Msemaji Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya
Katiba na Sheria, Tundu Lissu.
MSEMAJI Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni kwa Wizara ya
Katiba na Sheria, Tundu Lissu amedai kuwa matumizi ya fedha zilizoombwa
kwa ajili ya Tume ya Mabadiliko ya Katiba ni kufuru.
Lissu ambaye pia ni Mbunge wa Singida Mashariki kwa tiketi ya CHADEMA,
alitoa kauli hiyo wakati akitoa maoni ya kambi ya upinzani kwa bajeti
ya Wizara ya Katiba na Sheria kwa mwaka ujao wa fedha 2013/2014.
Alisema katika mwaka wa fedha 2013/14, Bunge linaombwa kuidhinisha sh
bilioni 33.944, sawa na kiasi kile kile kilichoidhinishwa mwaka wa fedha
uliopita.
Lissu alisema kiasi hicho ni pamoja na sh bilioni 12.193 kwa ajili ya
kulipia posho za vikao kwa wajumbe wa tume 34 na sekretarieti 160, sh
bilioni 1.728 kwa ajili ya posho ya kujikimu kwa wajumbe na sekretarieti
wanaposafiri ndani ya nchi kikazi na sh bilioni 1.650 kwa ajili ya
kulipa gharama za nyumba za wajumbe na sekretarieti wanaotoka nje ya Dar
es Salaam.
Akichanganua matumizi ya tume hiyo, inayoongozwa na Jaji Joseph
Warioba, Lissu alisema kuna sh milioni 18 zinazoombwa kwa ajili ya
kugharamia chakula kwa wajumbe wa tume na sekretarieti watakaopata
maambukizi ya ukimwi.
“Kambi rasmi ya upinzani bungeni inaitaka Serikali ya CCM itoe kauli
rasmi mbele ya Bunge lako tukufu kama kuna uhalali wowote wa kutumia
fedha za wananchi ili kununua ‘chakula maalumu’ kwa ajili ya wajumbe na
sekretarieti ya tume watakaopata ukimwi kwa sababu ya kuendekeza ngono
zembe na starehe zao binafsi,” alisema.
Lissu alisema wajumbe hao ambao wengi ni wazee, wanatakiwa wafanye
kazi ya tume vinginevyo Bunge lielezwe kwa ufasaha ni kwa namna gani
mchakato huu wa Katiba mpya unatazamiwa kusababisha maambukizi ya ukimwi
kwa wajumbe hao.
Kwa mujibu wa Lissu, pia kuna sh milioni 60 kwa ajili ya usafiri wa
ndani, sh milioni 50 kwa ajili ya gharama za malazi kwa wajumbe wa tume
na sekretarieti wanaposafiri kikazi, sh milioni 423 kwa ajili ya chai na
vitafunwa na sh milioni 50 kwa ajili ya wahudumu wanaosaidia kazi za
tume wakiwa mikoani wakati wa kushiriki kwenye mabaraza ya katiba na
shughuli za upigaji kura ya maoni.
Lissu alisema vile vile, Bunge limeombwa kuidhinisha sh milioni 60 ya
kulipia maji kwa matumizi ya ofisi za tume, sh milioni 30 kwa ajili ya
kulipia gharama za usafiri wa basi na teksi kwa wajumbe na sekretarieti
watakaposafiri ndani ya nchi kikazi na sh milioni 103 kwa ajili ya
kulipia gharama za simu za mkononi.
Akiendelea kuanika matumizi ya tume hiyo, Lissu alisema Bunge
linaombwa kuidhinisha posho na ulaji zaidi ya huu kwa ajili ya wajumbe
na sekretarieti ya tume.
Alisema ulaji huu mwingine unajumuisha sh milioni 604 kwa ajili ya
posho kwa wajumbe wa tume na sekretarieti wakati wa Bunge Maalumu la
Katiba.
Alisema maelezo ya tume yamejaribu kuhalalisha matumizi ya fedha hizi
za ziada kwa kuzibatiza jina la ‘posho ya mazingira magumu’, wakati
vikao vya Bunge Maalumu la Katiba vitafanyika jijini Dar es Salaam au
Dodoma.
Lissu aliongeza kuwa zipo sh milioni 266 zinazoombwa kwa ajili ya
chakula na viburudisho wakati wa vikao vya Bunge Maalumu la Katiba, sh
milioni 12 nyingine kwa ajili ya huduma za chakula na viburudisho kwa
shughuli zinazohusiana na tume na sh milioni 185 kwa ajili ya kulipia
usafiri wa basi na teksi.
Aidha, alisema kuna sh milioni 30 za utengenezaji wa fulana na kofia
kwa wajumbe wa tume na sekretarieti wakati wa kushiriki kwenye
uhamasishaji kuelekea upigaji wa kura ya maoni, sh milioni 40 nyingine
kwa ajili ya utengenezaji wa sare wakati wa maadhimisho mbalimbali ya
kitaifa na sh milioni 12 kwa ajili ya posho za kujikimu kwa watumishi wa
tume watakaohudhuria kwenye maadhimisho mbalimbali ya kitaifa.
