Jopo la mawakili wanaomtetea Mkurugenzi wa Ulinzi na Usalama
wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Wilfred Lwakatare leo
linaanza harakati za kumtoa mahabusu kwa dhamana.
Hatua hiyo inatokana na uamuzi wa Mahakama Kuu
Kanda ya Dar es Salaam, kumfutia Lwakatare mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa
yakimkabili yeye na mwenzake Joseph Ludovick Rwezaura, ambayo hayana
dhamana na kubaki na shtaka moja la kula njama ambalo linadhaminika.
Kesi hiyo namba 6 ya mwaka 2013, inayosikilizwa na
Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, inatajwa leo, lakini
mawakili wa Lwakatare wamejipanga kumwombea dhamana Lwakatare.
Mmoja wa mawakili wa Lwakatare, Peter Kibatala
aliliambia Mwananchi jana kuwa kwa kuwa kosa lililobaki linadhaminika,
basi jambo moja watakalolifanya leo ni kuwasilisha maombi ya dhamana.
“Kwa kuwa shtaka lililobaki linadhaminika na kwa
kuwa tayari file (jalada) la kesi limesharejeshwa (Kisutu) kutoka
Mahakama Kuu, basi tutakachokifanya kesho (leo) ni kuomba dhamana tu,”
alisema Wakili Kibatala na kuongeza:
“Kama hapatakuwa na pingamizi lolote tunaamini
kuwa leo anaweza kutoka kwani tumejiandaa kutekeleza masharti yoyote
yatakayotolewa na mahakama.”
Ikiwa hapatakuwa na pingamizi lolote la kisheria
kutoka upande wa mashtaka ambalo litaibua mabishano makali, huenda
mahakama ikatoa uamuzi wa maombi ya dhamana leo, na kama watuhumiwa
wataweza kutimiza masharti yatakayowekwa na mahakama, basi Lwakatare
anaweza kurejea uraiani leo.
Hata hivyo, kama kutakuwa na pingamizi la kisheria
na mabishano mahakama, inaweza kuahirisha na kupanga siku nyingine ya
kutoa uamuzi wa maombi hayo ili kupata muda wa kutafakari kwa kina hoja
za kisheria za pande zote zitakazokuwa zimetolewa.
Lwakatare na Rwezaura walikuwa wakikabiliwa na
mashtaka manne, matatu kati ya hayo yakiwa ya ugaidi na moja la kawaida
la jinai. Mashtaka hayo yalikuwa ni kula njama, kupanga kumteka Dennis
Msacky na kisha kumdhuru kwa kutumia sumu na kufanya mkutano wa vitendo
vya kigaidi.
Mashtaka hayo matatu yalikuwa yakiwakabili
washtakiwa wote wawili wakati shtaka la nne la kuhamasisha vitendo vya
ugaidi lilikuwa likimkabili Lwakatare peke yake, akidaiwa kuruhusu
nyumba yake ya Kimara King’ongo kutumika kupanga mipango ya ugaidi.
Hata hivyo, Mei 8, mwaka huu, Mahakama Kuu
iliwafutia mashtaka matatu ya ugaidi na kubakiwa na shtaka moja tu la
kula njama za kutenda kosa la kumdhuru Msacky kwa kutumia sumu.
Uamuzi huo wa Mahakama Kuu ulitokana na maombi ya
jopo la mawakili wa Lwakatare waliyoyawasilisha mahakamani hapo
wakiiomba ipitie uamuzi wa Mkurugenzi wa Mashtaka, kuwafutia kesi ya
awali na kisha kuwakamata na kuwafungulia tena kesi ya mashtaka
hayohayo.
Mwananchi
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment