia, yakagusa maisha ya watu
moja kwa moja. Lakini yalijaa utajiri mkubwa wa lugha, nahau, methali
na vibwagizo vingi. Yalisaidia sana kukuza lugha adhimu ya Kiswahili,
kiasi kwamba yaliitangaza nchi yetu kwa mapana makubwa.
Kutokana na utajiri huo, vitabu vingi vya watunga mashairi na hata
wale walioandika katika magazeti, vilitumiwa kufundishia katika shule
za msingi na sekondari, na baadhi yake vilitumiwa kwa kiwango kikubwa
katika vyuo vya elimu ya juu.
Kwa bahati mbaya, umahiri na ushindani wa watunga mashairi ulianza
kufifia miaka ya tisini, na tangu wakati huo hadi sasa ni watunzi
wachache sana waliobaki, na hata wao hawatungi tena yenye mguso na
hisia kubwa kama walivyokuwa watunzi wa zamani. Mashairi mengi
yanayotungwa sasa hayana mvuto wala utamu kiasi kwamba hayaleti
msisimko kwa anayeyasoma.
Najiuliza je, washairi wa zamani hawakurithisha ujuzi wao kwa kizazi
hiki? Najua kuwa ushairi ni kipaji na si kila mtu anacho, na wale
walionacho leo wanahitaji kusaidiwa kwa kuhamasishwa ili wakipende
kipaji chao, wapate mafunzo ya lugha katika sarufi fasihi na nahau
kwani mashairi ili yapendeze yanatakiwa beti zake ziwe na urari, mizani
na vina lakini pia na mantiki ili ujumbe wake uvutie msomaji.
Nakumbuka magazeti ya zamani ya Uhuru, Mzalendo, Ngurumo na gazeti
kongwe la Kiongozi lililoanzishwa enzi zile za ukoloni, yaani mwaka
1947 na hadi sasa bado liko mitaani, yalikuwa maarufu sana kwa
kuchapisha mashairi. Yalikuwepo pia magazeti kutoka majirani zetu nayo
ni Baraza, Mwafrika, Mwangaza na mengineyo.
Waliosoma magazeti hayo, nikiwemo mimi mwenyewe tulikutana na majina
maarufu katika fani hiyo. Malenga waliotingisha, wakitambia na kuonesha
weledi wao mkubwa katika kutumia lugha ya Kiswahili, ni pamoja na
gwiji wa Kiswahili duniani, Shaaban Robert. Huyu akichuana vikali na
Matias Mnyampala, Saadani Abdul Kandoro na mlemavu wa macho, Amir Said
Andanenga aliyejipachika jina la ushairi la Sauti ya Kiza.
Baadae wakazuka kwa kishindo watu kama Said M. Nyoka ‘Udongo si
hoja”, Ustaadh Bhalo Ahmad Nassir wa ‘Malenga wa Mvita’ na wengineo.
Kisha wakaja akina Mganga Romani Mihambo akijiita kwa ushairi kama
‘Bado Bichi’, Adam Amri Nanjanse ‘Mvumo’ na Omari S. Mtulia ‘Mbaya
Mimi’, ambaye amefariki akiwa katika harakati za kutoa kitabu cha
mashairi yake alichokiita ‘Chozi la Ulimwengu’ na wengineo wengi.
Hata hivyo, hawa hawakuwa waanzilishi wa kutunga mashairi, bali watu
waliojaliwa karama na kuyatosa maisha yao katika fani hii. Tunaweza
kusema kuwa utunzi wa malenga hawa unatokana na historia ya kule
yalikoanzia.
Utafiti unabainisha kuwa utunzi wa mashairi unaoeleweka vema katika
vitabu vingi vya historia unaonesha kuanza tangu miaka ya 1700 na
pengine kabla ya hapo. Yawezekana hayakujulikana zaidi kutokana na
ufinyu wa elimu ya kusoma na kuandika ambayo ilikuwa bado ni kwa
wachache katika pwani ya Afrika ya Mashariki ambako inaaminika kuwa
ndio chimbuko la Kiswahili.
Kumbe tunaposoma katika vitabu vya ushairi katika Diwani na majina ya
malenga mashuhuri yaliyomo katika kitabu cha Malenga wa Mvita, ni
pamoja na Diwani ya Myaka, Sheikh Sudi Al Mamasa, Ayubu, Mwalimu
Sikujua, Mtwana na Sumba na wengineo wengi. Mashairi yao ni mazito.
Lugha waliyoitumia ni Kiswahili, lakini lafudhi ya maneno ni ya
Kimvita ambayo ndiyo matamshi yaliyokuwepo sehemu ya Pwani ya Afrika ya
Mashariki wakati huo.
Washairi wa Tanzania ya leo mashairi yao kama nilivyodokeza awali,
hayana lugha ya kuzama. Hawana mashairi ya majigambo, malumbano au
kujibizana kwa jambo lolote. Wale wa kale wanasema kuwa mashairi yao
mengi yalitoka katika nyimbo na ngoma za asili kama vugo, gungu, diriji,
lelemama nk.
Malenga hawa sio tu walizama katika utunzi wa mashari, bali
walijikita pia katika kutunga tenzi mbalimbali ambazo twaweza kusema
zilikuwa katika mfumo wa nusu shairi. Zilikuwa na maneno machache,
lakini yaliyokuwa katika mpangilio mwanana kama ule wa shairi. Kulikuwa
na tungo za tenzi fumo liwongo na baadaye tenzi za nafsi.
Hizi nazo zimetoweka kabisa, afadhali kidogo mashairi na hivyo kuwa
sehemu ya chimbuko la kaburi linalozika lugha ya Kiswahili.
Badala yake baadhi ya walimu katika shule zetu wanajitahidi
kuwafundisha wanafunzi kutunga vitendawili, ngonjera na hadithi
mbalimbali, lakini si mashairi na ndiyo maana hatuna tena malenga wetu
wa mashairi na hata wale wa kughani hawapo tena.
Ningeshauri Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA) na Usanifu wa
Kiswahili na Ushairi Tanzania (UKUTA) walitupie macho jambo hili, na
pengine turejee kwa mhenga wa kale Hyder Mohamad Matano Kindy
aliyeanzisha tuzo ya D.P. yaani Diploma in Poesy.
0 comments:
Post a Comment