Kampuni nyingi za simu na za madini nchini zinadaiwa kuwanyonya wafanyakazi wao na kusababisha serikali kuamua kuingilia kati kwa kusimamia moja kwa moja usajili mpya wa mawakala wa ajira.

Kampuni hizo zinatuhumiwa kutumia mawakala kupata wafanyakazi kinyume na utaratibu wa kisheria, kuingia mikataba na mawakala hao, kuwalipa mishahara kisha mawakala kulipa wafanyakazi, ikiwa ni ujanja wa kuepuka kuwajibika moja kwa moja kwa wafanyakazi hao.
Kwa mujibu wa sheria, mawakala hao ambao awali walikuwa wakisajiliwa na Msajili wa Kampuni (Brela) na Wakala wa Ajira nchini (Taesa), walitakiwa kuwa kiunganishi kati ya waajiri na watafuta kazi kwa kulipwa kamisheni, lakini wamekuwa wakikodisha wafanyakazi kwa kampuni hizo kinyume cha sheria.
Msemaji wa Wizara ya Kazi na Ajira, Ridhiwan Wema alisema jana kuwa Wizara iliamua kuingilia kati suala hilo na kusimamia moja kwa moja usajili mpya wa mawakala hao kwa kuwa ilibaini ukiukwaji mkubwa wa sheria, ikiwamo kuwanyima haki zao za matibabu, pensheni na kuikosesha Serikali mapato yanayotokana na mishahara yao.
Kampuni hizo ndizo zinazotengeneza faida kubwa na zinazojiendesha kwa gharama za juu, huku zikipata ahueni ya kodi kutoka serikalini.
Mawakala 56 binafsi wa ajira wameshajiorodhesha na wizara imeongeza miezi miwili zaidi kwa ajili ya usajili huo.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top