Rais Jakaya Mrisho Kikwete
 
 SERIKALI imesema inakabiliwa na upungufu wa walimu wa somo la Sayansi na Hisabati 26,000, licha ya kuajiri walimu wapya 16,000 kwa mwaka huu. 
 
Hayo yalisemwa jana na Rais Jakaya Kikwete, wakati akizungumza na wamiliki na mameneja wa shule na vyuo visivyo vya Serikali jijini Mbeya.
Rais, alikuwa akijibu changamoto mbalimbali zinazoikabili sekta ya elimu, hususan adha wanayoipata wamiliki wa shule binafsi katika kuwapata walimu wa somo la sayansi na hisabati na kwa gharama kubwa.

“Wamiliki hao, wamekuwa wakitumia dola 1,500 za Marekani kwa Serikali kwa ajili ya kulipia kibali kwa mwalimu mmoja anayeingia nchini,” alisema.

Walisema, kiwango cha tozo hicho ni kikubwa huku mishahara, posho na malazi zikiwa ni juu ya mwajiri ambaye amemleta nchini.

Akitolea ufafanuzi suala hilo, Rais alisema uhaba wa walimu wa somo la Sayansi na Hisabati ni la kitaifa, kwani mpaka sasa Serikali inakabiliwa na upungufu wa walimu 26,000 wa masomo hayo muhimu.

Alisema uzalishaji wa Serikali kwa walimu wa masomo hayo kwa mwaka ni 2,200, huku vyuo vinavyotoa wataalamu hao ni vichache na kwamba vyuo hivyo vinatoa walimu ngazi ya cheti na stashahada tu.

Alisema kutokana na tatizo kuendelea kuwa kubwa, ni wajibu wa Serikali kwa kushirikiana na sekta binafsi ya elimu, kulitafutia ufumbuzi tatizo hilo.

Alisema Serikali, inatarajia kunufaika na muungano wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, kutoa fursa kwa walimu kutoka nchi wanachama kufundisha watoto.

“Fursa ya kupata walimu kutoka nchi jirani, itasaidia, kwani zipo nchi ambazo zinachukua walimu wetu kwa ajili ya kufundisha watoto wao na hii ndio faida ya kujiunga na jumuiya hii,” alisema.

Hata hivyo, wamiliki na mameneja, wakuu wa shule na vyuo visivyo vya kiserikali, wamesema wataendelea kutoa kipaumbele kwa kusomesha watoto yatima na wasiojiweza.

“Mpaka sasa shule zetu, zimekuwa zikifundisha watoto yatima na wasiojiweza 1,600 kila mwaka na kwa mwaka huu tunarajia kuchukua watoto 1,048,” alisema mwenyekiti wa jumuiya hiyo, Mahamudu Mlingo.

Mtanzania 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top