Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

Tume ya Mabadiliko ya Katiba imetoa rasimu ya mwongozo kuhusu uundwaji wa Mabaraza ya Katiba yakiwemo yatakayoundwa na asasi, taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana, huku ikitoa siku nane kwa wadau kutoa maoni yao kuhusu rasimu hiyo.
 
Mwongozo huo unaainisha muundo, utaratibu na uendeshaji wa mabaraza yote ya Katiba, huku mwisho wa kuwasilisha maoni kwa tume hiyo kuhusu Rasimu ya Mwongozo huo ikiwa ni Mei 19, mwaka huu.
Watakaounda mabaraza hayo ni pamoja na Jumuiya ya Kidini, Chama cha Siasa, Asasi ya Kiraia, Taasisi ya Elimu ya Juu, Chama cha Wafanyakazi, Chama cha Wakulima, Chama cha Wafugaji, Chama cha Wanahabari na Baraza la Watoto. Nyingine ni Taasisi ya Wafanyabiashara, Baraza la Wanawake, Taasisi ya Wanataaluma, Baraza la Vijana, Baraza la Wazee na Kundi au makundi ya watu wenye mahitaji maalumu katika jamii.
Kutolewa kwa rasimu hiyo kumekuja mwezi mmoja tangu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kutishia kujitoa kwenye mchakato wa Katiba Mpya, kikitaka kurekebishwa kwa baadhi ya mambo katika mchakato huo.
Aprili 11, mwaka huu chama hicho kilitangaza kwamba ifikapo Aprili 30, mwaka huu kitajitoa endapo mambo muhimu mawili hayatapatiwa ufumbuzi.
Mambo hayo ni kufutwa kwa uchaguzi wa wajumbe wa Mabaraza ya Wilaya ya Katiba uliofanywa na Kamati za Maendeleo za Kata (WDC), badala yake wachaguliwe moja kwa moja na wananchi wa kata husika bila kuchujwa na kamati hizo.
Hata hivyo, baadaye kilieleza kuwa kinafanya mikutano ya ndani kabla ya kutoa jibu kamili kuhusu suala hilo.
“Tume inaweza kuruhusu asasi, Taasisi na makundi ya watu wenye malengo yanayofanana kuandaa mikutano kwa ajili ya kutoa fursa kwa wanachama wake kutoa maoni yao juu ya rasimu ya Katiba na kisha kuwasilisha maoni hayo kwa Tume.
Hilo tumeruhusu kwa mujibu wa sheria,” alisema Mwenyekiti wa Tume ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.
Alisema kuwa tume hiyo imeamua kuwa mabaraza ya Katiba yatakuwa katika makundi mawili, la kwanza likiwa ni mabaraza ambayo tume itayasimamia na kukusanya maoni (Mabaraza ya Katiba ya Wilaya – Ngazi ya Mamlaka ya Serikali za Mitaa).
Mabaraza mengine ni yale ambayo hayatasimamiwa na tume hiyo, bali yatajisimamia yenyewe na kukusanya maoni yatakayowasilishwa kwenye tume kwa mujibu wa maelekezo.
 Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top