Kuna baadhi ya marafiki huingia kwenye ndoa wakiwa na matumaini ya kujifunza – hata kama hana mapenzi na mwenzi wake. Hilo ni kosa kubwa. 

Hakuna kujifunza ndani ya ndoa. Wiki mbili zilizopita nilifafanua mambo mengi ya msingi lakini kubwa zaidi nilikazia kuwa, ndoa si tendo la majaribio. Linahitaji kujipanga na kuwa na uhakika na mwenzi unayekwenda kuungana naye.
Tuendelee kujifunza marafiki zangu.

SUALA LA UMRI
Je, wewe una umri gani? Ni msichana mwenye zaidi ya miaka 20 au mvulana unayezidi miaka 23? Kama ndivyo, tunaweza kuendelea na mada hii.

Najua kuna watu wananishangaa baada ya kuandika umri huo hapo juu. 

Ni kweli umri unaotambulika kiserikali wa kijana kuingia kwenye ndoa ni kuanzia miaka 18 lakini msichana anaweza kuolewa hata akiwa na miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi wake.

Je, inamaana kwamba kijana mwenye miaka 18 hapaswi kuoa au kuolewa? La hasha. Sina maana hiyo.  Ndugu zangu, wengi huingia kwenye ndoa na baadaye hugeuka majuto. 

Uwezo wa ubongo wa binadamu kufikiri umegawanyika katika makundi. Kuna kipindi binadamu huwa na mawazo ya zimamoto.

Anawaza kwa kuongozwa na hisia, lakini ubongo wake ukikua anabadilika. 

Ukweli ni kwamba, angalau msichana mwenye zaidi ya miaka 20 (hasa kuanzia miaka 22 hivi) angalau anaweza kuwa na uamuzi/uchaguzi sahihi wa nani awe mumewe.

Wavulana ndiyo kabisaaa! Hawa wanahitaji muda wa kutosha kufanya uamuzi wa nani awe mke wake wa ndoa.

Wengi hujidanganya na hisia za machoni, lakini baadaye wanakuja kugundua walifanya uchaguzi kimakosa.

Inaamika kuwa angalau kijana aliyefikisha miaka 25 na kuendelea ndiye mwenye uwezo (angalau) wa kufanya uchaguzi wa mke wa maisha yake. Kwa ambao hawana umri huu, wanaweza wasikubaliane na ukweli huu.

NDIVYO ILIVYO
Utafiti mdogo unaonyesha kwamba, vijana wengi wanaokutana shuleni (hasa sekondari) na kuanzisha uhusiano huwa hawafiki mbali. Ama mapenzi huishia njiani au mara baada ya kumaliza shule na kila mmoja kurudi nyumbani kwao.

Huu ni uhusiano wa kitoto wa kudanganyana zaidi ambao mwisho wake huwa si ndoa. 

Wapo ambao wameanza mapenzi tangu wakiwa shule na baadaye wakaoana lakini si zaidi ya asilimia tano!

Hawa wana tofauti kidogo na wale wanaokutana vyuoni – ni walewale, lakini wana nafuu kidogo, maana umri unakuwa umesogea kidogo (kuanzia miaka 22) hivyo kuweza kufanya uamuzi sahihi, lakini wengine wanaangushwa na wenzao.

Wanaanzisha uhusiano lakini kumbe mmoja wao akirudi kwao likizo anakuwa na mwingine. Huo ni udanganyifu.

UMAKINI UNAHITAJIKA
Wewe kijana uliyeko chuoni (hasa msichana) uwe makini na namna ya kuanzisha uhusiano. Wengi ni walaghai, wanatafuta hifadhi ya muda tu. Ni vyema kutumia hekima yako vizuri. Usikubali kuwa pumziko la mtu ambaye atakwenda kuoa mwanamke mwingine.

Kinachowaponza ni ngono, kuna sababu gani ya kuanza kufanya ngono mapema kama ni kweli ana mapenzi ya kweli? Akishakujua kuna nini tena? Anajiburudisha halafu mwisho wa siku anakutosa.
Utaolewa na nani? Hili ni jambo muhimu kutafakari ukiwa ndani ya umri nilioueleza hapo juu.

WAZAZI SOMENI HAPA
Wazazi ni viunganishi muhimu katika ndoa za vijana wao lakini wakati mwingine huwa vikwazo au husababisha maisha mabovu kwa vijana wao kutokana na kuwachagulia wapenzi. Hili ni tatizo kubwa sana.
Kuna binti mmoja alilazimishwa na wazazi wake kuolewa na mwanaume ambaye yeye hakumpenda.

Akaomba sana wazazi wake wasikilize hisia zake, hawakumuelewa. Akafunga ndoa kwa shingo upande, sasa hivi ni majuto!

Mwanaume ni mlevi kupindukia, kosa dogo tu anapiga! Mwanamke amegeuka ngoma. Akikaa muda mrefu sana bila kupewa kipigo ni wiki tatu.

Hayo ni mateso yasiyo na ulazima. Vipi kama wazazi wakiwaacha vijana wakafanya uamuzi wao peke yao? Si vibaya wazazi kushauri lakini haifai kulazimisha. Wazazi tumieni hekima katika jambo hili.
GPL 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top