Marekani imetoa ripoti inayozungumzia usafirishaji wa binadamu
ya mwaka 2013, huku ikiitaja Tanzania kuwa kinara wa kunyanyasa
wasichana, kuwatumikisha katika ngono na usafirishaji wa binadamu.
Ripoti hiyo iliyotolewa na idara ya nchi hiyo
inayohusika na diplomasia (US Department of State, Diplomacy in Action),
pia inaitaja Tanzania kuwa ni kitovu cha njia ya kusafirisha wanawake,
watoto na wanaume ambao hutumikishwa kwenye kazi za mashambani na
biashara ya ngono.
Ripoti hiyo iliyozinduliwa Julai mwaka huu na
Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Seneta John Kerry inaweka bayana
kwamba biashara ya usafirishaji wa binadamu hufanywa na baadhi ya ndugu
na marafiki ambao hutoa ahadi kwa wahusika kwamba wanakwenda kuwasomesha
au kuwatafutia ajira nzuri mijini.
“Unyonyaji wa wasichana wadogo na utumikishaji
majumbani ndilo tatizo linaloongoza, ingawa kesi za watoto kusafirishwa
kwa ajili ya biashara ya ngono katika mpaka wa Tanzania na Kenya
zinaongezeka. Pia, wasichana wananyonywa kwenye maeneo ya utalii,”
inasema sehemu ya ripoti hiyo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, watoto kutoka Burundi
na Kenya, watu wazima kutoka Bangladesh, Nepal, Yemen na India
wanatumikishwa kufanya kazi kwenye sekta za kilimo, madini na majumbani
nchini Tanzania.
“Baadhi ya raia kutoka nchi jirani huingia
Tanzania kwa hiari yao, lakini hulazimishwa kufanya kazi majumbani kabla
ya kupelekwa kutumikishwa kwenye biashara ya ngono Afrika Kusini, Ulaya
na Mashariki ya Kati,” inaeleza.
Naibu Waziri wa Katiba na Sheria, Angela Kairuki
alimtaka mwandishi kumtumia ripoti hiyo kwa njia ya baruapepe ili aweze
kuisoma na kuitolea maelezo.
Alipotafutwa siku ya pili, alisema kuwa ameipokea
na kuikabidhi ofisi ya Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka (DPP) ili ifanyiwe
kazi na baadaye kutoa majibu.
“Ripoti niliipata nikaikabidhi ofisi ya DPP kwa
kuwa wao ndio wanaoweza kuitolea maelezo baada ya kuisoma. Maoni yangu
lazima yawe ya kitaalamu siwezi kusema bila kupata taarifa kutoka kwao,”
alisema.
Lawama kwa Serikali
Ripoti hiyo inaitupia lawama Tanzania kwa kutokuwa
na sheria thabiti za kupambana na biashara haramu ya kusafirisha
binadamu, huku ikitolea mfano namna ilivyoshindwa kuwasaidia raia wake
waliokuwa wakinyanyaswa nje ya nchi.
“Kamati ya Serikali ya kupambana na usafirishaji
binadamu, haijachukua hatua za kutosha katika kutekeleza mpango mkakati
wa kupambana na vitendo hivyo,” inaeleza na kuongeza kuwa:
TOA MAONI YAKO HAPA CHINI
“Serikali imeshindwa kutenga fedha kwa ajili ya kuwasaidia
waathirika wa usafirishaji wa binadamu kama ambavyo inaelekezwa kwenye
sheria ya kudhibiti biashara hiyo ya 2008.”
Taarifa hiyo inaitaka Tanzania kuongeza nguvu
katika kutekeleza sheria ya kudhibiti biashara ya kusafirisha binadamu
ya 2008 kwa kuwakamata na kuwashtaki wahusika wote, lakini ikaikosoa kwa
kusema inatoa adhabu ndogo kwa mtu anayebainika kufanya makosa, ikiwa
ni pamoja na kumhukumu kwenda jela miaka 10, kulipa faini au vyote
viwili kwa pamoja.
“Sheria hiyo haifanani na nyingine kama za mtu
anayepatikana na kosa la kubaka au kufanya kosa jingine la jinai.
Mamlaka imesema ina kesi nne inazozichunguza, saba zipo mahakamani toka
mwaka jana, zikiwepo mbili mpya,” inasema ripoti.
Pia, Serikali ya Tanzania imelaumiwa kwa kushindwa
kuripoti maendeleo ya uchunguzi wa maofisa wake waliotuhumiwa
kujihusisha na biashara ya usafirishaji binadamu.
LHRC na TGNP
Mkurugenzi wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu
(LHRC), Dk Hellen Kijo-Bisimba alisema tatizo la usafirishaji wa
binadamu pia linachangiwa na wasichana kuwa na tamaa ya maisha mazuri,
hivyo kukubali ahadi ambazo hupewa kwamba wanapelekwa kusoma,
wasifahamu wanarubuniwa.
“Wengi wanatamani kwenda ‘majuu’ wakidhani
watapata elimu, lakini baadaye wanaingizwa kwenye vitendo
vinavyowafedhehesha na kuwafanya wakate tamaa kabisa,” alisema.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Jinsia
Tanzania (TGNP), Usu Mallya alisema katika siku za karibuni kumekuwa na
ongezeko kubwa la vitendo vya unyanyasaji dhidi ya wasichana
waliochukuliwa vijijini kwenda mijini kufanya kazi.
Alisema pamoja na tatizo hilo kuongezeka hapa
nchini, hakuna tafiti za kutosha ambazo zimefanywa na wadau mbalimbali
kuonyesha madhara yaliyopatikana hadi sasa.
“Katika siku za usoni kumekuwa na ongezeko kubwa
la vitendo vya kunyimwa chakula, kupigwa na kufukuzwa kazi huku
wasichana wengine wakitumika kwenye biashara ya ngono,” alisema na
kuongeza:
“Ripoti hii isiishie kwenye makabrasha bali ifanyiwe kazi ili jamii yote ijue kuwa hili ni tatizo.”
Ripoti hiyo inabainisha kuwa watu 47,000 pekee
ndio walioweza kuokolewa mwaka jana kutoka kwenye mazingira ya
utumikishwaji kati ya milioni 27 waliopo katika hali hiyo duniani.
Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi 44 ambazo zinajaribu kupambana na biashara hiyo, lakini hali inazidi kuwa mbaya zaidi.
Mwananchi
Tanzania imetajwa kuwa ni miongoni mwa nchi 44 ambazo zinajaribu kupambana na biashara hiyo, lakini hali inazidi kuwa mbaya zaidi.
Mwananchi
0 comments:
Post a Comment