Marehemu Venance Mushi enzi za uhai wake.
JUMANNE, Juni 10, mwaka huu majambazi yapatayo sita, yalivamia Kituo
Kidogo cha Polisi Kimanzichana na kupora silaha na baadaye kumuua askari
polisi mmoja, mgambo mmoja na kumjeruhi mwingine na kutoweka.
Kwa mujibu wa mashuhuda, majambazi hayo yalifika katika kituo hicho
majira ya saa saba usiku, yakiwa yanakokota bodaboda mbili huku wengine
wakijifanya wanachechemea kuonyesha kuwa walipata ajali.
Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Mariam Ally, aliyelazwa katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili, wodi namba mbili ndani ya jengo la
Mwaisela ambaye ni mgambo, anasimulia jinsi mkasa huo ulivyotokea, baada
ya Uwazi kumtembelea.
Mke wa marehemu akilia kwa uchungu na simanzi kubwa.
“Tukiwa kituoni hapo, ghafla tuliona watu wakikokota pikipiki mbili
aina ya Boxer huku baadhi yao wakitembea kwa kuchechemea kama vile watu
waliopata ajali.
“Hakuna mtu aliyefikiri kama kungekuwa na tukio la uvamizi, walipaki na kusogea kwa ajili ya kupata huduma,” alisema Mariam.
Alisema jambo la kwanza walilofanya ni kumvamia askari aliyekuwa na
bunduki na kumpora kisha wakaelekea chumba cha kuhifadhia silaha na
kuchukua SMG nyingine kabla ya kuanza kufyatua risasi hewani.
“Nilipoona hali imeshakuwa mbaya, nililala chini na kuanza kupiga
simu kuomba msaada, kumbe simu hiyo ilitoa mwanga hivyo majambazi
yakanigeukia na kuanza kunishambulia kwa mapanga na mateke hadi
nikazimia kutokana na kuvuja damu nyingi.
Mke wa marehemu akiaga mwili.
“Mimi ninachokijua pale kituoni tulikuwa na silaha mbili (bunduki mbili aina ya SMG) ambazo zilichukuliwa na majambazi hao.”
Mtoto mkubwa wa askari mgambo, Venance Urio aliyefia hospitalini
aliyejitambulisha kwa jina la Tumaini alisema siku ya tukio alikuwa
Gongo la Mboto.
“Sina la kufanya maana tegemeo langu limeondoka, ameniacha katika
wakati mgumu sana,” alisema wakati wa zoezi la kuaga mwili wa mzazi
wake.
Ndugu jamaa na marafiki wakiuaga mwili wa marehemu.
Mke wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Veneranda Urio
alisema alifuatwa usiku wa manane na mwenyekiti wa kijiji akiwa na
baadhi ya majirani na kumtaka atoke nje, lakini alikataa kwa kuhofia
usalama wake.
“Lakini baada ya kugongewa kwa muda mrefu nikaamua kufungua ndipo
nilipoambiwa mwenzangu amevamiwa na majambazi, na kwamba wamempeleka
hospitali, nikafanya hima kwenda Muhimbili nilikoambiwa amepelekwa na
majeruhi mwenzake, nilimkuta kawekewa pamba kubwa tumboni, alikokuwa
amepigwa risasi.
“Kauli ya mwisho ya mume wangu aliitoa baada ya kumshika mkono alisema usiniache tuondoke sote nyumbani.
Kamanda
Matei (kushoto) akimjulia hali Mariam Ally katika Hospitali ya Taifa
Muhimbili mwishoni mwa wiki baada ya kujeruhiwa na majambazi.
“Hata hivyo, muda wa kuona wagonjwa uliisha nikawa nimetoka kurudi nyumbani huko nyuma akaaga dunia.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani, SACP Ulrich Onesphory Matei alisema
tukio hilo ni pigo kubwa na linafanyiwa kazi kwa kiwango cha juu kwani
hadi hivi sasa watu 17 wanashikiliwa na uchunguzi unaendelea.
Mariam Ally akionyesha jeraha alilolipata baada ya tukio hilo.
“SMG mbili zilizokuwa kwa ajili ya ulinzi zimechukuliwa, makachero wa kutosha wamemwagwa, ni imani yangu wahusika watakamatwa.
“Ninawaomba wananchi kutoa ushirikiano ili tuweze kukomesha vitendo hivi viovu,” alisema kamanda huyo.
0 comments:
Post a Comment