WAKATI
Chama Cha Mapinduzi (CCM) kikiendelea kumwandama kwa kejeli Mwenyekiti
wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba, mmoja wa
makamishna wa tume hiyo naye ameonja ‘joto ya jiwe’ kwenye kamati za
Bunge Maalumu la Katiba.
Mjumbe huyo ni Al- Shymaa Kweigyir (mbunge), ambaye jana
alishulutishwa na wajumbe wenzake wa CCM kupiga kura ya wazi ili
kukataa kuafiki ibara ya kwanza ya sura ya kwanza ya rasimu.
Kwa mujibu wa chanzo chetu, Kwegyir alikumbana na zahama hiyo wakati
wa kupiga kura katika kamati yake namba 12 inayoongozwa na Paul Kimiti.
Ingawa Kimiti ambaye amekuwa mgumu kutoa taarifa za kamati yake kwa
waandishi hakupatikana kuthibitisha tukio hilo, gazeti hili lilidokezwa
kuwa Kwegyir aliomba kupiga kura ya siri ambayo CCM wanaikwepa akitaka
kulinda uhuru wake kwa sababu ana masilahi na tume.
Kwa kawaida, Kwegyir kama mmoja wa wajumbe wa tume iliyoandaa rasimu lazima angepiga kura ya kuunga mkono mapendekezo yao.
Kamati namba 12 ina wajumbe 53 ambapo 36 wanatoka Bara na 17 Zanzibar
na ili kufikia theluthi mbili ya kura kwa Bara zilitakiwa 24 na
Zanzibar 12.
Kwa mujibu wa chanzo hicho, zilipopigwa kura za kuamua ibara ya
kwanza ya sura ya kwanza, theluthi mbili haikupatikana kwa pande zote,
ndipo CCM wakaaza kusaka ‘mchawi’ anayekwamisha.
Tanzania Daima lilidokezwa kuwa baadhi ya wajumbe wa CCM wakiwemo
mawaziri walianza kumzomea Kwegyir wakimwita msaliti kwa sababu ndiye
alipiga kura ya siri tofauti na msimamo wa chama chao.
“Hali hiyo ilimkasirisha Kwegyir hadi akafikia hatua ya kutoa
machozi, akishangaa kuona ananyimwa haki yake wakati kanuni zinaruhusu
mjumbe kupiga kura aitakayo kati ya wazi na siri.
“Baada ya hali kuwa mbaya, wajumbe wa upinzani waliingilia kati
wakipinga kitendo hicho ingawa CCM waliendelea kumwandama wakitaka
atamke wasikie kama anakubali pendekezo la ibara hiyo au hapana,”
alisema msiri wetu.
Hata alipolazimishwa kupiga kura ya wazi kwa kutamka, inadaiwa kuwa
Kwegyir alilikubali pendekezo la tume kuhusu muundo wa muungano wa
serikali tatu.
Mjumbe Edward Lowassa (Mbunge wa Monduli) ndiye anadaiwa kuokoa
jahazi hilo baada ya kuingilia kati na kuwasihi wajumbe wenzake kutulia,
hivyo shughuli ya upigaji kura kusimama kwa muda.
Miongoni mwa viongozi wakubwa wa CCM wanaounda kamati hiyo ni, Prof.
Anna Tibaijuka (waziri), Pandu Ameir Kificho (Spika Zanzibar), Binilith
Mahenge (naibu waziri) na Aden Rage (mbunge).
Wapo pia Michael Laizer (mbunge), Ahmed Shabiby (mbunge), Amos
Makalla (naibu waziri), Seleman Jaffo (mbunge), Henry Shekifu (mbunge na
mwenyekiti wa CCM Tanga), Jesca Msambatavangu (mjumbe na mwenyekiti wa
CCM Iringa) na wengine.
Theluthi mbili Zanzibar utata
Theluthi mbili ya kuamua ibara na sura za rasimu ya Katiba imekuwa
kikwazo kwa kamati nyingi za Bunge Maalumu la Katiba hususan upande wa
wajumbe wa Zanzibar.
Hali hiyo ilijitokeza jana wakati kamati hizo 12 zilipopiga kura ya
kuamua vifungu vya ibara za sura ya kwanza na sita huku ibara ya kwanza
inayopendekeza muundo wa serikali tatu ikileta mgawanyiko.
Katika ibara ya kwanza ya sura ya kwanza (1), rasimu inapendekeza
kuwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni Nchi na Shirikisho lenye mamlaka
kamili ambalo limetokana na Jamhuri ya Tanganyika na Jamhuri ya Watu wa
Zanzibar, ambazo kabla ya hati ya makubaliano ya muungano ya mwaka
1964, zilikuwa nchini huru.
Wakizungumza na waandishi wa habari jana, baadhi ya wenyeviti wa
kamati hizo walisema kuwa licha ya wajumbe kuafikiana katika baadhi ya
ibara, lakini katika suala hilo la shirikisho waligawanyika kulingana na
pande za muungano.
Hadi jana mchana hakuna kamati hata moja iliyokuwa imepata theluthi
mbili kwa pande zote za muungano katika suala hilo la shirikisho ambapo
wajumbe wengi wa CCM wanataka pendekezo hilo lifutwe kwa madai inakwenda
kinyume cha hati ya makubaliano ya Muungano.
Ili kufikia theluthi mbili kwenye kamati yenye wajumbe 52 au 53,
upande wa Tanzania Bara wenye wajumbe kati ya 33 hadi 37 unatakiwa
kupata kura zaidi ya 23 za ndiyo na upande wa Zanzibar wenye wajumbe
kati ya 15 hadi 19 zinahitajika kupata zaidi ya 10.
Kwa upande wa Bara ni rahisi kwa CCM kupata theluthi mbili kwa sababu
ina wajumbe kati ya 23 hadi 28 kila kamati bila kutegemea za wajumbe wa
kundi la kuteuliwa lakini kwa Zanzibar ni vigumu kwani idadi ya wajumbe
wake inalingana na ile ya CUF.
Kutokana na msimamo wa vyama hivyo kuwa tofauti katika suala la
muundo wa muungano ni vigumu kupata theluthi hiyo ya kura kwa upande wa
Zanzibar.
Ibara ya pili kuhusu eneo la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na ile
ya tano kuhusu tunu za taifa zilizua ubishano mkali katika kamati nyingi
kiasi cha baadhi ya wajumbe kuleta majedwali ya marekebisho wakiongeza
na kupungua baadhi ya vitu.
Mwenyekiti wa kamati namba moja, Ummy Mwalimu, alisema kuwa katika
sura ya kwanza yenye ibara tisa, ni ibara mbili za sita na tisa ambazo
zilipata theluthi mbili ya kukubalika kwa pande zote.
Mwenyekiti wa kamati namba tano, Hamad Rashid Mohammed, alisema kwa
sura ya kwanza, ibara ya pili, tano na saba zilikataliwa kwa theluthi
mbili huku ibara ya kwanza ikikosa idadi hiyo ya kura kwa upande wa
Bara.
Naye Anna Abdallah, mwenyekiti wa kamati namba 10, alisema
hawakukubaliana kwa ibara nyingi na hivyo kufanya theluthi mbili
kushindikana hasa upande wa Zanzibar.
Hali kama hiyo ya wajumbe kutofautiana kuhusu muundo wa muungano
ilijitokeza pia kwa kamati namba 11 inayoongozwa na Anne Killango
Malecela na nane ya Job Ndugai, ambazo wajumbe wake walitarajiwa kupiga
kura jana jioni.
Chanzo: Tanzania Daima
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:
Post a Comment