“Kwa ujumla, Mheshimiwa Spika, Bunge lako tukufu linaombwa kuidhinisha
jumla ya sh bilioni 19.039 kwa ajili ya posho za aina mbalimbali na
malipo mengine yanayowahusu wajumbe na sekretarieti ya tume kwa mwaka wa
fedha 2013/14. Hii ni zaidi ya asilimia 56 ya bajeti yote inayoombwa
kwa ajili ya tume,” alisema.
Kwa mahesabu hayo, Lissu alisema wajumbe wa tume, katibu na naibu
katibu pamoja na wakuu wa vitengo saba vya tume na madereva wao, kila
mmoja atalipwa wastani wa sh milioni 16.756 kwa mwezi huo mmoja, au sh
558,547 kama posho ya kujikimu kwa kila siku moja.
“Mheshimiwa Spika, katika nchi ambayo wauguzi katika hospitali za umma
wanalipwa mshahara wa kuanzia takriban sh 360,000 kwa mwezi na walimu
wa shule za msingi wanaanzia sh 250,000 na wale wa sekondari sh 325,000
kwa mwezi, malipo haya kwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba yana uvundo na
harufu mbaya ya rushwa kwa wajumbe wa tume,” alisema Lissu.
Mabaraza ya Katiba
Lissu alisema Februari mwaka huu, tume ilichapisha mwongozo kuhusu
muundo, utaratibu wa kuwapata wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya
(Mamlaka za Serikali za Mitaa) na uendeshaji wake.
Alisema mwongozo huo ulisainiwa na Mwenyekiti wa Tume Jaji Warioba na ulianza kutumika Machi Mosi, mwaka huu.
Alisema ingawa tume imedai kwamba mwongozo huo ulitolewa kwa
kuzingatia matakwa ya Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, kambi hiyo
inaamini kwamba ulitolewa kinyume na matakwa ya sheria hiyo na kwa lengo
la kuinufaisha CCM na washirika wake.
Kwa maana hiyo, alisema mikutano ya uchaguzi wa mabaraza ya katiba ya
wilaya kwa upande wa Tanzania Bara imeendeshwa na makada wa CCM wakati
kwa upande wa Zanzibar imeendeshwa na viongozi waliochaguliwa na
wananchi walioshiriki katika mikutano hiyo bila kujali itikadi au
uanachama wao katika vyama vya siasa.
Alisema ndiyo maana karibu nchi nzima wananchi wengi wasiokuwa
wanachama wa CCM ambao walipata kura nyingi katika kura za mikutano ya
uchaguzi ya vijiji na mitaa walienguliwa kwenye michujo iliyofanyika
katika kamati za maendeleo za kata zilizowekwa kwa mujibu wa mwongozo wa
tume.
Lissu alisema hata mahali ambapo wananchi wasiokuwa wanaCCM
walifanikiwa kupenyeza katika chekeche la kamati za maendeleo za kata
(WDC) wamefanyiwa mizengwe na wanaCCM ili waondolewe katika orodha ya
wajumbe wa mabaraza ya katiba ya wilaya.
Alisema mfano mzuri ni Beatus Kipeya aliyechaguliwa mjumbe wa Baraza
la Katiba la Wilaya ya Arusha Mjini kwa kupitia Kata ya Sombetini.
Alisema mara baada ya Kipeya kuchaguliwa kwenye kikao cha Kamati ya
Maendeleo ya Kata ya Sombetini cha tarehe 8 Aprili, 2013, siku hiyo hiyo
Katibu wa CCM Wilaya ya Arusha, Allan G. Kingazi alimwandikia Mkuu wa
Wilaya ya Arusha kumlalamikia juu ya kuchaguliwa kwake.
Alisema ukiacha Ofisa Uhamiaji wa Mkoa wa Arusha, watu wengine wote
walionakiliwa barua ya malalamiko ya Katibu wa CCM Kingazi ni makada wa
CCM.
“Wote hawa hawahusiki kisheria kwa namna yoyote ile katika mchakato wa
uundaji wa mabaraza ya katiba ya wilaya. Chombo pekee ambacho
kinahusika kisheria na mchakato wa kuunda mabaraza hayo na ambacho
kilitoa mwongozo wa namna ya kuyaunda, yaani tume, haikuandikiwa wala
kunakiliwa barua ya malalamiko ya Katibu wa CCM Kingazi,” alisema.
Lissu aliongeza kuwa endapo serikali itashindwa kutekeleza ahadi ya
Waziri Mkuu Mizengo Pinda wakati akihitimisha mjadala wa bajeti ya ofisi
yake, na endapo muswada utakaoletwa hautakidhi matakwa ya kuboresha
mchakato wa upatikanaji wa katiba mpya, basi CHADEMA itahamasisha
Watanzania kuikataa rasimu ya katiba mpya kwenye kura ya maoni.
“CHADEMA itawaalika wanachama, wafuasi na mashabiki wake Tanzania
nzima, pamoja na taasisi za kiraia na za kidini, vyama vya siasa na
Watanzania wote wenye nia njema na taifa hili kuhamasisha Watanzania
kuikataa rasimu ya katiba mpya kwenye kura ya maoni,” alisema.
0 comments:
Post a Comment