Rais Jakaya Kikwete ametoa ahadi mbili za kuwafurahisha
wafanyakazi. Kwanza ametangaza nia ya kuongeza mishahara yao na pili,
kupunguza kodi inayokatwa kwenye mishahara hiyo mambo ambayo ameahidi
kutekelezwa katika Bajeti ya mwaka 2014/2015 inayotarajiwa kuwasilishwa
bungeni hivi karibuni.
Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya
Wafanyakazi (Mei Mosi), yaliyofanyika kitaifa Dar es Salaam jana, Rais
Kikwete alisema anatambua kuwa wafanyakazi wana hamu ya kujua Serikali
itasema nini kuhusu masilahi yao.
Alisema malalamiko ya wafanyakazi wengi ni kutaka
kuona kima cha chini cha mshahara kinaongezwa huku kodi kwenye mishahara
(Paye), ikipungua.
“Mimi na wenzangu serikalini hatuna upungufu wa
dhamira ya kufanya hivyo, tumethibitisha miaka iliyopita na tutaendelea
kuwa hivyo,” alisema.
Huku akishangiliwa na wafanyakazi waliofurika
katika Uwanja wa Uhuru, Rais Kikwete alisema: “Najua kuwa nyongeza
tuliyotoa mwaka jana si kubwa kama wafanyakazi walivyotaka iwe... hata
mimi nisingependa iwe hivyo.”
“Kwa nyongeza iliyofanywa mwaka jana, hivi sasa
Serikali inatumia asilimia 44.9 ya Bajeti kulipa mishahara ambayo ni
asilimia 10 ya Pato la Taifa.”
Akifafanua namna Serikali ilivyofikia uamuzi wa
kuongeza mishahara kwa mwaka huu, Rais Kikwete alisema kulikuwa na
mjadala mkali baina ya wafadhili waliodai nyongeza ni kubwa mno.
“Ni kweli mapato yetu ni madogo lakini kwa kuwa
mishahara ni midogo, lazima tuendelee kuongeza, hata hicho kidogo lazima
ukitoe ili uijenge ile nafuu, alisema bila kutaja kiwango
kitakachoongezwa.
“Hata sasa kumekuwa na ubishi mkali kati ya Wizara
ya Utumishi na Hazina kuhusu nyongeza ya mwaka huu iwe mpaka kiasi
gani, nikaingilia kati nikakubaliana na utumishi, Hazina walikuwa
wanataka ipungue kidogo,” alisema.
Walimu na shemeji yao
Suala la mshahara lilijitokeza kwa namna nyingine
kwenye maandamano ya wafanyakazi pale walimu walipoamua kusimama mbele
ya jukwaa kuu na kumweleza Rais Kikwete ambaye walimtaja kama shemeji
yao, kwamba hawajapata mshahara wa Aprili wakimtaka aingilie kati.
“Shemeji, shemeji, shemeji, hatujapata mishahara yetu ya Aprili, tunaomba utusaidie,” walitoa ujumbe huo kwa njia ya wimbo.
Tofauti na wafanyakazi wengine ambao walipita mbele ya mgeni
rasmi bila kusimama, walimu walisimama kwa dakika moja kuhakikisha
ujumbe huo unamfikia.
Wakati hayo yakitokea, Rais Kikwete na viongozi
wengine walikuwa wakicheka huku wakiwaangalia walimu hao waliokuwa
wakiendelea kuimba wimbo huo.
Ajira kwa wageni
Rais Kikwete aliagiza yafanyike marekebisho kwenye
sheria ya vibali vya ajira ili kudhibiti ongezeko la wafanyakazi wa
kigeni nchini ambao wanafanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.
Aliagiza hatua hiyo itekelezwe haraka hata ikibidi
kwa kupeleka bungeni hati ya dharura ili kuhakikisha jambo hilo
linaanza mara moja.
Malalamiko ya Tucta
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Wafanyakazi Tanzania
(Tucta), Nicholas Mgaya alisema pamoja na ongezeko la mishahara
kufanyika kila mwaka, limekuwa dogo mno kiasi cha kushindwa kufikiwa
kima cha chini ya mshahara kinachotakiwa.
Alisema kwa upande wa sekta binafsi, Serikali
imeongeza mshahara kutoka Sh100,000 hadi Sh450,000 mwaka jana, huku
sekta ya kilimo ikiwa ya mwisho kwa kuwa na kiwango cha chini zaidi.
“Hali hii imesababisha kuwapo kwa upungufu mkubwa
wa wafanyakazi mashambani na hivyo kuathiri uzalishaji wa mazao,”
alisema na kuongeza:
“Tunapenda kuikumbusha Serikali kwamba kumlipa
mfanyakazi mshahara unaokidhi mahitaji muhimu ya maisha siyo jambo la
fadhila, bali ni mojawapo ya haki za msingi za binadamu zinazosisitizwa
na jumuiya za kimataifa.”
Tanga
Mkuu wa Wilaya ya Pangani, Hafsa Mtassiwa alisema
Serikali inatambua changamoto zinazowakabili wafanyakazi zikiwamo za
kodi ya mishahara kuwa juu na kwamba inazifanyia kazi.
Mbeya
Mratibu wa maadhimisho hayo mkoani Mbeya, Joseph
Sayo ameiomba Serikali iache kuwanyonya wafanyakazi na kuwa mwajiri
msumbufu kuliko wengine nchini.
“Serikali inadaiwa na wafanyakazi fedha nyingi na
pia inawakopa wafanyakazi kwa njia mbalimbali zikiwamo za kupitia kwenye
mifuko ya hifadhi za jamii na kushindwa kurudisha kwa wakati,” alisema.
Arusha
Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo amewataka
waajiri kufuata sheria na taratibu za kazi katika kuhakikisha kuwa
wanawalipa wafanyakazi wao stahili zao ikiwamo nyongeza ya mishahara,
kupandishwa vyeo na motisha kwa wanaostahili.
Geita
Wafanyakazi mkoani Geita, wameilalamikia Serikali
kwa kushindwa kutekeleza ahadi mbalimbali ilizotoa kuboresha maisha yao,
hivyo kulazimika kufanya kazi kwenye mazingira magumu.
Morogoro
Mratibu wa Tucta Mkoa wa Morogoro, Charles Luvunzu
amesema rushwa na ukosefu wa uadilifu ni miongoni mwa mambo
yanayokiukwa na waajiri wengi licha ya vyama vya wafanyakazi kuyapigia
kelele.
Shinyanga
Tucta imewataka waajiri kuacha tabia ya kuwafukuza
wafanyakazi kama kuku. Imeshauri wakae meza moja kujadiliana ili
kutatua matatizo yanayowakabili sehemu za kazi.
Mwanza
Mratibu wa Tucta Mwanza, Evarist Mwalongo ameutaka uongozi wa
mkoa kuwachukulia hatua za kisheria waajiri wasiofuata sheria za kazi
huku akiitaka Serikali kubadilisha sheria ya mifuko ya hifadhi ya jamii,
ili itoe mafao mazuri kwa wastaafu na kiwango cha kodi kwenye mshahara
kipungue hadi asilimia moja.
Mara
Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Mara, John Henjewelle
amewaagiza waajiri kuwalipa wafanyakazi masilahi yao kwa wakati ili
kuepusha migogoro ya mara kwa mara kazini.
Chanzo: Mwananchi
0 comments:
Post a Comment