Mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Godfrey Mgimwa
Pingamzi lililowekwa juzi na mgombea wa Chadema dhidi ya mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM, Godfrey Mgimwa limetupiliwa mbali baada ya mgombea huyo wa CCM kuwasilisha nyaraka mbalimbali zinazothibitisha uraia wake kwa msimamizi wa uchaguzi Jimbo la Kalenga, Pudenciana Kisaka.
 
Msimamizi wa uchaguzi, Pundenciana aliliambia gazeti hili jana kuwa, alipokea vielelezo kutoka kwa mgombea wa CCM vinavyothibitisha uraia wake baada ya kumwandikia barua ya kumtaka kufanya hivyo.
Alisema kwa mujibu wa sheria ya uchaguzi, mgombea anapowekewa pingamizi anaarifiwa kwa barua, akitakiwa kuwasilisha vielelezo huku aliyeweka pingamizi akitakiwa kuwasilisha vielelezo vinavyomtaka athibitishe madai yake.
“Mgombea wa CCM Mgimwa alileta vielelezo vyake na wa Chadema ameleta barua lakini hakuwasilisha vielelezo alivyokuwa amedaiwa, kwa hatua hiyo nimeshatoa majibu ya madai yao na hayo mnaweza kuyapata kwa wagombea wenyewe,”alisema.
Akithibitisha kutolewa kwa uamuzi huo, Mratibu wa Chadema, Frank Mwaisumbi alisema, “Ni kweli tumepata majibu ya mgombea wa CCM kupitia kwa msimamizi wa uchaguzi, hatujaridhika nayo,” alisema.
Mgombea wa Chadema aliwasilisha pingamizi lake Februari 19 akitoa madai matano, likiwamo la kuwa na shaka na uraia wa mgombea wa CCM walipodai si Mtanzania.
Akizungumza na waandishi, mgombea ubunge kupitia CCM, Godfrey Mgimwa alisema ameshangazwa na tuhuma za kudaiwa yeye si Mtanzania wakati amezaliwa katika Hospitali ya Mkoa wa Iringa na kusoma Shule ya Msingi Wilolesi iliyopo mkoani hapa.
Huku akionyesha vielelezo vya kuthibitisha uraia wake, Mgimwa ambaye pia ni mtoto wa aliyekuwa Mbunge wa Jimbo la Kalenga, Marehemu Dk William Mgimwa alisema, asingekuwa raia wa Tanzania asingekuwa na hati ya kusafiria ya Tanzania kwa kuwa nchi hii ina uraia wa nchi mmoja.
Mgimwa alifafanua kuwa, baada ya kutoka Shule ya Msingi Wiloles ya mjini hapa alijiunga na Shule ya Sekondari ya Azania ya Dar es Salaam na baadaye alikwenda St Marys kabla ya kujiunga na elimu ya chuo ngazi ya Shahada ya Kwanza Uingereza.
Kwa upande wake Kaimu Katibu wa CCM mkoani hapa, Hassan Mtenga alisema ameshangazwa na taarifa hizo za Chadema kumwekea pingamizi mgombea huyo akidai si za kweli na wameonyesha hofu dhidi ya mgombea wao.
Naye Katibu wa Iringa Vijijini, Amina Mahimbo alikanusha kauli ya Chadema kuwa wanachama 25 waliomdhamini mgombea wa CCM si wazawa wa Kalenga na kusema wote walitoka katika jimbo hilo ambao ni viongozi na wanachama wa Jimbo la Kalenga. Uchaguzi mdogo wa Jimbo la Kalenga mkoani hapa, unatarajiwa kufanyika Machi 16 ukiwashirikisha wagombea kutoka vyama vitatu.
Mwananchi 
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI

0 comments:

 
Top