Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe.

CHUO cha Taifa cha Usafirishaji (NIT) kinakusudia kuanza kutumia viwanja vya ndege vya Dodoma na Tanga kwa ajili ya mafunzo ya marubani wa ndege.

Kauli hiyo ilitolewa bungeni jana na Waziri wa Uchukuzi, Dk. Harrison Mwakyembe, wakati akiwasilisha makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi kwa mwaka wa fedha 2013/2014.

Waziri Mwakyembe alisema kuwa maandalizi ya mafunzo hayo yanaendelea ambapo kwa sasa mitaala imekamilika na inasubiri ithibati kutoka kwenye mamlaka husika.

Alisema kuwa katika mwaka 2013/2014, chuo kinatarajia kuanzisha programu ya stashahada ya uzamili katika uhandisi wa usafirishaji; lengo ni kuwa na wataalamu wa kutosha katika sekta ndogo za bandari, viwanja vya ndege, reli na usafirishaji kwa njia ya mabomba.

“Kazi nyingine inayotarajiwa kutekelezwa ni kukarabati majengo ya chuo ili kuboresha mazingira ya kufundishia na kujifunzia,” alisema.

Kuhusu kuboresha usafiri wa reli nchini, alisema kuwa katika mwaka 2013/2014, Kampuni ya Reli Tanzania (TRL) imetengewa sh bilioni 113.12 kwa ajili ya kukamilisha ununuzi wa vichwa vya treni 13, mabehewa 22 ya abiria, mabehewa 274 ya mizigo, mabehewa 34 ya breki, mashine ya nyakua, matoroli 30 na vifaa vingene na kulipa madeni ya kampuni.

Waziri Mwakyembe aligusia usafiri wa magari madogo aina ya NOAH akisema kuwa wizara imepokea malalamiko mengi kutoka mikoa kadhaa juu ya hatua ya Mamlaka ya Usafiri wa Majini na Nchi Kavu (Sumatra) kuyazuia kutoa huduma ya usafirishaji wa abiria.

Alisema kuwa serikali imeiagiza Sumatra kuandaa utaratibu wa kutoa leseni kwa magari hayo kwa sharti la kurekebisha madirisha yake ya nyuma, kubeba idadi ya abiria itakayotajwa na nauli elekezi ya Sumatra baada ya kuwashirikisha wadau.

Nayo Kamati ya Bunge ya Miundombinu kupitia kwa mwenyekiti wake Peter iliishauri serikali kwa kutoa kipaumbele katika ujenzi wa gati namba 13 na 14 katika Bandari ya Dar es Salaam.
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top